0
MAASKOFU 35 wanaounda Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wametoa ujumbe wa Kwaresima kwa 2018, huku wakiwataka waamini wakatoliki wote kuuitikia ujumbe huo kwa moyo wa toba, mageuzi na kushiriki kwa kujitoa zaidi katika uinjilishaji wa nchi kama mwanga na chumvi ya ulimwengu wa Tanzania.
Katika ujumbe huo unaoongozwa na kaulimbiu “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu: Mt.28:19” wamesema kuwa Kwaresima huwaalika wakristo kutumia muda huo kufunga, kufanya toba na kufanya matendo ya huruma kwa wote wenye mahitaji huku wakijitafakari kuhusu uhalisia wa hali yao ya kuwa ni wenye dhambi mbele ya Mungu, ili waweze kufanya toba ya kweli na yenye mageuzi na wongofu katika maisha.
“Hivyo basi, ili kuhakisha kuwa tuna pata majibu ya kweli na yenye kuleta mabadiliko katika nafsi zetu na mahusiano na mashirikiano katika jamii yetu, ujumbe huu wa Kwaresima una lengo la kuwahimiza, kuwahamasisha na hata kuwadai waumini Wakatoliki wote kuuitikia kwa moyo wa toba, mageuzi na kushiriki kwa kujitoa zaidi katika uinjilishaji wa nchi yetu kama mwanga na chumvi ya ulimwengu wa Tanzania” wameeleza.

Upekee wa kwaresima ya 2018
Aidha maaskofu wamesema kuwa kwaresima ya mwaka huu ni kipindi chenye upekee wa aina yake kwa sababu kuu tatu ikiwa nii katika mwaka huu Kanisa Katoliki Tanzania  linaadhimisha na kusherehekea miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, na kilele chake kitakuwa Oktoba 7 Mwaka huu, pia utakuwa ni mwaka wa 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania watoe tamko rasmi kuhusu mwelekeo na hatima ya nchi. Pia mwaka huu ni mwaka wa maandalizi ya utekelezaji wa haki ya msingi ya kidemokrasia ya raia wote ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji  hapo mwakani 2019

Uminyaji wa demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari
Hata hivyo, maaskofu wamesema kuwa shughuli za siasa bado zinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola.  Wamesema kuwa shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa,  kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani, ambayo ni haki ya kila raia, zimekoma mpaka uchaguzi mwingine. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi.
“Vile vile baadhi ya vyombo vya habari vimefungiwa au kusimamishwa kwa muda, na hivyo kupunguza uwigo wa uhuru wa wananchi wa kupata habari, maoni na wa kujieleza. Kufungiwa huku kwa vyombo vya habari kumeenda sambaba na kuminya uhuru wa mahakama na bunge kwa njia ya kuminya haki wabunge na kutowapa nafasi ya mikutano ya hadhara kama haki yao ya msingi ya Kikatiba” wameongeza.

Chapisha Maoni

 
Top