0
Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa mageuzi ya Kiliturujia yaliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, amechapisha barua binafsi inayojulikana kama “Motu Proprio: Magnum Principium” inayobadilisha Sheria za Kanisa namba 838. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Vatican walikazia umuhimu wa Sala ya Liturujia kufahamika vyema na waamini na dhamana hii nyeti wakakabidhiwa Maaskofu Mahalia ili kuhakikisha kwamba, wanachapisha vitabu kwa lugha inayoeleweka na waamini wao.


Vitabu vya Kiliturujia vilipaswa kuhakikiwa na hatimaye, kupitishwa. Kwa miaka mingi Kanisa limetumia lugha ya Kilatini katika maadhimisho ya Liturujia zake. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kusoma alama za nyakati wakaamua kuruhusu maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kufanyika pia hata katika lugha mbali mbali za watu sanjari na lugha ya Kilatini. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican tangu mwanzo walitambua matatizo na changamoto ambazo zingeweza kujitokeza katika kutafsiri vitabu vya Liturujia ya Kanisa ndiyo maana wakakazia umuhimu wa kuwaunganisha vyema waamini wa kila umri na tamaduni ili kufaidi haki yao kufahamu na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa mintarafu Madhehebu ya Kirumi.
Ikumbukwe kwamba, lugha mbali mbali duniani zinaendelea kukua na kubadilika, hali ambayo ingeweza kukinzana na mawazo ambayo yanalenga kurutubisha imani ya Kanisa. Kutokana na changamoto hii, viongozi wa Kanisa wakaifafanua kwa njia ya Sheria za Kanisa na Miongozo kutoka Vatican kwamba, kabla ya Vitabu vya Liturujia havijaanza kutumika katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, havina budi kwanza kabisa kupatiwa idhini na Vatican, kama inavyofafanuliwa na Sheria za Kanisa inayotoa mwongozo unaopaswa kutekelezwa na wote na kwamba, dhamana hii inatekelezwa kwa dhati kabisa na Tume za Liturujia kwa kuzingatia uaminifu wa tafsiri iliyofanywa kwenye vitabu vikuu vya maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Vitabu ya Liturujia ya Kanisa ni chombo muhimu sana cha mawasiliano pamoja na kwamba, kwa waamini hata neon linakuwa ni sehemu ya Fumbo linaloadhimishwa, hasa ikiwa maneno haya yanatoka katika Maandiko Matakatifu, kwani kwa njia hii, Mwenyezi Mungu na Kristo Yesu wanazungumza na waamini kwa njia ya waadhimishaji wa Sala na Mafumbo ya Kanisa wanayowezeshwa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Lengo msingi la tafsiri ya Neno la Mungu na Vitabu vya Liturujia ya Kanisa ni kuwatangazia waamini Neno la Wokovu mintafu utii kwa imani inayoshuhudiwa katika Sala ya Kanisa kwa Kristo Yesu. Ili kuweza kufikia lengo hili kuna haja ya kuhakikisha kwamba, lugha ya watu mahalia inafikisha ujumbe uliokusudiwa, ujumbe ambao Kanisa lilikusudia kuwafikishia waamini kwa njia ya Lugha ya Kilatini.
Kumbe, hapa kinachotiliwa mkazo ni maana ya jumla ya maneno yanayotumika katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa mintarafu Imani ya Kanisa Katoliki. Tafsiri zote za vitabu vya Liturujia ya Kanisa vinapaswa kuakisi uaminifu wa Mafundisho ya Kanisa na wala si kinyume chake. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, katika kipindi cha miaka yote hii tangu baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kumejitokeza matatizo na changamoto kati ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na Sekretarieti kuu ya Vatican. Ili kuendeleza mageuzi ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kwa wakati huu na kwa siku za usoni, kuna haja ya kuwepo na ushirikiano wa karibu sana unaofumbatwa katika kuaminiana, kulinda na kuendeleza kipaji cha ubunifu kati ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na Sekretarieti kuu ya Vatican, hususan Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa ambalo limekabidhiwa dhamana ya kuendeleza Liturujia ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ili kuendeleza mchakato wa upyaisho ya maisha ya kiliturujia inaonekana kwamba, ni vyema sasa kuhakikisha kuwa kanuni msingi zilizopitishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican zinafuatwa na kutekelezwa kikamilifu.
Vitabu hivi havina budi kuwa ni kwa ajili ya ustawi na mafao ya waamini, kwa kutambua dhamana na mchango wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Mahalia, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kikanda pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican kuhakikisha kwamba, tafsiri ya Vitabu vya Liturujia ya Kanisa vinafuata kikamilifu tafsiri asilia ya Vitabu vya Liturujia ya Kanisa mintarafu madhehebu ya Kilatini. Ili kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na ushirikiano kati ya Vatican na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia mintarafu huduma hii tete inayopaswa kutolewa kwa waamini, kwa kusikiliza kwa makini mapendekezo ya Tume za Liturujia za Maaskofu kwa mamlaka aliyokabidhiwa na Mama Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko anatamka kwamba, Sheria za Kanisa namba 838 zinapaswa kuwa wazi zaidi.
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu lugha ya Liturujia wanatoa mamlaka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Mahalia pamoja na kuzingatia maoni ya Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu Kikanda sanjari na kupata kibali kutoka Vatican. Tafsiri ya vitabu vya Liturujia ya Kanisa kwa lugha ya Kilatini lazima ikubaliwe na Baraza la Maaskofu Katoliki husika pamoja na kuzingatia kanuni zinazotajwa katika mchakato wa kufanya marekebisho ya Liturujia ya Kanisa mintarafu lugha katika ibada.
Baba Mtakatifu Francisko anatamka kwamba, kuanzia sasa Sheria ya Kanisa namba 838 itasomeka kuwa Vatican ina dhamana kuu ya kuratibu maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kadiri ya Sheria za Kanisa pamoja na Askofu Mahalia. Sheria hii inafafanuliwa kwamba, Vatican ina dhamana ya kuratibu Liturujia Takatifu; kupitia marekebisho ya Vitabu vya Liturujia vilivyopitishwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria kwa uaminifu mkubwa. Ni wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kuandaa vitabu vya Liturujia kadiri ya mipaka na uwezo wake baada ya kupitishwa na kuidhinishwa na Vatican. Maaskofu Mahalia kadiri ya mamlaka yake anayo dhamana pia ya kutunga sheria za Liturijia Jimboni mwake. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, marekebisho ya sheria hii mpya yataanza kutumika rasmi tarehe 1 Oktoba 2017.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top