Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu asubuhi, tarehe 20 Juni 2016 ameongoza mkutano wa kawaida wa Makardinali wakati wa sala ya hadhuhuri, ili kupiga kura kwa ajili ya wenyeheri wanaotarajiwa kutangazwa na Mama Kanisa kuwa ni watakatifu. Baba Mtakatifu ameridhia kwamba, wenyeheri hawa wafuatao hapa chini watangazwe kuwa watakatifu katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa hapo tarehe 16 Oktoba 2016.
Wenyeheri hawa ni: Salome Leclercq, Shahidi, Mtawa wa Shirika la Shule za Kikristo; Manuel Gonzàles Garcìa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Palencia na Muasisi wa Umoja wa Upatanisho wa Kiekaristi na Shirika la Wamissionari wa Ekaristi wa Nazareth. Padre Lodovico Pavon, Muasisi wa Shirika la Mabinti wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Padre Alfonso Maria Fusco, mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Mtakatifu Yohane Mbatizaji na mwishoni ni Elizabeth wa Utatu Mtakatifu, Mtawa wa Shirika la Wakarmeli.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amewapandisha hadhi Makardinali wafuatao katika madaraka ya huduma kama Mashemasi na Mapadre. Kardinali William Joseph Levada amepandishwa hadhi na kuwa ni Padre wa huduma katika Kanisa kuu la S. Maria in Domenica. Kardinali Franc Rodè amepandishwa hadhi na kuwa ni Padre wa huduma katika Kanisa kuu S. Francesco Saverio huko Garbatella.
Wengine ni Kardinali Andrea Cordero Montezemolo aliyepandishwa hadhi na kuwa ni Padre wa huduma kwenye Kanisa kuu S. Maria huko Portico na mwishoni ni Kardinali Albert Vanhoye aliyepandishwa pia hadhi ya kuwa ni Padre wa huduma kwenye Kanisa la S. Maria wa Mercede na S. Adriano huko Villa Albani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni