0
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude amesema amewasamehe wale wote waliomzushia kifo wakati akiwa nchini India akiendelea kupatiwa matibabu kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
Askofu Mkude ameyasema hayo hivi karibuni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrick jimboni Morogoro wakati akitoa shukrani kwa waamini wa Kanisa hilo mara baada ya  misa ya tegemeza Jimbo iliyofanyika kanisani hapo ikiongozwa na Makamu wa Askofu padri Patrick Kung’alo ambapo amesema kuwa kwa kawaida mtu yoyote anayesikia taarifa za kifo cha  ndugu, rafiki au jirani huanza kwa kusinyaa na kuwa na simanzi na majonzi.
Askofu Mkude amesema kuwa taarifa walizozipata waamini kwa uzushi wa msiba wake hata yeye mwenyewe binafsi alizipata akiwa nchini India kwa matibabu ambapo amesema kuwa zilimtia simanzi na huzuni kubwa lakini hakuwa na namna ya kuweza kukanusha.
“Ni habari ya kusikitisha ukisikia mtu unaempenda ameondoka duniani, si habari ya kuchangamsha hata kidogo,” amesema Askofu Mkude.
 Hata hivyo Askofu Mkude amewataka waamini kutambua kuwa duniani wapo wengi na kwamba yapo mengi yanayotokea yakiwemo hayo ya kuzushiana mambo mbalimbali ambapo amesema kuwa hataki kujibu lolote kwa watu wachache waliofanya hivyo hasa usambazaji wa taarifa za uzushi zilizokuwa zimeenea katika mitandao.
 “Kupigana na mtu usiyemjua ni sawa na kupigana na mtu ukiwa gizani utarusha ngumi itaenda hewani, yalimpata kiongozi wetu Yesu Kristo, alipata kashfa na matusi aliyopata wakati wote tena hata alipokuwa msalabani lakini alisema baba wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo, vivyo hivyo nami nimeona dozi yake ni hiyo hiyo,” amesema Askofu Mkude.
 Hata hivyo amesema kuwa baada ya uvumi na uzushi wa taarifa zilizokuwa zimeenea juu ya kifo, alichoamua yeye ni kusamehe na kuacha ambapo amesema kuwa imani ya Kanisa Katoliki  inawaagiza wanadamu kusamehe na kupendana.
 Askofu Telesphor Mkude akizungumza kwa huzuni kubwa amewataka waamini hao waliohudhuria ibada kanisani hapo kuchunguza na kuchagua  kila linalopita masikioni mwao, kuliko kuamini kila jambo wanalosikia masikioni mwao.
 Aidha amesema kuwa  hana budi kuwashukuru watu hao ambapo amesema kuwa  inawezekana kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wakimuombea katika kipindi chote tangu ugonjwa wake na wakazidisha maombi baada ya taarifa hizo lakini pia huenda baada ya uvumi  wa kifo waombaji waliongezeka, hivyo amewashukuru kwa maombi yao.
 Askofu Mkude aliondoka nchini  Tanzania kwenda nchini India kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi Agosti 25 mwaka huu ambapo alikuwa akisumbuliwa na maradhi, amerejea Oktoba 25 akiwa na afya njema na kuendelea na majukumu yake ya kichungaji jimboni humo.

Chapisha Maoni

 
Top