KATIBU Mkuu wa Jimbo Katoliki Morogoro Padri Luitfrid Makseyo amewaasa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuondokana na hofu na mashaka ya maisha katika nafsi zao ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao hatimaye waje kulitumikia vyema taifa.
Padri Makseyo amesema hayo katika mahafali ya kuwaaga wana jumuiya ya Wanafunzi Wakatoliki Tanzania [TMCS] iliyofanyika katika Kampasi ya Mazimbu jimboni humo, ikiambatana na utoaji wa sakramenti ya kipaimara kwa vijana 29 chuoni hapo.
Amesema moja ya sababu zinazowafanya wanafunzi wengi nchini kutokufaulu vizuri masomo ni hofu, mashaka na woga miongoni mwao hali inayosababisha kushindwa kujiandaa vyema katika mitihani yao huku akisema kuwa katika maisha ya kawaida hakuna mwanadamu ambaye hajawahi kujenga hofu moyoni mwake japo kwa wanafunzi ndio zaidi hasa wanapokabiliwa na mitihani.
Hata hivyo Katibu huyo amesema kuwa kutokana na hofu hiyo inayotawala miongoni mwa wanafunzi katika masomo yao, inafika wakati wengine kujihusisha na imani za kishirikina kwa waganga wa kienyeji pamoja na matumizi ya hirizi jambo ambalo huongeza hofu nyingine kwa jamii inayowazunguka.
“Ukidhani kwamba Yesu hafai kwa lolote na kwenda kwa waganga wa kienyeji nenda kajaribu uone matokeo yake, watakwambia uchukue hirizi wakati wa kusoma ikuongoze kuelewa, kwanza kuibeba tu unajenga mashaka mengine kwa kujiuliza pengine wenzangu wanaweza wakaiona ikidondoka, ukifikia hatua hiyo ujitambue wazi akili zako hazipo sawasawa badala ya kuondoa mashaka unaongeza mashaka mengine,” Amesisitiza
Sambamba na hayo Padri Makseyo amesema kuwa njia pekee ya kuepukana na hofu ni kumwamini Mwenyezi Mungu pekee, kwa kuwa hakuna jambo gumu linaloshindakana kwake badala ya kushiriki katika imani za kishirikina.
Wakati huo huo Padri Makseyo ametoa rai kwa wahitimu hao kuwa na utayari wa kulitumikia taifa, wakiamini kwamba watanzania wanahitaji mchango wao katika upatikanaji wa huduma zinazoendana na taaluma zao.
Mbali na hayo amewataka wahitimu hao kujenga uvumilivu katika changamoto watakazokabiliana nazo katika uwajibikaji wao katika taifa huku wakikubali kukosolewa na kushauriwa na wataalamu wengine badala ya kutumia taaluma zao pekee.
“Nyie mmetekeleza jukumu lenu kwa ajili ya kulitumikia taifa, huko mnapoenda mtakutana na makundi ya kila aina, wajinga wanawahitaji,wasomi wanawahitaji, na jamii inawahitaji pia, jambo pekee la kujua ni kuzitendea haki taaluma zenu bila kujiingiza katika vitendo vya rushwa, ufisadi, na dawa za kulevya, mkiepukana na hayo mtaleta manufaa kwa taifa.”
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni