0
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 24 – 26 Juni, 2016 anafanya hija ya 14 ya kitume kimataifa kwa kutembelea nchini Armenia, kama awamu ya kwanza, awamu ya pili Baba Mtakatifu atatembelea nchini Georgia na Azerbagian, hapo mwezi Septemba 2016. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Armenia inaongozwa na kauli mbiu “Hija kwa nchi ya kwanza ya Kikristo”. Hija hii inajikita zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja sanjari na kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani, hasa huko Mashariki ya Kati.

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, Armenia ilikuwa ni nchi ya kwanza kabisa kupokea dini ya Kikristo kama dini rasmi, baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Mtakatifu Gregori anayeheshimiwa na kupendwa na waamini wengi duniani! Baba Mtakatifu anakwenda nchini Armenia ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, ili waweze kutembea katika njia ya haki, amani na upatanisho baada ya mateso na mahangaiko makubwa yaliyopelekea sehemu kubwa ya wananchi wa Armenia kuikimbia nchi yao na kwa sasa wanaishi ugenini, lakini bado wanaendelea kuwa waaminifu kwa mapokeo ya imani, tamaduni, mila na desturi zao njema.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Armenia atapata nafasi ya kusali Liturujia Takatifu, ili kuombea amani, ustawi na maendeleo ya wengi na waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema pamoja na kuzungumza na viongozi wa kidini, kiserikali na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao huko Armenia. Atapata nafasi ya kutembelea maeneo nyeti ya kumbu kumbu ya historia ya Waarmenia. Baba Mtakatifu kabla ya kurejea tena Vatican, ataungana na Patriaki Karekin wa II kwenye Monasteri ya Ararat na hapo watarusha njiwa alama ya kuombea amani nchini Armenia.
Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika hija hii ya kitume anaambatana na Kardinali Leonardi Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki na anatarajiwa kuondoka majira ya asubuhi kutoka Roma. Safari hii itamchukua mwendo wa masaa matano na anatarajiwa kuwasili uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa  Yerevan majira ya saa 9: 00 Alasiri. Hapo Baba Mtakatifu atazungumza na viongozi wa Serikali na wanadiplomasia.
Jumamosi tarehe 25 Juni 2016 Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na Patriaki Karekini II atatoa heshima zake za dhati kwa wahanga wa mauaji ya kimbari ya Metz Yeghèm, katika uwanja wa kumbu kumbu wa Tzitzernakaberdi na jioni watashiriki katika mkutano wa kiekumene na kwa ajili ya kuombea amani. Hili ni tukio ambalo linatarajiwa kuwa na mvuto kwa watu wengi zaidi. Eneo la ukarimu, umoja na udugu litakuwa ni Etchmiadzin, nje kidogo ya mji mkuu wa Yerevan, mahali ambapo ni Makao makuu ya Kanisa la Kitume la Armenia. Wakati wote wa hija ya kitume huko Armenia, Baba Mtakatifu atakirimiwa na Patriaki Karekin II.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 25 Juni 2016 atatembelea mji wa Gyumri na huko ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Vartanants. Kwa mara ya kwanza Ibada hii itaadhimishwa nje ya Kanisa, kwani kwa Waarmenia Ibada zote hufanyika ndani ya Kanisa. Atatembelea Kanisa kuu na kwenda kusalimia watoto yatima wanaotunzwa na Watawa wa Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya Asili.
Monsinyo Antranig Ayvazian anayefundisha Chuo kikuu cha Yerevan ambaye ameshiriki katika mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Armenia anasema, familia ya Mungu nchini humo inasubiri kwa hamu baraka za kitume kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, chemchemi ya furaha na matumaini mapya kwa Waarmeni kwa siku za usoni.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top