Wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili, (Mk 1:15), haya ndiyo maneno ya kwanza ya Yesu ambayo kadri ya Mwinjili Marko yanafungua kazi ya hadhara ya Yesu, kwa maana hiyo kazi ya Yesu inaanza kwa kuwaandaa watu katika toba ili hatimaye, wapate kuukaribia au kuingia katika ufalme wa Mungu. Na wakati ndiyo sasa. Wakati ni sasa , Yesu anatuhubiria na Kwaresima imewadia, na ndiyo maana siku ya Jumatano ya majivu, kwa kuitikia mwito wa maneno ya Yesu
kanisa linatualika kuingia katika kipindi cha Kwaresma, ambacho ni kipindi cha kujikusanya, kujitayarisha, kijitengeneza na kujikarabati hasa kwa toba, kufunga, kusali na kujitoa sadaka zaidi mambo yanayorutubishwa kwa tafakari ya kina ya Neno la Mungu.
kanisa linatualika kuingia katika kipindi cha Kwaresma, ambacho ni kipindi cha kujikusanya, kujitayarisha, kijitengeneza na kujikarabati hasa kwa toba, kufunga, kusali na kujitoa sadaka zaidi mambo yanayorutubishwa kwa tafakari ya kina ya Neno la Mungu.
Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini ambacho ni mwaliko wa kusafiri kiroho na Kristo Mwokozi wetu, kama walivyofanya Waisraeli jangwani kwa muda wa miaka arobaini. Katika safari ya Kwaresima, Kanisa linatuongoza kwa tafakari na mazoezi yatakayotusaidia kukua zaidi kiroho na zaidi kukutana na Kristo mfufuka aliye Jiwe kuu la msingi la Ufalme wa Mungu. Katika Agano la Kale, ilichukuwa taifa la Israel miaka arobaini kuingia katika Nchi ya ahadi, hiki kilikuwa ni kipindi kirefu ambacho pamoja na kutawaliwa na matendo makuu ya Mungu, kilitawaliwa pia na vishawishi kiasi hata cha kuwafanya Waisraeli wajisikie mara kadhaa kuiacha safari iliyokuwa inawaelekeza mbele kwenye nchi ya ahadi.
Pia kilikuwa ni kipindi cha kuterereka na kukataa tamaa hasa pale Waisraeli walipopata shida (kut 14:10-12), mbali na hayo kilikuwa pia ni kipindi kilicho jaa huruma ya Mungu. Katika Agano Jipya, ilimchukuwa Yesu siku arobaini za kufunga ambamo ndani yake Yesu anashiriki hali yetu dhaifu akitufundisha na kutuonyesha njia ya kuvishinda vishawishi, dhambi na nafasi zake. Safari hii ya Yesu ya siku arobaini ilikuwa ni kielelezo cha kipindi cha maisha yetu, maisha yaliyojaa raha na karaha, yakidai kupokea hayo yote kwa jicho na uradhi wa moyo unaongozwa na Imani katika matendo! Hivyo basi, ni matumaini kuwa pamoja na vikwazo na changamoto nyingi tunazozipitia katika safari ya imani, kipindi cha Kwaresma kinatupatia fursa ya mazoezi ya kiroho na tafakari zitakazo saidia kukutana na Kristu mfufuka.
Ikumbukwe kuwa, kuna mambo manne, ambayo yaweza kufanya imani yetu kubakia imara hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima na wakati wote wa maisha yetu. Nayo ni sala, kufunga, matendo ya huruma na tafakari ya kina ya Neno la Mungu; mambo yote haya huenda sanjari! Kufunga ni roho ya sala, matendo ya huruma ni damu ya kufunga, hivyo sasa kama ukisali, funga na kama ukifunga, onyesha huruma na kama ukitaka maombi yako yasikilizwe sikiliza maombi ya wengine, na ndiyo kusema asiyefunga masikio yake kwa wengine, anajifungulia masikio ya Mungu kwake mwenyewe. Ukifunga angalia mfungo wa wengine pia, na ukitaka Mungu ajue kuwa una njaa basi nawe tambua kama mwingine au mwenzako ana njaa, na ukitaka huruma onyesha huruma. Hivyo, Kipindi hiki kitupe fursa ya kumjua Mungu zaidi, na hivyo tumwendee Mungu kwa sala, toba, tafakari ya kina ya Neno la Mungu, matendo ya huruma, kufunga, kuwajali wenzetu na hasa wale wanaoteseka na wanahitaji.
Kutoka Radio Vatican, ni mimi Padre, Agapiti Amani, ALCP/OSS
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni