Bikira Maria kupalizwa
mbinguni. Kanisa Katoliki linajivunia kwa imani hiyo kwani linaamini na
kusadiki tendo hili la Mungu kumpaliza mbinguni mwanamke Pekee duniani
aliyeshiriki ukombozi wa mwanadamu.
Ijapo Kanisa linakumbwa na changamoto kutoka kwa watu wanaohoji
na kukataa tendo hili la imani, msimamo wa mafundisho ya Kanisa unabaki
palepale kwani ni kweli Bikira Maria amepalizwa mbinguni.
Fundisho la Kupalizwa Bikira Maria mbinguni mwili na roho,
linatakiwa limakinike kwanza kwa lugha ya kiimani.
Ni hivi, Kanisa Katoliki lina chemichemi moja ya kimungu ya
ufunuo lakini chemichemi hiyo hutiririka kwa mikondo miwili iliyo na thamani
sawa, yaani Maandiko Matakatifu na Mapokeo Matakatifu.
Kwa kushindilia maelezo yangu, katika makala hii, nitawavusheni
hata nje ya mikondo hiyo rasmi. Nia yangu ni kutoa maelezo ya kuwashibisheni
ninyi wasomaji wapendwa.
Kwa faida yetu sote, aheri leo tuanze na maelezo ya Mapokeo
Matakatifu na baadaye tuingie kwenye Maandiko Matakatifu, madhali mikondo yote
miwili itathibitisha fundisho hili hili moja.
Zaidi ya hilo, natumaini kwa mtindo huu wa kulitazama fundisho
hili, nitathibitisha pia kwamba imani ya Kikristo haikuanza na maandishi
isipokuwa na mambo yaliyoshuhudiwa au kuaminiwa na wafuasi wa mwanzo na kisha
wao kutuandikia sisi.
Hivi Maandiko Matakatifu ni mtoto wa Mapokeo Matakatifu, na si
kinyume chake kama wengine wanavyotaka kutuvuruga wenzao kwa hoja na madai
batili. Kuthibitisha hili, Maandiko Matakatifu yenyewe yanakiri kwamba si yote
yaliyofanyika wakati wa Yesu yaliandikwa. Kwa kifupi, ni kwamba yaliyoandikwa
ni baadhi tu ya mengi yaliyoshuhudiwa au kuaminiwa (rej. Yn 20:30-31 na 21:25).
Tusome
sehemu hizo na tuzitafakari bila jazba.
Kumbe, tumeandikiwa hivi: “Basi, kuna ishara nyingine nyingi
alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki
(yaani Biblia au Injili). Lakini hizi zimeandikwa, ili mpate kuamini ya kwamba
Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu na kwa kuamini muwe na uzima kwa jina
lake. Kuna na mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu ambayo yakiandikwa moja
moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu
vitakayoandikwa”.
Mapokeo Matakatifu
Basi, tuanze na mkondo wa Mapokeo Matakatifu. Tukianza na
Mapokeo Matakatifu, ni hivi tangu zamani makanisa ya Mashariki (ya
Kiorthodoksi) na Magharibi (Kanisa Katoliki) yalikuwa yakisherehekea sikukuu
hiyo kwa namna moja au nyingine. Ndiyo maana wakati wa karne ya saba, yaani
enzi za Baba Mtakatifu Sergio, kulikuwa na sherehe ya “Kulala au Kusinzia kwa
Bikira Maria (Dormitio). Baadaye mambo yalihamishiwa tarehe 15 Agosti.
Kumbe, ushahidi wetu wa kwanza ni kutoka kwenye Mapokeo. Mapokeo
ni nini? Ni mambo yale yanayohusu imani ya kikristo ambayo hayakuandikiwa. Na
tukumbuke hapo mwanzo, Ukristo ulienezwa kwa masimulizi ya mdomo tu kwani Yesu
hakuwa na kitabu na wala hakuwaagiza watu waandike habari za maneno na matendo
yake.
Vitabu vya kwanza ni barua mbili kwa Wathesalonike, vitabu
vilivyoandikwa na Paulo kwa hiari yake mwenyewe, yaani pasipo shinikizo la mtu
yeyote. Mitume wote walitumaini masimulizi ya mdomo kwani ukiachilia mbali
Agano la Kale hawakuwa na kitabu chochote kilichohusu habari za Yesu.
Barua hizo ziliandikwa mwaka 50 au 51. Injili ya kwanza ilikuja
mwaka 70 BC yaani miaka kama 37 baada ya Yesu kufa, kufufuka na kupaa mbinguni.
Hiyo ilikuwa Injili ya Marko, zikafuatia Injili za Mathayo na Luka kati ya
mwaka 80 na 85 na mwishowe Injili ya Yohane kati ya mwaka 90 na 100. Kushuhudia
kwamba mitume na wafuasi wa Kristo hapo kwanza walitumaini mafundisho ya mdomo
yaani Mapokea na wakaandika mambo hayo katika miaka ya baadaye soma 1 Kor
11:23, 15:1-3, Gal 1:9.12, Flp 4:9, Kol 1:12, 1 The 1:6 na 2 The 3:6.
Ndipo, kwa kadiri ya Mapokeo ya Wakristo wa karne ya mwanzo,
Bikira Maria alifariki na kuzikwa huko Yerusalemu, karibu na maeneo ya bustani
ya Gethsamane, ambako kaburi lake lipo mpaka leo hii. Tunafahamu Bikira Maria
aliishi duniani na watu walimfahamu vyema katika Kanisa la mwanzo.
Bikira hakuishi peke yake bali aliishi na watu wengine wengi tu.
Yaliyompata watu hao waliyaona, kuyasikia na hata kuyashuhudia. Basi jinsi
alivyoyamaliza maisha yake ya kidunia watu hao wana habari nayo kwani
walikuwepo pamoja naye na si wewe na mimi tunaobisha leo hii.
Bikira Maria aliyamaliza maisha yake kwa kulala au kuzinzia
ambako Mungu alimbadilishia mwili wake wa kibailojia kwenda kwenye mwili wa
kiroho, mwili ambao kila mmoja atauhitaji ikiwa anataka kuishi milele. Hakuna
mtu atakayeweza kuishi milele na mwili huu wa kibailojia. Ni lazima awe na
mwili wa kiroho. Tulio wengi tutaupata mwili wa namna hiyo siku ile ya ufufuko
wa wafu.
Basi, kutokana na maelezo ya watu walioishi na Bikira Maria na
kushuhudia jinsi alivyomaliza maisha yake ya kidunia kwa mtindo wa ajabu Kanisa
linatueleza kwamba sikukuu ya kupalizwa Bikira Maria mbinguni mwili na roho
ilianza kuadhimishwa tangu karne ya sita ambapo ilikuwa ikiitwa kulala usingizi
au kusinzia kwa Maria.
Mapokeo pia yanatupatia sababu kadhaa kuthibitisha kuwa Bikira
Maria alipalizwa mbinugni mwili na roho.
Kimuhtasari, sababu za kupalizwa mbinguni ni kadhaa lakini
tuziweke daima mbele yetu sababu nne: kukingiwa dhambi ya asili, umama wake wa
Mungu (Yesu Kristo), ubikira wake na kushiriki kwake kikamilifu katika kazi ya
ukombozi pamoja na mwanawe. Usihangaike. Nazifafanua hoja sasa hivi.
Kwanza, Bikira Maria hakuwa na dhambi ya asili, kama
tulivyoeleza hapo juu, hivyo hakuwa na doa. Kwa hali hiyo, hakustahili kufa na
kuoza jambo ambalo ni adhabu iliyotokana na dhambi ya asili, adhabu ambayo wewe
na mimi hatukujaliwa kuiepuka. Kumbe, Bikira Maria alizaliwa akiwa na uzima wa
neema ya utakaso. Ndipo, mwili wake haukuharibika. Kwa hiyo, alistahili
achukuliwe mbinguni mwili na roho.
Kumbe, mambo yalianzia kwenye ukweli kwamba tangu milele Mungu
alikusudia kumtakatifuza na kumtukuza Bikira Maria kwa namna ya ajabu.
Alimkingia dhambi ya asili ili Mwana wa Mungu, aliye mtakatifu (rej. Lk 1:35),
afikie patakatifu. Kama ajapo mfalme wa kidunia tu, watu huangaika kukiandaa
chumba atakachofikia, haikuwa zaidi sana kwa ujio wa Masiya, Mtakatifu, Mwana
wa Mungu?
Mbona Rais anapotembelea mahali fulani watu huchonga barabara,
kupaka rangi nyumba na kuandaa kitanda kwa shuka mpya? Sasa Mungu asiandaliwe
mahali anapofikia? Basi, ilimpendeza Mungu kumwandaa Maria kabla Yesu
hajatungwa mimba. Ndipo “akampiga deki sana” ndiyo huko kumkingia dhambi ya
asili inayochafua maelekeo na tabia za watoto wote wa Adamu na Eva.
TUNAKAZIA ukweli wa Bikira
Maria kukingiwa dhambi kabla ya kumzaa mtoto wake mtakatifu. Mtu hawezi
kumpokea mgeni halafu akaanza kukisafisha chumba chake wakati mgeni mwenyewe
amekwisha karibishwa ndani.
Mafundisho haya yamefumbuliwa na Mungu na yamefundishwa na
walimu wa Kanisa tangu mwanzo wa Kanisa. Papa Pio IX, kama mwalimu na mchungaji
mkuu wa Kanisa lote, kwa msaada wa Roho Mtakatifu alitangaza mafundisho hayo
tarehe 8 Desemba 1854. Kwa maneno haya kuwa Bikira Maria amekingiwa dhambi ya
asili yaani ile dhambi tuliyoirithi sisi kutokana na kosa la kwanza
walilolifanya wazee wetu Adamu na Eva.
Bikira Maria alikingiwa dhambi ya asili kusudi awe safi,
mtakatifu, asiye na doa lolote toka mwanzo wa uhai wake ili kutuletea Mkombozi
yaani Bwana wetu Yesu Kristo.
Kuzaliwa kwa Bikira Maria ni kama pambazuko la alfajiri
yaani ujio wake ndio dalili kwamba Mkombozi mwenyewe hawezi kukawia kuonekana.
Kanisa limetunga wimbo huu, “Kuzaliwa kwako, ee Bikira Maria, Mama wa Mungu
kumeleta habari ya furaha kwa watu wote wa dunia, kwa sababu ndiwe uliyemzaa
Jua la Haki, yaani Yesu Kristo Mungu wetu.”
Pamoja na kusema haya yote, hatuna budi kuongeza kwamba
kutokana na matokeo ya Mama Bikira Maria kwa watu mbalimbali hapa duniani mfano
kule Lourdes na Fatima tunapata ushahidi wa ziada kwamba Bikira alikingiwa
dhambi ya asili na pia kwamba alipalizwa mbinguni mwili na roho. Hayo tunayajua
kutokana na mwonekano wake pamoja na kauli zake mwenyewe kwa hao aliowatokea.
Pili, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Mwili wake ulimchukua
mimba Mwokozi Yesu Kristo. Ndipo basi, kutokana na uhusiano wa karibu sana
uliokuwepo kati ya Bikira Maria na Yesu, Yesu asingelisita kuutukuza mwili wa
mama yake uliomchukua mimba.
Tatu, ni kwamba Bikira Maria alibaki Bikira daima. Ubikira
wake haukudhurika. Ndipo basi, ilistahiki kabisa mwili wake ambao haukudhurika
usioze wala kuharibika.
Hatimaye, sababu ya mwisho ni kwamba Bikira Maria,
alishiriki kazi ya ukombozi, yaani alifaulu kuambatana sana na mwanawe.
Aliambatana naye katika furaha na katika uchungu. Akiwa duniani, Mama Bikira
Maria ameshiriki kazi ya ukombozi ulioletwa na mwanaye Yesu Kristo kwa kufanya
yafuatayo: kukubali kumzaa Mkombozi Yesu Kristo, kumtoa Yesu hekaluni,
kuvumilia taabu za Misri, kumtafuta Yesu aliyebakia hekaluni, kumsihi Yesu
awasaidie watu kwenye harusi ya Kana, kushuhudia njia ya mateso ya
mwanawe, kushuhudia kifo cha mwanawe msalabani na hatimaye kushuhudia
mazishi yake.
Hivyo, Bikira Maria ameshiriki katika kazi ya ukombozi ya
mwanawe kwa kukubali kwa hiari yake kuvumilia mambo magumu mengi kwa kuwa Mama
wa Mkombozi (rej Lk 2:35). Kisha ameshiriki katika kazi ya ukombozi pale
alipomtolea Mungu Baba mateso yake pamoja na mateso ya Yesu ili dhambi za watu
ziondolewe.
Alipata taabu tangu utotoni mwa Yesu kwa kulazimika kwenda
naye ukimbizini. Wakati wa Yesu kuutangaza ufalme wa Mungu kulikuwa na matukio
chungu mzima ambayo Bikira Maria, kama mama aliionja vilivyo. Hata pale
msalabani, Bikira Maria alikuwepo chini ya msalaba akiugulia maumivu ya mwanawe
mpenzi ambaye watu walimsulubisha bila huruma na walikuwa wakimkejeli kama
gaidi au mhalifu.
Ndiyo maana ya unabii wa mzee Simeoni ambaye alisema
kwamba upanga wa mateso ungepenya roho yake pia. Hivyo, uhusiano huu wa karibu
ulibidi usiishie hapa duniani bali uendelezwe hata mbinguni. Basi Bikira Maria
amepata tuzo la kushirikiana na Yesu katika taabu na raha. Ni ukweli wa kudumu
kwamba mtu yeyote anayeshiriki katika mapinduzi yoyote yenye mafanikio lazima
atuzwe cheo cha maana.
Acha tuendelee. Ndugu yangu, kama tulivyosema hapo juu,
Mapokeo yametujuza kwamba Bikira Maria alikufa ili abadilishe mwili huu na
kupata mwili wa utukufu wenye uwezo wa kuishi milele. Ndiyo kisa basi, imani
yetu inashuhudia uwepo wa Bikira Maria mbinguni mwili na roho. Basi pamoja na
Yesu Kristo, katika hali ya mbinguni, mtu wa pili mwenye mwili na roho ni
Bikira Maria.
Maandiko Matakatifu
Sasa tuhamie kwenye Maandiko Matakatifu. Wala si siri,
ndugu zangu kwamba Wakatoliki hukabiliwa kila kukicha na madai ya watu
wasiompenda Bikira Maria dhidi ya fundisho la kupalizwa kwake mbinguni mwili na
roho. Katika madai yao, watu wa namna hiyo hudai eti hakuna ushahidi wowote wa
kimaandiko wa kuonesha kuwa Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho.
Yaani hukana yote wakisema kwamba hata kwenye Biblia hakuna dokezo lolote.
Ndipo kwa ujumla watu hao huikana haja ya kuliamini fundisho hilo.
Ndugu zangu msidanganyike, kimaandiko, kuna ushahidi tosha
wa kuonesha kuwa Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho. Madokezo ya
nguvu kwenye Biblia huanzia kwenye Yn 20:30-31 na 21:24-24 hadi kwenye Ufu
12:1-17.
Kisha kuna ushahidi wa kimapokeo kutokana na imani ya kale
kabisa iliyochanua kwenye tangazo rasmi la tarehe 8 Desemba, 1854 na sambamba
na ushahidi huo kuna mwanga katika kitabu kilicho nje ya chemichemi za ufunuo,
ndiyo kitabu cha ‘apokrifa’ kiitwacho Kupalizwa Bikira Maria Mbinguni.
Habari za kitabu hiki zikichujwa sana, ukweli wa kiini
hubaki kuwa Mungu alimpaliza Bikira Maria mbinguni mwili na roho kama zawadi ya
nafasi yake ya kuwa mama wa Yesu Kristo. Basi kwa ushahidi uliopo ipo haja ya
kuliamini fundisho hilo kwani ni fundisho la ufunuo wa kweli.
Sisi sote tunajua kwamba swali juu ya Bikira Maria
kupalizwa mbinguni mwili na roho ni moja ya maswali maarufu sana wanayobandikwa
Wakatoliki. Huulizwa mara kwa mara na watu mbalimbali na kujibiwa na wataalamu
mbalimbali tena kwa mitindo mbalimbali.
Maandiko Matakatifu: Tukienda kwenye Maandiko matakatifu,
tunasoma katika Ufu 12:1-17 habari za mwanamke na joka. Imeandikwa, “Ishara
kubwa ilionekana mbinguni. Mwanamke aliyevikwa jua na mwezi chini ya miguu yake
na juu ya kichwa chake taji la nyota kumi na mbili.”
Kwa hakika, mwanamke anayeongelewa hapa kinabii si
mwingine isipokuwa ni Mama Bikira Maria ambaye baada ya kufika mbinguni
amefanyiwa mambo makuu mno. Kitabu cha Ufunuo wa Yohane ni kitabu cha unabii na
unabii huongelea mambo kwa mtindo usio wa moja kwa moja na hivyo hutakiwa
kueleweka kwa jicho la imani na unyenyekevu wa moyo. Mtu akitanguliza ubishi
hawezi kuuelewa unabii.
Na Titus Amigu
Padri wa Jimbo katoliki Lindi.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni