Mwaka mmoja umegota tangu Baba Mtakatifu Francisko alipofanya hija ya kitume Amerika ya Kusini kuanzia tarehe 5 – 12 Julai 2015 kwa kutembelea Equador, Bolivia na Paraguay. Familia ya Mungu katika matatifa haya imefanya kumbu kumbu ya maadhimisho haya, ili kuendelea kuzifanyia kazi changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika nchi hizo.Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea kutoka katika hija hiyo, njiani aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwamba, Amerika ya Kusini ina utajiri mkubwa; ni Kanisa changa lakini imara na thabiti linaloendelea kufanya tafiti ili kuwa na msimamo wa kitaalimungu. Ni Kanisa ambalo lina matatizo na changamoto nyingi pia ambazo zinahitaji kurekebishwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Nidhamu ya Kanisa.
Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri amehitimisha hija yake ya kikazi nchini Paraguay kama sehemu ya kumbu kumbu ya hija ya kitume iliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko nchini humo, mwaka mmoja uliopita. Amewakumbusha vijana kwamba, Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini mwao, aliwataka vijana kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kuwa na moyo huru usiomezwa na malimwengu wala kuwa watumwa wa vitu, bali kusimama kidete kulinda na kutetea utu wao kama binadamu. Vijana waombe kuwa na uhuru wenye mipaka kwani uhuru usiokuwa na mipaka ni hatari kwa maisha ya ujana, huko wanaweza kukumbana na cha mtema kuni!
Kardinali Stella anawataka vijana kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ukweli hata kama katika maisha watashutumiwa, kudhulumiwa hata kunyanyaswa, lakini nyoyo zao daima zitakuwa huru, wataweza kupenda pasi na woga na bila kujibakiza. Moyo wa kiongozi wa Kanisa hauna budi kuwa huru kwa kutambua na kuguswa na mahangaiko ya watu wake tayari kujitosa kimasomaso kulinda na kutetea utu na heshima yao kama binadamu.
Ni moyo ambao uko huru kufuata maelekezo yanayotolewa na Kristo Yesu, Mchungaji mwema, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika huruma na mapendo, tayari kuganga na kuponya madonda ya maisha ya kiroho kwa mafuta ya huruma ya Mungu. Wakleri wanapaswa kuwa ni mashuhuda na chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, hasa pale wanapotekeleza majukumu yao ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!
Kwa namna ya pekee, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nafasi muafaka ya kumwilisha Injili ya huruma ya Mungu kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hasa zile Sakramenti zinazowakirimia waamini huruma ya Mungu, yaani Ekaristi Takatifu inayowapatia waamini chakula cha njiani wanapokuwa safarini hapa duniani bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha unaoponya na kukomboa. Hizi ni Sakramenti zinazozima kiu ya maisha ya kiroho.
Kardinali Stella akizungumza na Majandokasisi wa Seminari ya Kitaifa ya Lambarè amesema, hiki ni kisima cha matumaini ya maisha na utume wa Kanisa la Paraguay. Katika maisha na utume wa Upadre, kamwe hakutakosekama Msalaba, vishawishi na hata pengine hali ya kukata tamaa. Wakleri wanapokumbana na matatizo pamoja na changamoto zote hizi za maisha wanapaswa kumkumbuka Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chemchemi ya maisha ya uzima wa milele. Wakleri wawe na ujasiri wa kupokea na kuambata Msalaba wa maisha, daima wakitafuta ukweli wa maisha na ushuhuda wa Kikristo.
Wakleri wameteuliwa kutoka ulimwenguni kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu, bale wawe ni mashuhuda wa upendo usiogawanyika kwa ajili ya Mungu, Kanisa na Watu wake. Upendo wenye nguvu ya kuweza kutoa matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha; kwa watu wanaoteseka:kiroho na kimwili.
Seminari iwe ni mahali ambapo, Majandokasisi wanapata nafasi ya kufanya hija ya maisha yao, tayari kutoa maamuzi magumu katika maisha yao kwa kuacha yote na kuamua kumfuasa Kristo Yesu katika maisha na wito wa Kipadre, ili kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Ili kufikia maamuzi haya, Majandokasisi wanapaswa kutambua kwamba, ndani mwao kuna nguvu ya Kimungu inayotenda kazi, lakini pia wakati mwingine wanaweza kuelemewa na udhaifu wa kibinadamu. Wawe makini ili wasielemewe sana na mapungufu ya kibinadamu na hivyo kuhatarisha utume wao kama waadhimishaji wa Mafumbo ya Kanisa.
Wakleri wajitahidi kuwekeza mahali salama katika maisha na wito wao, daima wakijiweka chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Kardinali Stella anasema, hapa Wakleri wanapaswa kukita maisha yao katika: Sakramenti za Kanisa kwa kuwa mstari wa mbele kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao; kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao. Wajenge utamaduni wa kuchunguza dhamiri zao, katika ukweli na uwazi mbele ya Mungu na kwa namna ya pekee, Majandokasisi wanahamasishwa kujiachilia mikononi mwa viongozi na walezi wao wa maisha ya kiroho, ili waweze kuwafunda vyema tayari kuwa huru na wazi kwa ajili ya kujisadaka kwa Kristo na Kanisa lake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni