Kuwashauri wenye shaka; kuwafundisha wajinga; kuonya wakosefu; kufariji wenye huzuni; kusamehe makosa; kuvumilia wasumbufu; kuwaombea walio hai na marehemu ni sehemu muhimu sana ya matendo ya huruma kiroho. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano, tarehe 16 Novemba 2016 amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kuwavumilia wasumbufu ambao wanaweza kutambulikana mara moja katika maisha ya watu.
Hawa wanaweza kuwa ni majirani, ndugu na hata jamaa, lakini waamini wanapaswa kutambua kwamba, hata wao wakati mwingine wamekuwa ni wasumbufu kwa ndugu na jirani zao, ndiyo maana wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu wote wanakumbushwa kuwavumilia wasumbufu! Maandiko Matakatifu yanaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu amekuwa mvumilivu, mpole kwa wana wa Israeli waliokuwa wamesheheni litania ya malalamiko mbele ya Mussa, akamfundisha kuwa na uvumilivu mbele yao, kielelezo makini cha imani.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia ikiwa kama hata wao wamekuwa ni wasumbufu kwa wengine, ili waweze kujifunza kuwa na subira! Yesu kwa muda wa miaka mitatu, alionesha uvumilivu sana kwa wote waliokuwa wanamsumbua. Mama yake akina Yakobo na Yohane aliyetaka watoto wake wapewe upendeleo wa pekee katika Ufalme wa Mungu, lakini Yesu anawafundisha wote kwamba, madaraka ni huduma na sadaka kwa ajili ya Mungu na jirani.
Baba Mtakatifu anasema, kuonya wakosefu na kuwafundisha wajinga ni sehemu ya matendo ya huruma kiroho, dhamana nyeti inayowawezesha wengine kuweza kukua na kukomaa katika imani na maisha. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Makatekista, wazazi na walezi wanaojisadaka usiku na mchana ili kuwafundisha watoto mambo msingi ya imani. Inachosha hata kwa watoto ambao pengine wangefurahia kucheza kuliko hata kusikiliza katekesi.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwasindikiza jirani zao katika mchakato wa kutafuta kilicho chema na kizuri katika maisha yao kwa kuzama zaidi katika undani wa hazina ya nyoyo zao. Kufundisha na kuangalia mambo msingi ni msaada mkubwa katika ulimwengu mamboleo unaotaka kuridhisha tamaa ya mambo mpito. Waamini wawe na ujasiri wa kuwafundisha na kuwaongoza watu katika mambo msingi ambayo Mwenyezi Mungu anataka kutoka kwao; kwa kuzingatia wito ili kufuata njia ya furaha ya kweli kwa kuondokana na wivu, chuki, uchu wa mali na madaraka, vishawishi ambavyo daima vitaendelea kumwandama mwamini katika safari ya maisha yake hapa duniani.
Dhamana ya kufundisha, kuonya na kuelekeza, isiwafanye watu kujisikia kuwa na kiburi na hivyo kuwadharau wengine, bali ni changamoto ya kuzama katika undani wao ili kuangalia ikiwa kama kweli wanaishi kile ambacho wanataka kuwashauri wengine. Daima maneno ya Yesu anayewataka wafuasi wake kutokuwa wanafiki, kwa kuangalia kibanzi kilichoko kwenye jicho la jirani yao na kushindwa kuona boriti lao wenyewe iwe ni changamoto ya kuvumiliana katika unyenyekevu na upole wakati wa kushauriana!
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake ametumia fursa hii kuwakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Jumapili ijayo, tarehe 20 Novemba 2016, Ni Siku ya Haki ya Mtoto Kimataifa. Baba Mtakatifu anawataka wadau kuanzia kwenye familia na taasisi mbali mbali kuhakisha kwamba, wanasimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza watoto, ili wasitumbukie katika utumwa mamboleo, kupelekwa mstari wa mbele kama askari au kunyanyaswa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kujizatiti katika kulinda maisha yao, uhakika wa kwenda shule na kupata elimu bora, ili hatimaye, waweze kukua kwa utulivu na kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni