0
Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri limechapisha mwongozo wa malezi ya Kipadre  unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”. Utangulizi wa mwongozo huu unabainisha changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli Wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia!



Mwongozo huu ni matunda ya ushirikiano mkubwa kutoka katika Sektretarieti kuu ya Vatican, kazi iliyoanza kutimua vumbi kunako mwaka 2014. Mwongozo unatoa kwa muhtasari wa sheria, kanuni na mambo msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwa ajili ya malezi na makuzi ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Unabainisha wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki; Waratibu wa Seminari kitaifa na kimataifa pamoja na mwongozo wa malezi ya Seminari moja moja.
Sura ya Pili ya Mwongozo huu inapembua kwa kina na mapana kanuni msingi za maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre: Yaani wanapaswa kuunganika na Kristo ili kuwaongoza, kuwachunga na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wanapaswa kuungana na Kristo Yesu katika maisha, upendo na ukweli kwa ajili ya wokovu wa watu na kuendelea kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia. Dhamana ya Kanisa ni kulea, kusindikiza na kupalilia miito mitakatifu, lakini kwa namna ya pekee wito wa Daraja Takatifu.
Seminari ndogo na nyumba za malezi ni mahali pa kulea na kuwasindikiza vijana katika maisha na wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Hapa waseminari wadogo wanapaswa kupewa malezi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kukazia majiundo ya kiakili, kiroho, kiutu na kimaadili. Ni mahali pa kukuza ukomavu, umoja na mshikamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno la Mungu na Mashauri ya Kiinjili. Walezi wawe kweli ni mashuhuda wa Injili ya Kristo! Mwongozo pia unaangalia wito kwa Daraja takatifu wa watu wenye umri mkubwa, wasaidiwe na kupatiwa malezi makini katika nyumba maalum, ili waweze hatimaye, kufanya maamuzi muhimu katika maisha yao! Kanisa linaangalia pia wito wa Kipadre unaoweza kuibuka miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji na jinsi ya kuwasaidia vijana wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!
Sura ya Tatu inagusia misingi ya malezi ya Kipadre. Hapa wahusika wakuu ni majandokasisi na kiini cha malezi haya ni utambulisho wa Padre mintarafu mafundisho ya kitaalimungu kwa kutambua kwamba, Padre ni Sadaka hai na takatifu inayompendeza Mungu na Sakramenti hii inapata chimbuko lake katika Ubatizo, lakini wanapaswa mafuta matakatifu ili kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na Kusamehe dhambi za waamini wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu. Padre anajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili pamoja na Kanisa. Kumbe, safari ya majiundo ya Kikasisi imwezeshe Jandokasisi kufanana na Kristo Yesu kwa kuwa mtakatifu pasi na mawaa; mtu mwenye huruma na mapendo kwa ajili ya wokovu wa watu. Malezi ya maisha ya kiroho ni muhimu sana ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa. Majandokasisi wanapaswa katika safari ya maisha yao kuwa na Baba wa maisha ya kiroho atakayemsaidia hatua kwa hatua. Malezi yanapaswa kuwa na umoja, imara na thabiti, changamoto inayohitaji walezi walioandaliwa vyema!
Sura ya Nne: Malezi ya awali na endelevu. Malezi ya awali ni yale yanayotolewa kwa majandokasisi Seminarini kabla ya kupewa Daraja Takatifu ya Upadre. Malezi endelevu ni nyenzo msingi zinazomwezesha Padre kupyaisha maisha na utume wake, kwa kuwa na wongofu endelevu, kwa kusoma alama za nyakati katika mwanga wa imani, upendo wa kichungaji na sadaka binafsi. Malezi haya ni wakati wa masomo ya falsafa ili kujenga dhana ya Ufuasi wa Kristo na masomo ya taalimungu ni kumwezesha jandokasisi kujifananisha zaidi na Kristo mtumishi na mchungaji mwema na hatima ya safari hii ya malezi ni Daraja ya Ushemaji na hatimaye Daraja takatifu ya Upadre.
Majiundo endelevu kimsingi yanajikita katika upendo wa shughuli za kichungaji unaofumbatwa katika maisha na utakatifu wa Wakleri. Ni wajibu wa Maaskofu kuwa makini kwa maisha na wito wa Mapadre wao vijana, ili wasijikute wanaingia katika mazingira magumu na hatarishi katika maisha na wito wao wa Kipadre. Watambue mapungufu yao ya kibinadamu na kwamba, wao ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa na wala si wafanyakazi wa mshahara. Wawe makini katika kupambana na changamoto za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kukuza umoja na udugu katika maisha ya Kipadre sanjari na Mashauri ya Kiinjili.
Mapadre waendelee kupyaisha maisha na wito wao wa Kipadre kwa tafakari ya Neno la Mungu, “Lectio Divina”; Kwa kuwa na Padre wa maisha ya kiroho; kwa kushiriki mafungo, maisha ya kijumuiya pamoja na kushirikiana na Mapadre wengine kwa njia ya vyama vinavyowaunganisha Mapadre kwa malengo mbali mbali.
Sura ya tano inapembua mielekeo ya malezi kwa kujikita katika malezi ya maisha ya kiutu: hapa malezi ya mtu mzima ili kweli aweze kujiandaa kuwa ni Mtumishi wa Mungu na watu wake; kwa kuboresha mahusiano na watu wanaomzunguka, tayari kushikiri kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Jumuiya ya watu wanaomzunguka. Awe na mahusiano mema na wanawake, kwa kuthamini na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, kwani anapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa Uinjilishaji. Matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, kwa kutambua faida nahasara zake.
Malezi kiroho: yanajikita katika tafakari ya Neno la Mungu; Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho; Maisha ya Sala na Ibada pamoja na kuwa na mahusiano ya karibu na Padre mlezi wa maisha ya kiroho pamoja na kukuza kwa kina na mapana Mashauri ya kiroho. Malezi: kiakili ni kumwezesha jandokasisi kuwa mahiri katika falsafa na taalimungu ili kupambana changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika masuala ya kitamaduni kwa kutoa malezi ya kina kwa milango yote ya fahamu za binadamu! Majiundo haya yazingatie pia utamaduni na historia ya nchi husika.
Malezi ya kichungaji, mambo yanayomwezesha Padre kuwajibika na kutoa huduma makini zaidi kwa familia ya Mungu kwa njia ya upendo wa shughuli za kichungaji. Kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kuamua na kutenda; kwa kuwaheshimu na kuwajali watu; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kusimamia tunu msingi za maisha ya Kikristo, daima akionesha ari na utume wa Kimissionari.
Sura ya sita inabainisha mihimili mikuu ya malezi kwa kuzingatia kwamba, mlezi mkuu ni Fumbo la Utatu Mtakatifu, Askofu mahalia, Mapadre, Waseminari wenyewe, Jumuiya ya walezi yaani Majaalimu na wataalam mbali mbali wanaoalikwa ili kusaidia kutoa malezi kwa majandokasisi. Familia na Parokia pia zinahusika kikamilifu katika malezi ya majandokasisi. Watawa na waamini walei wanaweza pia kuhusishwa katika malezi ya Mapadre wa baadaye. Makundi yote haya ni muhimu sana katika malezi endelevu ya Wakleri katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa.
Sura ya Saba: inazungumzia kuhusu uratibu wa masomo ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika mchakato wa Uinjilishaji mpya! Kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na uratibu wa masomo unaounganisha na kukamilisha majiundo ya Mapadre ili kuwa kweli ni watumishi wa Kristo na Kanisa lake, tayari kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kadiri ya mazingira na mahitaji ya watu wa nyakati. Changamoto mamboleo zinahitaji majiundo makini na ya dhati kwa Mapadre tangu wakati wa kuwapokea kabla ya kuanza masomo ya falsafa na taalimgu. Wawe na majiundo yenye uwiano mzuri kati ya maisha ya kiutu na maisha ya kiroho; kitamaduni pamoja na kuwa na ufahamu mpana zaidi wa imani ya Kanisa Katoliki.
Hapa kuna haja ya kuwa na ufahamu mkubwa zaidi wa Maandiko Matakatifu, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mapadre wafundwe mambo msingi ya maisha ya kiroho na ibada. Pale inapoonekana inafaa, baadhi ya Mapadre wapelekwe kwenye masomo maalumu ili kulisaidia Kanisa kuweza kuwa na wataalam katika medani mbali mbali za maisha na utume wake.
Sura ya Nane inatoa kanuni na sheria za kuzingatiwa katika malezi ya majandokasisi kwa kutambua kwamba, kimsingi Seminari ni Jumuiya ya malezi, kumbe, kuna uwezekano wa Majimbo kushirikiana katika malezi ya waseminari na hapa kuna haja ya kuwa na uangalifu mkubwa. Baraza la Kipapa la Wakleri linatoa vigezo vya vijana wanaoweza kuchaguliwa kujiunga na Seminari au kuondolewa seminarini kwa kuzingatia na kutegemea sayansi ya tiba, masuala ya kisaikolojia kwa ajili ya utume wa Mapadre wa baadaye. Wawe ni watu wenye afya njema: kimwili, kisaikolojia. Vijana wanaoonesha tabia na mienendo ya ushoga na ndoa za jinsia moja, hawatakubalika Seminari. Watoto wadogo wanapaswa kulindwa na kutunzwa, wale wote watakaojihusisha na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto washughulikiwe kadiri ya sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwa sasa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.


Chapisha Maoni

 
Top