0
Baba Yetu Uliye mbinguni ni sala inayomwonesha mwamini uso wa huruma ya Mungu ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake na mwongozo thabiti wa maisha ya Mkristo. Sala ni muhimu sana katika maisha ya Mkristo kama anavyofundisha na kushuhudia Yesu mwenyewe katika maisha yake. Katika mafundisho yake makuu, Yesu anawafundisha wanafunzi wake namna ya kusali vyema, huku wakimwelekea Mwenyezi Mungu, Baba mwenye huruma.
Mwenyezi Mungu anatambua mahitaji ya waja wake hata kabla ya kumwomba, kwani Mungu ni Baba mwenye huruma, anayesikiliza kwa makini kutoka katika undani wa mtu, changamoto na mwaliko kwa waamini kusali kutoka katika undani mwao kama anavyofundisha Kristo Yesu, kwani kwa njia hii waamini wanapata utambulisho wao kama watoto wa Mungu, neema kutoka kwa Roho Mtakatifu.
Baba Yetu ni maneno na sala ambayo Yesu alikua akiitumia wakati alipokuwa anakabiliana na magumu pamoja na changamoto katika maisha na utume wake; wakati alipokuwa na furaha au huzuni. Yote haya yanaonesha kwamba, Kristo alikuwa ni kiongozi na mwalimu wa sala. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 16 Juni 2016.
Papa anasema, Baba Yetu ni utambulisho na mzizi wa sala ya Kikristo! Ni kweli kabisa waamini wanaweza kuelekeza sala zao kwa Bikira Maria, Watakatifu na Malaika, lakini Sala ya Baba yetu ni nguzo ya maisha na utambulisho wa Kikristo. Kila sala inapaswa kupata msingi wake hapa na baadaye waamini wanaweza kuendelea na hija, ibada na sala nyinginezo zinazotolewa na Mama Kanisa. Katika sala ya Baba Yetu, waamini wanamwomba Mungu toba na msamaha wa dhambi zao; inaonesha utambulisho wao wa umoja, udugu na familia ya Baba wa mbinguni, tayari kusamehe na kupokea msamaha kutoka kwa wengine ili kuondokana na kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuchunguza dhamiri zao jinsi wanavyosali na kuimwilisha Sala ya Baba Yetu katika uhalisia wa maisha yao, kiasi cha kujisikia kuwa Mwenyezi Mungu ni Baba yao mwingi wa huruma na mapendo. Wasisite kumwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kukimbilia huruma ya Baba wa mbinguni, tayari kusamahe na kusahau, ili kukuza na kudumisha utambulisho wa watoto na familia ya Mungu, tayari kusonga mbele kama mashuhuda na vyombo vya msamaha na huruma ya Mungu duniani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top