Mkutano wa Ukimwi wa Kanisa Katoliki Kimataifa unawaunganisha wataalam na wadau mbali mbali ambao wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa Ukimwi huko Durban, Afrika ya Kusini kuanzia tarehe 15- 17 Julai 2016 ili kujadili na hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa maboresho ya huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi hususan miongoni mwa watoto wadogo katika nchi changa zaidi duniani. Hili ni jopo la wadau wanaofadhili, wanaofanya tafiti na kutoa huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi sehemu mbali mbali za dunia.
Lengo ni kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi ifikapo mwaka 2030, kwani ugonjwa wa Ukimwi ni tishio kwa afya umma wanasema wataalam. Mkutano huu unaongozwa na Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayofumbatwa katika Maandiko Matakatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na huduma ya mapendo kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi. Kanisa linapenda kuwashukuru na kuwapongeza wadau mbali mbali ambao wamekuwa mstari wa mbele katika huduma ya upendo kwa wagonjwa na waathirika wa Virusi vya Ukimwi.
Takwimu zinaonesha kwamba, huduma inayotolewa na Kanisa pamoja na mitandao ya kijamii dhidi ya mapambano ya virusi vya Ukimwi ni muhimu sana na wala haina mbadala. Kanisa linawashukuru wahudumu katika sekta ya afya, wafadhili, watafiti na wadau mbali mbali ambao wamechangia kiasi kwamba, watoto waliofariki kutokana na ugonjwa wa Ukimwi kwa mwaka 2014 walipungua kwa asilimia 41% , yaani hawa ni sawa na watoto 150, 000 ambao wangekuwa wamekwisha kufariki dunia, ikilinganishwa na mwaka 2001.
Maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa watoto wadogo kuanzia mwaka 2000 yamepungua kwa kiasi cha asilimia 58%, lakini idadi ya vijana wa kizazi kipya wanaopata maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi imeongezeka maradufu na kwamba, kuna zaidi ya vijana millioni 2. 6 wanaoishi na virusi vya Ukimwi katika kipindi cha Mwaka 2014. Kuanzia mwaka 2000 dawa za kurefusha maisha zimetolewa kwa watoto zaidi ya millioni 1. 4. Takwimu zinaonesha kwamba, walau asilimia 73% ya wanawake wajawazito duniani wamesaidiwa kupata huduma ya tiba dhidi ya maambukizo kwa watoto wao wachanga.
Haya ni mafanikio makubwa yaliyopatikana kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2009. Kwa mwaka 2013 ni asilimia 42% ya watoto waliozaliwa waliokuwa kwenye hatari ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi, waliweza kupimwa afya zao na kuhudumiwa kikamilifu katika kipindi cha miezi miwili ya kwanza ya maisha yao! Haya ni mafanikio makubwa yaliyochangiwa pia na Kanisa pamoja na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi.
Pamoja na mafanikio yote haya, Shirikisho la Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Mtandao dhidi ya virusi vya Ukimwi duniani pamoja na wadau mbali mbali katika mapambano haya kutoka Afrika ya Kusini wanasema, bado kuna changamoto kubwa na vikwazo vinavyopaswa kupewa ufumbuzi wa kudumu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi duniani: elimu ya kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi; huduma ya dawa za kurefusha maisha kwa waathirika hasa wale wanaoishi vijijini pamoja na msaada wa hali na mali kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi unaoendelea kupukutisha rasilimali watu na nguvu kazi. Kuweka mikakati ya kupunguza vifo vya watoto wadogo kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.
Takwimu zinaonesha kwamba, kwa sasa kuna zaidi watoto millioni 6 wanaofariki dunia kutokana na Ukimwi kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano katika nchi ambazo ziko Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kusini mwa Bara la Asia. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua kikuu duniani, lakini zaidi katika nchi changa duniani. Idadi ya wagonjwa wa Ukimwi wanaopata dawa ya kurefusha maisha imeongezeka kutoka asilimia 14% hadi asilimia 32% kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2014.
Ni watoto 820, 000 kati ya watoto millioni 2.6 wanaopata huduma ya matibabu ya dawa za kurefusha maisha. Hii inatokana na kuchelewesha watoto kupimwa virusi vya Ukimwi na kuanza kupewa matibabu kwa wale wanaogundulika kuwa na virusi vya Ukimwi. Hali hii inachangiwa pia na ukosefu wa vifaa vya huduma na tiba kwa wagonjwa wa Ukimwi katika maeneo mengi duniani. Maboresho ya huduma ya dawa za kurefusha maisha ni muhimu pamoja na kuondokana na unyanyapaa kwa waathirika wa Ukimwi.
Caritas Internationalis pamoja na wadau mbali mbali wanasema, kuanzia sasa hadi kufikia mwaka 2020 kuna haja ya kuwa na uhakika wa rasilimali fedha katika huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi duniani. Kuweka mikakati madhubuti zaidi ya kupambana na maambukizi mapya ya Ukimwi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Ukusanyaji wa takwimu ni muhimu ili kuweza kupima mafanikio na changamoto zilizopo kwa kutumia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari. Kuna haja ya kuwekeza zaidi katika huduma za kijamii kwa kuzijengea familia zilizoathirika kwa Ukimwi uwezo wa kupambana na umaskini, nyanyaso na unyanyapaa.
Vijana wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwani hawa ndio waathirika wakubwa zaidi. Mkakati huu hauna budi kwenda sanjari na huduma ya kupima afya kwa mama wajawazito, watoto wadogo mara tu wanapozaliwa pamoja na kuanza kutoa tiba kwa watoto walioathirika wa virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama zao. Mapambano haya yaelekezwe pia kwenye magonjwa kama vile Kifua kikuu na Malaria.
Wadau wanakaza kusema, kuna haja ya kuendelea kushughulikia kikamilifu mahitaji na changamoto za wagonjwa wa Ukimwi: kiroho na kimwili; kuhamasisha mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya Ukimwi duniani pamoja na kuondokana na unyanyapaa. Kanisa liendelee kushirikiana na wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya Ukimwi pamoja na kutoa huduma makini kwa waathirika kwa kukazia pia maadili na utu wema.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni