Ndugu yangu, twasikia kwa mbali sauti ya mtu aliyaye nyikani na huyu si mwingine bali ni Yohana Mbatizaji, sauti hii ya mtu aliyaye nyikani yatutangazia, kutimia kwa wokovu wetu kama ilivyo kwisha nenwa na Manabii. Hii ni sauti ya maandalizi, maandalizi ya kumpokea mwokozi. Sauti hii yatuambia mwokozi amekaribia na kipindi cha kumsubiri kimekaribia, kipichi hicho ni kipindi cha majilio. Ni kipindi cha matumaini kwani mwokozi yu karibu, na ukamilifu wa ahadi ya Bwana unakaribia, na furaha ya mwanadamu inaongezeka.
Habari hizi za ujio wa Kristo, ni habari zilizokwisha nenwa na manabii toka enzi. na kuzaliwa kwa Yesu kwadhihirisha na kudhibisha utimilifu huu, yaani utimilifu wa ahadi ya Mungu, ukweli wa manabii na tabiri zao. Hebu kwa ufupi tangalie baadhi ya tabiri hizo za kinabii, na utimilifu wake, ili wote tupate kuamini ya kuwa Kristo ni Bwana, na kila goti litapigwa kwa ajili yake.
Yapata miaka 750, KK. Nabii Isaya alinena maneno haya; “Haya basi tazama msichana Bikira atachukuwa Mimba na atajifungua mtoto wa Kiume na kumwita jina lake Emmanueli. (Rej. Is 7:14), unabii huu unatimia sasa katika kuzaliwa Bwana, kama Luka Mwinjili anavotuambia; Siku yake ya kujifungua ikawadia akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo zake za kitoto akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni (Lk 1:6-7).
Mnamo mwaka wa 587-542, KK, Nabii Mika anatuandikia utabiri mwingine, kuhusu kuzaliwa kwa Yesu. Kwamba atazaliwa wapi na katika mji gani’ kwani anasema ‘ mwenyezi Mungu, Mungu asema; “lakini wewe Bethlehemu katika Efratha, wewe ni mdogo tu kati ya jamii ya Yuda, lakini kwako kutatoka mtawala atakayetawala juu ya Israeli kwa niaba yangu (Mik 5:1ff.) Utabiri huu unatimia katika maandiko ya Mwinjili Luka anayetuambia; “alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yudea alikozaliwa mfalme Daudi , walipokuwa huko siku yake ya kujifungua ikawadia. (Rej. Lk 2:4-7. Yesu anazaliwa kweli Bethlehem kama ilivyonenwa na nabii Mika.
Mnamo mwaka wa 742 KK, Nabii Isaya anaendelea kutabiri ; “maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto wa kiume, naye atapewa mamlaka ya kutawala (Rejea Is 9:6) Unabii huu unatimia kama Luka mwinjili atuandikiavyo.. kwa maana leo hii katika mji wa Daudi , amezaliwa mwokozi kwa ajili yetu ndiye Kristo Bwana. (Rej. Lk 2:11-12).
Unabii mwingine ni huu; “Tazama namtuma mjumbe wangu na ataindaa njia kabla yangu Is 40:3, utabiri huu ulinenwa na Nabii Isaya yapata miaka 700 KK, na unatimia kwa Sauti ya Yohane mbatizaji aliyehubiri ujio wa Bwana, akisema Sauti ya mtu aliaye jangwani, mtayarishieni Bwana njia yake, nyosheni barabara zake, na akaendelea kuhubiri watu watubu na kubatizwa, ili Bwana awasemehe dhambi zao. (Mk 1:3-4). Na Yesu alipokuja, Yohane Mbatizaji akamtambulisha kwetu kwa maneno haya..” Huyu ndiye mwanakondoo wa Mungu, aondoaye dhambi za ulimwengu. Huyu ndiye nilieongea juu yake niliposema ‘ baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu kuliko mimi. (Rej. Yn 1:29-30.) Yohane Mbatizaji anakuwa mmojawapo wa manabii wanao hubiri katika ukaribu sana ujio wa Kristo. Yohani mbatizaji ndiye Sauti ya mtu aliaye nyikani, aliyenenwa na nabii Isaya Takribani miaka 720 KK.
Ndugu yangu sasa utabiri wa manabii umetimia, malaika anatumwa kwa msichana Bikira na anampa habari ya kuzaliwa Bwana, naye huyu Bikira anajibu ‘mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe ulivyonena Lk1:38. Hivyo hili ni tukio kubwa na la ajabu kuwahi kutokea Dunia hii, ambapo mwana wa Mungu anajivika ubinadamu wetu katika tumbo la Mama Bikira Maria, na hivyo tunaona utimilifu wa wazo la Mungu katika kumkomboa mwanadamu, kwani toka kuumbwa kwa ulimwengu na kwa anguko la kosa la Adamu na Hawa la kutotii, Mungu alianza kazi ya kumkomboa mwanadamu hatua kwa hatua, na hatua hii inafikia utimilifu wake katika Yesu. Kwa kuzaliwa Yesu tunatambua huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu, na kupitia Yesu wote tunafanyika wana wa Mungu na waridhi wa ufalme wa mbinguni. Kwa jambo hili kubwa tumrudishie Mungu sifa na shukrani.
Kipindi hiki cha majilio ni kipindi muhimu cha kuangalia na kuchunguza ndani ya mioyo yetu na kuona tena ni kwa namna gani tusimamapo mbele ya Mungu. Hivyo twatakiwa kumrudishia Mungu sifa na shukrani kwa kuishi ki- ukweli na kiualisia kama wafuasi wa kweli wa Kristo, na kama hatujafanya hivyo wakati ni sasa wa kubatilisha mioyo yetu na kuacha ubaridi wa Imani, na mengine yanayofanana na hayo; ili kupata kumgeukia Bwana na kuishi ukweli katika njia iendayo mbinguni. Mungu anatuita tuyafanye haya leo, na huku ndiko kuitikia mwito wa sauti ya Yehoni mbatizaji, asemayo; “Tubuni, muache dhambi zenu, mmgeukie Mungu; kwa maana Ufalme wa mbinguni umekaribia.
Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi wako Padre, Agapiti Amani, ALCP. OSS
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni