0
Familia Barani Afrika: Jana, Leo na Kesho kadiri ya mwanga wa Injili ndiyo kauli inayoongoza maadhimisho ya mkutano wa 17 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM uliofunguliwa rasmi kuanzia tarehe 18 Julai 2016 na unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 25 Julai 2016 huko Luanda, nchini Angola. Ni mkutano unaohudhuriwa na wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu kutoka Afrika na Magascar.
Katika mahojiano maalum na Radio Vatican kutoka Luanda, Angola Askofu Tarcisisu Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema SECAM inafanya maadhimisho haya baada ya miaka mitatu na kwamba, mara ya mwisho mkutano mkuu wa 16 wa SECAM uliadhimishwa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC. Mwaka huu, familia ya Mungu Barani Afrika inajadili na kutafakari kuhusu changamoto zinazoendelea kutishia maisha na utume wa ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo Barani Afrika.
Mababa wa SECAM anasema Askofu Ngalalekumtwa wanataka kuibuka na mikakati ya shughuli za kichungaji itakayoimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya Kiafrika na Kikristo kweli kweli. Anasema, kuna haja ya kukazia umuhimu wa maandalizi kwa wanandoa watarajiwa, katekesi makini na endelevu; Sakramenti za Kanisa; Sheria za Kanisa na Kiraia; tunu msingi za maisha na ndoa na familia. Lengo ni kujenga familia imara na thabiti kadiri ya mfano na matakwa ya Kristo Yesu kwa Kanisa lake alilolionesha udumifu na uvumilivu hadi mwisho.
Ni matarajio yake kwamba, Mababa wa SECAM wataweza kuimarisha ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia Barani Afrika, kwa kuzijengea uwezo familia ili kuweza kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia katika uhalisia wa maisha ya Kiafrika bila kumezwa na utandawazi wala malimwengu. Ukuu na utakatifu wa ndoa unafumbatwa katika Sakramenti ya Ndoa ambayo ni ngazi ya kupandia kwenda mbinguni kwa wanandoa wenyewe kama ilivyotokea kwa wazazi wake Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu waliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Familia, Oktoba 2015.
Askofu Ngalalekumtwa anakaza kusema, utakatifu na ukuu wa maisha ya ndoa na familia unahitaji majitoleo makubwa yanayofumbatwa katika sala, maandalizi mahususi ya kiroho na kimwili; kisaikolojia, kiuchumi, ki hali na kijamii. Lengo ni kudumisha taasisi ya ndoa ambayo ni msingi wa maisha ya kijamii dhidi ya dhana, sera na siasa potofu zinazokwamisha maisha na utume wa familia kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top