Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake Jumatano tarehe 7 Desemba 2016 amegusia maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Rushwa Kimataifa inayoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 9 Desemba. Jumuiya ya Kimataifa tarehe 10 Desemba ya kila mwaka inaadhimisha Siku ya Haki Msingi za binadamu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, rushwa ni saratani inayopaswa kushughulikiwa kikamilifu kwa kuanzia kwenye dhamiri ya mtu binafsi; kwa kuwa makini katika maisha ya hadhara hasa yale yanayoonesha kuwa na utata zaidi. Penye rushwa hapo hakuna haki kwani haki hugeuka kuwa ni bidhaa inayoweza kununuliwa sokoni!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote, daima zikiendelea kupyaishwa, ili wote waweze kushirikishwa na kamwe asiwepo mtu awaye yote anayetengwa wala haki zake msingi kunyanyaswa. Baba Mtakatifu anawaombea wadau wote, ili waweze kutekeleza vyema dhamana hii tete katika maisha ya watu wengi duniani. Mwishoni amewakumbusha waamini kwamba, Kipindi cha Majilio ni wakati muafaka wa kufanya hija ya kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu anayekuja katika historia ya maisha yao.
Tarehe 8 Desemba, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria kukingiwa Dhambi ya Asili. Mama huyu awe ni mfano na kielelezo cha maandalizi ya maisha ya ndani, ili kukutana na hatimaye, kumkaribisha Mwana wa Mungu, Uso wa huruma ya Baba, kwa njia ya kusikiliza Neno lake linalomwilishwa katika matendo ya huruma pamoja na sala!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni