Umuhimu wa kujizatiti katika kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani hata katika maeneo ya vita; kuheshimu na kuthamini maisha ya binadamu kuwa ni matakatifu na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; uhuru wa kidini na huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora ni kati ya mada tete zilizojadiliwa na Tume ya pamoja kati ya Rabi mkuu na Tume ya Vatican ya Mahusiano ya kidini na Wayahudi, katika mkutano wao uluiohitimishwa hivi karibuni mjini Roma.
Tamko la pamoja na wajumbe wa Tume hii limetiwa mkwaju na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani kwa niaba ya Vatican na kwa niaba ya Wayahudi, Rabi David Rosen. Viongozi hawa wa kidini wanatambua mchango mkubwa ambao unaweza kutolewa na dini mbali mbali katika medani za kimataifa kwa kujikita katika haki, amani, maridhiano sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Utakatifu wa maisha ya binadamu, uhuru wa dhamiri pamoja na kuheshimu na kuthamini tofauti zinazojitokeza baina ya waamini wa dini mbali mbali kama chachu ya umoja na mshikamano badala ya kuwa ni chanzo cha kinzani, misigano na hata vita.
Ikumbukwe kwamba, binadamu wote ni sawa kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Katika changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika uso wa dunia, kuna haja kwa dini mbali mbali duniani kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Viongozi wa dini wajizatiti kuwalinda na kuwatetea wanyonge na maskini ndani ya jamii kwani hili ni kundi ambalo halina sauti hata kidogo.
Waamini wa dini mbali mbali wanatakiwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu na kwamba, hakuna kitendo chochote kinachoweza kuhalalisha vita, nyanyaso na ukatili dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Ni wajibu wa viongozi wa kidini kulaani kwa nguvu zote wale wote wanaotumia jina la Mungu kuhalalisha vitendo viovu kama vile mashambulizi ya kigaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba, dini zinapaswa kuwa ni chemchemi ya umoja, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa na wala si vinginevyo.
Wajumbe wa tume hii, wameungana kwa kauli moja kulaani vitendo vya kigaidi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Hata katika nchi za Kiislam, tofauti za kidini na kiimani zisiwe ni sababu ya kinzani na mipasuko ya kijamii, bali wote kwa pamoja wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utakatifu wa maisha ya binadamu, utu na heshima yake. Waamini wa dini mbali mbali wanahamasishwa kushikamana ili kujenga familia kubwa ya binadamu, ili kuziwezesha fadhili na kweli kukutana; haki na amani kubusiana, ili kweli iweze kuchipua katika nchi na haki kuchungulia kutoka mbinguni kama anavyosema Mzaburi.
Wajumbe wa tume hii ya pamoja wameonesha umuhimu wa kuwafunda vijana wa kizazi kipya katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, ili kukuza na kudumisha haki, amani, maridhiano pamoja na kuheshimiana. Maeneo na nyumba za Ibada zinapaswa kuheshimiwa kwani zinafumbata historia ya maisha ya waamini wa dini husika. Historia ya Maandiko Matakatifu, Imani na Siasa za nchi husika hazina budi kuheshimiwa kwani kuna uhusiano mkubwa katika historia na imani ya watu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni