Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Jarida la “Tertio” linalomilikiwa na kuchapishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji, anapembua kwa namna ya pekee kabisa: matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; mchango na dhamana ya waamini walei; matatizo, fursa na changamoto za vijana wa kizazi kipya pamoja na changamoto za Umoja wa Ulaya. Baba Mtakatifu anagusia pia dhana ya Sinodi kama mchakato wa maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Baba Mtakatifu anasema, vyombo vya mawasiliano ya jamii vina dhamana na wajibu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya watu: kiroho na kimwili, mwishoni, Baba Mtakatifu kama mchungaji mwema, anatoa ushauri makini kwa Wakleri katika maisha na utume wao ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa wale wote wanaokimbilia na kutaka kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao.
Baba Mtakatifu anasema, kuna hatari kubwa ya kung’oa dini katika maisha ya hadhara ingawa mambo haya mawili yanapaswa kutekelezwa kwa uangalifu mkubwa bila ya kuchanganya mambo. Pale ambapo Serikali inajiondoa kabisa kwa masuala ya kidini ni hatari sana kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu. Kutambua na kuthamini uwepo wa Mungu katika maisha ya watu ni cheche zinazoiwezesha jamii kuthamini utu na heshima ya binadamu. Sera na siasa zisizo thamini utu na heshima ya binadamu zina madhara makubwa katika asili na sehemu kubwa ya maisha ya binadamu.
Baba Mtakatifu anasema, vita, mashambulizi ya kigaidi, misimamo mikali ya kidini na kiimani ni mambo ambayo yanasigana kimsingi na lengo kuu la dini yoyote ile duniani. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mungu ni asili ya maisha, wema na utakatifu na kamwe hawezi kuwa ni chanzo cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ni jambo lisilokubalika kuanzisha vita kwa jina la Mwenyezi Mungu au dini yoyote ile duniani. Kutokana na ukweli huu vitendo vyote vya kigaidi na vita havina mahusiano yoyote yale na dini, kile kinachotendeka na kusikika kwa watu ni kudhalilisha ukweli na misingi ya dini duniani na kwamba, hakuna sababu msingi ya kuweza kuhalalisha vitendo hivi vinavyokwenda kinyume cha utu, maisha na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila dini ina waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani, hata Wakristo kuna wale wenye imani kali ya Kikristo! Haya ni makundi ambayo yamedhohofisha dini zao na hivyo kuwa ni chanzo cha kinzani, migawanyiko na mipasuko ya kijumuiya na matokeo yake ni vita!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bara la Ulaya linakabiliwa na changamoto ya uongozi makini, utakaosaidia kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya raia wake. Imepita takribani miaka 100 tangu kuibuka kwa Vita kuu ya Kwanza ya Dunia iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, lakini hadi leo hii, bado watu ni wagumu kujifunza kuhusu madhara ya vita, ndiyo maana hata leo hii kuna mataifa mengi Barani Ulaya yako kwenye kinzani na mipasuko ya kijamii, wanaoteseka zaidi ni maskini na raia wa kawaida.
Viongozi wengi wa Ulaya wanakosa ujasiri wa kusimamia maamuzi yao, kwani ni wale wale wanaopinga vita kwa maneno, lakini wa kwanza kutengeneza na kufanya biashara haramu ya silaha ambazo zimekuwa ni chanzo kikuu cha maafa na mateso ya watu wasiokuwa na hatia. Hii ni damu ya watu wasiokuwa na hatia inayoendelea kumwagika sehemu mbali mbali za dunia! Bara la Ulaya linawahitaji watu jasiri na makini katika maamuzi na matendo yao! Hawa ni kama akina Schumman, De Gasper na Adenauer, waasisi wa Umoja wa Ulaya, waliosimama kidete kupinga vita, kumbe, Bara la Ulaya linahitaji viongozi mashuhuri na wajasiri watakaosaidia kusongesha mbele mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu!
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, dhana ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni cheche zilizoanzishwa na Mwenyeheri Paulo VI, zikavaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II na kwa upande wake, akaongeza ari, kasi na mwendo zaidi, ili kuwawezesha waamini kutafakari na kumwilisha mambo msingi ya imani yanayofumbatwa katika huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.
Maadhimisho ya Mwaka wa huruma ya Mungu ni tukio ambalo limekuwa na mafanikio makubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kwa watu kutambua na kuguswa na huruma ya Mungu katika maisha yao, changamoto kwa sasa ni kuendelea kuwasha moto wa huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu duniani, kwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Waamini wengi wamejipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, wakaonja upendo wa Mungu kwa njia ya matendo ya huruma na rehema zilizotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka wa huruma ya Mungu. Waamini kwa mara nyingine tena wanakumbushwa kwamba, Jina la Mungu ni huruma na haki ya Mungu ni huruma yake inayofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Dhana ya Sinodi” katika maisha na utume wa Kanisa inapata chimbuko lake katika maisha ya kijumuiya kutoka katika ngazi ya chini kabisa kwa kushirikishana karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa katika utofauti wake; umoja wa Kanisa chini ya usimamizi na uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa na utajiri mkubwa na matokeo yake ni Wosia wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo katika familia”, matunda ya sala, tafakari na upembuzi yakinifu uliofanywa na Mababa wa Sinodi kwa muda wa miaka miwili.
Dhana ya Sinodi inaliwezesha Kanisa la Kiulimwengu kusikiliza kwa makini, sauti ya Makanisa mahalia, ili kujenga umoja na kutoa mang’amuzi ya pamoja kama Kanisa la Kristo! Ni mahali pa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, kuheshimiana, kuthamianiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi si mahali pa kutupiana vijembe! Dhana ya Sinodi ni utajiri mkubwa unaofumbatwa katika maisha na utume wa Makanisa ya Kiorthodox.
Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, Jimbo kuu la Cracovia, Poland, hivi karibuni amewataka vijana kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo! Wawe tayari kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake bila woga wala makunyanzi! Kwa vijana wasioamini bado wawe na ujasiri wa kutafuta maana ya maisha kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi bila kwenda pensheni wakiwa na umri wa miaka 20 kutokana na uchovu wa maisha. Vijana wawe na ujasiri wa kuwekeza katika tunu msingi za maisha ya binadamu!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, vyombo vya mawasiliano ya jamii vina dhamana na mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya jamii! Vinaweza kusaidia kuchangia mchakato wa ujenzi wa mawazo bora au kwa kuipotosha jamii, kwani kimsingi vyombo vya mawasiliano ya jamii ni wajenzi wa jamii katika: kufikiri na kutenda; kwa kuelimisha, kufunda na kuburidisha! Lakini vyombo hivi pia vimekuwa ni chanzo cha kuanguka kwa maadili na utu wema! Hii inatokana na matokeo ya dhambi yanayopelekea baadhi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii kutumiwa na baadhi ya watu katika jamii kwa ajili ya mafao binafsi, kwa kuwapaka wengine matope na kuwasifia baadhi kwa kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa! Ni vyombo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu, jambo ambalo ni hatari kabisa kwani linakiuka misingi ya haki, ukweli na uwazi. Kwa bahati mbaya, vyombo vingi vya habari vinataka kuchapisha kashfa na mambo ya udaku, hatari katika ustawi na maendeleo ya binadamu! Wadau katika tasnia ya habari wanapaswa kujielekeza katika mambo msingi ya maisha ya binadamu!
Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kutoa wosia kwa Wakleri kuhakikisha kwamba katika maisha yao wanajenga na kukuza Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, ili kamwe wasijisikie kuwa ni watoto yatima! Wajitahidi kusoma na kulitafakari Neno la Mungu; wajenge utamaduni wa sala inayomwilisha katika uhalisia wa maisha kwa kukutana na Kristo Yesu kati ya maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakleri waoneshe na kumwilisha upendo kwa watu wao bila kuona aibu, kwani watu wa dunia hii wana kiu ya upendo wa kweli na wa dhati katika maisha yao!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni