Tafakari zinazotolewa na Padre Raniero Cantalamessa wakati huu wa Kipindi cha Majilio kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa mwaka 2016 zinaongozwa na kauli mbiu “Roho Mtakatifu ni chemchemi ya matumaini”. Hizi ni ni tafakari zinazohudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko, viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume.
Tafakari ya tatu katika mfululizo huu iliyotolewa Ijumaa, tarehe 16 Desemba 2016 imejikita katika “kulewa busara ya Roho Mtakatifu” maneno yanayopata chimbuko lake kutoka katika hotuba iliyotolewa na Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1975 kwa wanachama wa Chama cha Upyaisho Cha Wakarismatiki Wakatoliki, akiwataka kwa furaha kuu kuchota busara ya Roho Mtakatifu kama dira na mwongozo wa maisha na utume wao!
Padre Cantalamessa ametumia fursa hii pia kumtakia heri, baraka na matashi mema Baba Mtakatifu Francisko anapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 80 tangu kuzaliwa kwake, Jumamosi, tarehe 17 Desemba 2016. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, Kristo Yesu anakuwa ni chakula chao cha kiroho; chemchemi ya maji ya uzima wa milele na kwa njia yake wanaweza kulewa busara ya Roho Mtakatifu kama kielelezo cha maisha na ushuhuda wa uwepo wa Roho Mtakatifu anayewawezesha kutoka katika ubinafsi wao kwa mawazo na kuishi kadiri ya mwongozo wa Roho Mtakatifu, tayari kufisha dhambi na kuwa na maisha mapya ya kiroho.
Padre Cantalamessa akifanya rejea ya safari ya Waisraeli Jangwani, waliponyweshwa maji kutoka mwambani anakaza kusema wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata na mwamba ule ulikuwa ni Kristo na hapo akawajaza furaha, uzima mpya na busara inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu na hivyo kuenea katika akili na kuupatia moyo nguvu ya kutenda mema.
Huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba, Roho Mtakatifu anapewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa, kwani zawadi ya Roho Mtakatifu kutoka kwa Kristo ni amana ya ukombozi wake unaotolewa kwa ajili ya watu wa nyakati zote. Zamani ilifikiriwa kwamba, ili kuweza kufyonza busara ya Roho Mtakatifu, waamini walipaswa kufunga na kujitesa; kwa kusali Sala ya Yesu; kwa kuwa makini na kukesha; kwa kusafisha dhamiri ili kuondokana na mawazo machafu pamoja na kukataa kumezwa na malimwengu. Huu ni mwaliko wa kujiweka wazi mbele na kwa ajili ya Mungu kwa kuondokana na tabia ya mazoea ilikujenga umoja na Mungu na hatimaye, kupata neema na baraka yake; mambo yanayowaunganisha waamini kwa Muumba wao!
Mchakato huu wa maisha ya kiroho ni kwa ajili ya wakamilifu, kumbe, waamini wengine wanapaswa kuendelea na mapambano dhidi ya vilema na mapungufu ya maisha yao ili kuweza kung’amua uwepo wa Mungu na Roho Mtakatifu katika hija ya maisha yao, kielelezo makini cha jitihada ya mwamini ili kushuhudia imani tendaji. Roho Mtakatifu ndiye anayewawezesha waamini kuweza kulewa busara ya Roho Mtakatifu. Lengo ni kuufisha udhaifu wa binadamu kwa kumwezesha Roho Mtakatifu kuleta mageuzi katika maisha yao ya kiroho.
Yesu Kristo kwa muda wa miaka mitatu aliwaongoza na kuwafundisha mitume wake Mafumbo makuu ya maisha na utume wake, lakini Siku ile ya Pentekoste, waliposhukiwa na Roho Mtakatifu, wakawa na ujasiri wa kumwilisha katika maneno na matendo mafundisho makuu ya Yesu, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kama ushuhuda wa Kristo na Kanisa lake. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kukua na kukomaa katika maisha ya utakatifu, utume, huduma, utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Pasi na uwepo wa neema na karama za Roho Mtakatifu, juhudi zote hizi ni bure!
Katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, waamini wana haja zaidi ya kuwa na busara ya Roho Mtakatifu, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa kizazi hiki, wanaoogelea katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni kwa njia ya silaha za maisha ya kiroho tu, waamini wanaweza kushinda vita hii kwa maana silaha za vita vyao si vya kimwili, bali zina uwezo katika Mungu kiasi hata cha kuweza kuangusha ngome, kumbe wanapaswa kuangusha mawazo na kiburi na mambo yote yale yanayojiinua juu ya elimu ya Mungu sanjari na kuteka kila fikra ipate kumtii Kristo Yesu.
Padre Cantalamessa akizungumzia kuhusu Ubatizo wa Roho Mtakatifu anasema, mahali pa kuchota hekima ya Roho Mtakatifu ni katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Maandiko Matakatifu pamoja na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa kwenye Kanisa la mwanzo na kwamba uzoefu wa Siku kuu ya Pentekoste ni endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Roho Mtakatifu anatenda kazi katika Sakramenti za Kanisa na hata nje ya Kanisa lenyewe kama inavyojidhihirisha kwa njia ya Chama cha Upyaisho cha Wakarisimatiki Wakatoliki. Roho Mtakatifu ndiye anayeleta mabadiliko katika maisha ya waamini, kielelezo cha Ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Upyaisho wa maisha ya Kikristo unatekelezwa kwa njia ya Ubatizo na Kipaimara! Roho Mtakatifu anaendelea kutenda kazi kwa waamini wanaofunga Ndoa Takatifu na Wakleri wanapopokea Daraja Takatifu na watawa kuweka nadhiri zao. Katekesi makini inawawezesha waamini kukutana na kweli za imani: Upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; dhambi na wokovu; maisha mapya katika Kristo Yesu; Karama na Matunda ya Roho Mtakatifu bila kusahau mahusiano binafsi na Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!
Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni mwanzo wa mchakato wa ukomavu katika imani, dhamana na maisha ya Kikristo ndani ya Kanisa. Ubatizo wa Roho Mtakatifu umekuwa ni chachu ya mageuzi ya Wakristo katika Makanisa mbali mbali kwani matunda ya Roho Mtakatifu ni upendo, furaha na amani. Pentekoste ni tukio endelevu katika maisha na utume wa Kanisa kama wanavyokaza kusema, Mtakatifu Yohane XXIII na Mwenyeheri Paulo VI. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa linahitaji tukio hili katika maisha na utume wake ili kuendelea kutangaza na kushuhudia: upendo, ukweli na tunu msingi za maisha ya Kikristo; matunda ya Roho Mtakatifu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni