Utangulizi:
Ili
tunufaike na mada hii, hebu tuanze kwa kuorodhesha maswali au dukuduku zote
tulizo nazo kuhusu Mama Bikira Maria. Natumaini baada ya kupitia kurasa hizi
kwa makini tutakuwa tumepata majibu karibu yote.
Baadhi ya maswali
tuliyozea kuyasikia kuhusu Mama Bikira Maria kama shutuma dhidi ya wakatoliki:
·
Kwa nini wakatoliki wanamwomba Maria badala ya kumwomba Mungu
moja kwa moja?
·
Maria ni Bikira daima?
·
Kwanini wakatoliki wanamwita Maria Mama wa Mungu?
·
Wakatoliki wanamwabudu Maria na watakatifu wengine?
·
Yesu alikuwa na ndugu wa kiume na wa kike kwa mama mmoja
(Maria)?
·
Kwa nini Maria alipalizwa mbinguni?
·
Je, Maria alikuwa na hiari kuhusu kukubali au kukataa kuwa Mama
wa Yesu?
·
Je, Maria na Yesu wangeweza kutenda dhambi?
·
Kwanini tunasali Salamu Maria mara kumi na Baba yetu moja tu
katika sala ya Salamu Maria?
·
Kwa nini tuvae skapulari?
·
Kwanini wakatoliki wanaamini na kufundisha vitu ambavyo
havijaandikwa kwenye Biblia? (Yn 21:25, Lk 10:16, 1Timoteo 3:15, 2The 2:15)
·
Wakatoliki wanawaomba wafu?
·
Wakatoliki wanaabudu picha na sanamu?
·
Kusali kupitia watakatifu sio kumwibia Mungu utukufu wake?
·
Nk.
Lengo
kuu la mada hii ni kuwezesha tafakari ya sala ya Salamu Maria.
“Salamu
ewe uliyejaa neema” (Luka 1:28a)
Nilikuwa naangalia televisheni
siku moja, kilikuwa ni kipindi cha mchungaji mmoja maarufu hapa nchini. Niliona
kuwa wakati wa kufanya huduma ya uponyaji na kufukuza pepo, kijana mmoja
aliyekuwa amevaa Rozari shingoni, alijitokeza kwa ajili ya huduma hiyo, na
mchungaji alimwambia aivue Rozari hiyo kwanza kwani ndio kizuizi cha uponyaji
wake, na yule kijana akaivua na kuitupa chini, watu wakaendelea kuikanyaga……..
Nilishituka sana na ilinipa kutafakari tukio hili na mengine yanayofanana na
hayo kwa muda mrefu. Kuna mambo mawili. Inawezekana mchungaji huyu aliogopa
kutoa “huduma” yake kwa mtu aliyevaa Rozari kwa sababu alikuwa anatumia nguvu
inayopingana na Mama Bikira Maria? Au; labda alimwandaa mtu huyu ili apate
nafasi ya kuidhalilisha Rozari Takatifu kwa sababu alitaka kulipiza kisasi kwa
Mama Bikira Maria? Kwa vyovyote huu ni mfano wa matumizi mabaya ya Jina la
Yesu.
Shetani hawezi kumdhuru
mtu mwenye kinga ya Mama Bikira Maria. Mfano B: Msichana mmoja aliyekuwa
anampenda sana Bikira Maria na anaomba ulinzi wake mara kwa mara, siku moja
alitekwa nyara na waabudu shetani ili akatolewe damu ya kafara. Kwanza
walimfungia kwenye chumba huku wakiandaa sehemu ya kumchinjia, kisha wakaenda
kumchukua kwenye kile chumba (muda wote alibaki anasali kwa Bikira Maria).
Wauaji hao walipomwangalia mara anabadilika badilika sura, wakati mwingine
wanamwoma kama yeye, na wakati mwingine wanaona sura yake imebadilika amekuwa
kama Bikira Maria. Ndipo walipomfukuza Yule binti, huku wakimwambia aliyeleta
ile kafara kuwa kafara hiyo haiwafai. Ndivyo yule msichana alivyonusurika kifo.
Mfano C: Kijana mmoja
aliingia mkataba na shetani ili afanikiwe mambo yake, lakini mama yake alikuwa
mtu wa ibada sana kwa Mama Maria, na akawa amemvalisha mtoto wake skapulari ya
Bikira Maria tangu akiwa mtoto, naye hakuwahi kuivua. Baadae shetani
alimfuatilia yule kijana kuhusu mkataba wao kuwa ili yeye afanikiwe duniani,
itambidi ampatie shetani chochote atakachohitaji kwake. Siku moja shetani
alihitaji yule kijana ajiue, na akampeleka hadi kwenye kisima kirefu na kumuamuru
ajitupe humo ili afe. Yule kijana alikaa kwa muda mrefu pembeni ya kisima kwa
hofu kuu ya kifo. Shetani alipomharakisha, kijana akamwambia, mimi naogopa sana
kufa, nashindwa kujitupa humu kwenye kisima, tafadhali nisukume. Shetani
alirudi nyuma na kumwambia, vua kwanza hiyo skapulari kisha nitakusukuma. Yule
kijana mara akakumbuka kuwa anayo kinga dhidi ya shetani, ni hiyo skapulari, na
shetani hawezi kumgusa akiwa ameivaa. Kijana akamwambia shetani kuwa kama
hamsukumi aondoke maana yeye hatajitupa humo kamwe. Shetani baada ya kufanya
vurugu nyingi na kelele za hasira akaondoka na kumwacha kijana peke yake,
hakuweza kumgusa. Baada ya kijana kujikuta peke yake alijikokota hadi kanisani
huku akilia sana akamweleza Padri kila kitu, akaungamishwa dhambi zake zote, na
baada ya hapo maisha yake yote yakabadilika, akiwa anatoa ushuhuda kwa
yaliyomkuta na jinsi alivyonusurika kifo cha mwili na cha roho milele.
Katika Sikukuu ya Bikira
Maria Mkingiwa dhambi ya asili tunamkumbuka Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya
asili. Ni fundisho la Kanisa ambalo kila Mkatoliki
lazima alikubali (Dogma). Sawa. Kama wakatoliki tunajua kuwa Sanduku la Agano
linalonenwa katika Agano la Kale ni kivuli cha Bikira Maria katika Agano Jipya.
Na kwa vile Maria ni Sanduku la Agano katika Agano jipya, ina maana kuwa hana
doa lolote. Kwa sababu, kwa vile Mungu ni Mtakatifu sana, na Mungu ni Roho,
hawezi katika hali yake hiyo kama Roho, kugusana na dhambi, na hivyo hawezi
kuchukua mwili wa kibinadamu kutoka katika chombo kichafu. Kwa hiyo, Maria
hawezi kuwa kwamba alikuwa na dhambi ya asili. Sawa.
Tunakubali yote haya.
Lakini, ili kuelewa
kwanini Maria alikingiwa dhambi ya asili, hatuna haja ya kutafuta majibu
magumu, kwani Malaika Gabrieli anatufunulia haya yote katika salamu yake wakati
Neno (Mungu nafsi ya pili ambaye alikuwa Roho tu) alipofanyika Mwili (na kuwa
Mungu-Mtu). “Salamu, ewe uliyejaa neema! Bwana yu nawe”. Gabrieli anampa Maria
jina la “Aliyejaa Neema”, na cheo hicho peke yake, kinajitosheleza katika
kutujulisha kuwa Maria hana dhambi yoyote.
Inawezekanaje?
Dhambi ni nini kwani?
Eeh., dhambi ni pale
tunapofanya mambo mabaya. Hapana, hayo ni madhara ya dhambi. Dhambi ni nini?
Eeh…, dhambi ni pale
tunapomwacha Mungu na kumgeukia kiumbe. Hapana, hayo ni matokeo ya dhambi.
Dhambi ni nini?
Dhambi ni ugonjwa wa
kiroho, kansa, uchafu uliogandamana nasi, ambao unaziba roho zetu na kutuzuia
kufanya mambo ilivyo sawa. Hapana! Hiyo ni tafsiri potofu iliyozoeleka kuhusu
maana ya dhambi.
Dhambi siyo ugonjwa wa
kiroho. Dhambi siyo kansa ya kiroho. Dhambi siyo uwepo wa kitu fulani ndani
mwetu ambacho hakistahili kuwa humo.
Ila, dhambi ni matokeo ya
ukosefu wa kitu ambacho kilipaswa kiwe ndani yetu. Ni kitu gani hicho?
NEEMA! Dhambi ni matokeo
ya ukosefu wa neema. Kaangalie kwenye Kateksimu yako vizuri utaona jibu hili.
Hivyo, iwapo dhambi ni
ukosefu wa neema, na iwapo mtu anaitwa na Malaika wa Mungu kama “aliyejaa
neema”, ni nini ambacho hakiko kwake? DHAMBI! Ona kwamba, Gabrieli
anamwita Maria “aliyejaa” neema, siyo anayejaa neema, au atakayejaa neema. Bali
aliyejaa neema. Wakati uliopita. Hili ni jambo ambalo lilishafanyika. Maria
amejaa neema. Kama Maria amejaa neema, hakuna nafasi ya dhambi ndani yake.
Sawasawa, lakini Maria
alipataje kuwa aliyejaa neema? Asante kwa kuuliza. Maneno ya Malaika Gabrieli
yanayofuatia yanajibu swali hilo. “Bwana yu nawe”. Ndugu zangu, hiyo ndiyo
maana ya neema wapendwa, uwepo wa Mungu!. Neema maana yake hasa ni “uwepo wa
Mungu ndani ya maisha yetu”. Kwa hiyo, kuwa aliyejaa neema, ni kuwa aliyejaa na
uwepo wa Mungu.
Tunapokeaje neema? Kwa
njia ya Sakramenti.
Maria alipokeaje neema? Kwa njia ya Sakramenti. Eeeh!
Hebu subiri kwanza! Unatuchanganya. Maria hakupokea Sakramenti!...
Ndiyo, Maria alipokea
Sakramenti! Maria alipokea Sakramenti Kuu. Yesu ni Sakramenti ya Milele. Yesu
ni Sakramenti iliyo hai ambaye kutoka kwake Sakramenti nyingine zote hutoka na
kutupa uhai. Na alikuwa katika hali hiyo ya umoja wa kimwili na Sakramenti Hii
kwa miezi tisa mfululizo. Hebu tafakari jambo hili kidogo.
Tuseme mtu anaanza
kupokea Komunyo Takatifu akiwa na umri wa miaka saba, na mtu huyu anahudhuria
Misa Takatifu kila siku kwa maisha yake yote, na anapokea Komunyo kila siku,
mpaka anapofikia umri wa uzee miaka tisini na saba. Tunaamini kuwa kila
tunapopokea Komunyo Takatifu, ambayo ni Mwili na Damu, Roho na Umungu Halisi wa
Bwana wetu Yesu Kristu, tunakuwa katika hali yaa muunganiko wa kimwili na
Mungu, kwa muda wa kama dakika mbili. Sasa tukichukulia kuwa mtu yuko katika
hali ya neema ya utakaso, na mtu huyu akaishi hadi miaka 97, na akaja Misa kila
siku na kokomunika bila kuruka hata siku moja, hakuugua wala kupokea Komunyo
bila kustahili, hakutenda dhambi ili aruke kukomunika, mtu kama huyo atakuwa
amekuwa katika hali ya muunganiko kamili na Mungu kwa kama siku arobaini za
maisha yake. Piga mahesabu. Huu ni kama mfano tu.
Hakuna uwezekano mkubwa
zaidi ya huo ukiangalia hali ya kawaida ya maisha yetu. Maria alikuwa katika
muunganiko kamili na Sakramenti Hai, Mungu wa milele, Neno wa Mungu, Nafsi ya
pili ya Utatu Mtakatifu, kwa muda wa miezi tisa mfululizo!. Ni kama siku 270!
Angewezaje kuwa na upungufu wa neema? Angewezaje kuwa na dhambi?
Enheeee. Sasa
tumekukamata! Kwa sababu Malaika alisema maneno hayo kwa Maria kabla hajapashwa
habari! Unawezaje kusema kuwa alipokea Neema hiyo kutokana na muunganiko wake
na Sakramenti Hai na ya Milele?
Ni kwa sababu daima
tunapaswa kukumbuka kuwa, wakati sisi wanadamu tunafikiria kwa kutumia muda na
nyakati, Mungu hazuiliwi wala kubanwa na muda. Na kama Yesu ni Mungu wa Milele,
Nafsi ya Pili ya Utatu Mtakatifu, basi matendo yake ya wakati uliopo yanaathiri
wakati ujao na wakati ULIOPITA. Lazima iwe hiyo, kama sivyo, basi Yesu siyo wa
milele, na kama Yesu siyo wa milele, sadaka yake pale Kalvari ingalikuwa na
uwezo tu wa kuwakomboa watu waliokufa kabla yake. Na kama ndivyo, imani yetu
haina maana kwa sababu sisi tuliokuja baada ya kile kifo chake Kalvari
hatujakombolewa na tumaini letu katika ufufuko baada ya kufa ni bure.
Kama Yesu ni Mungu, basi
lazima Yesu ni wa milele, na SASA yake inaathiri sio sasa hivi tu bali pia
inaathiri kesho na jana na milele (wakati uliopo, uliopita na ujao). Kwa hiyo
Maria aliweza kuwa “aliyejaa neema” kutokana na muunganiko wake na Sakramenti Hai
na ya Milele, ambayo ni Mwanae Yesu, kabla hata ya Neno
kufanyika Mwili tumboni mwake.
Lakini sisi hatuwezi kuwa
“waliojaa neema”. Zawadi hiyo ilikuwa spesheli kwa ajili ya Maria peke yake.
Tunachoweza kutumainia ni “kujazwa na neema”, na ili hilo litokee inatubidi
tuwe tunashiriki Sakramenti mbalimbali za Kanisa mara nyingi. Kumbuka, mara
nyingi tunashindwa kushiriki Sakramenti za Kanisa na hivyo tunashindwa
kuunganika kimwili na Mungu kwa sababu mbalimbali kama vile kutokwenda Misa
kila siku, kwenda Maungamo mara chache tu na hivyo dhambi zetu zinamzuia Mungu
kutujaza na neema anazotaka kutujalia. Na kama hatuungami mara kwa mara tena au
tunakomunika kwa kukufuru au hatukomunika mara kwa mara, na yote hayo ni muda
ambao haurudi katika maisha yako.
Na sasa tujiulize, ni
namna gani tunapaswa kujitahidi kwa bidii kuhudhuria Misa kila siku, ili
tuunganike na Mungu wetu katika Komunyo Takatifu (Anilaye mimi ataishi milele – Yn
6:48-58). Tunapokula chakula cha kawaida, kile chakula kinameng’enywa
kinakuwa sehemu ya mwili wetu; ila tunapomla Mwana wa Mungu Yesu Kristu, yeye
anatumeng’enya sisi tunakuwa sehemu ya Mwili wake Mtukufu, nasi tutafufuka
pamoja naye siku ya mwisho na kutawala naye milele). Yatupasa kuondoa vizuizi
vyote vinavyotuchelewesha au kutuzuia kupokea Sakramenti za Kanisa.
Kwa njia ya Sakramenti ya
Ekaristi, sisi ni Mwili mmoja ule ule, Mwili wa Fumbo wa Kristu. Kwa sababu
wote tunashiriki mkate mmoja na kikombe kimoja.
Tumwombe Mungu leo,
kwamba Maria, Mama yetu na Mwombezi wetu, atuombee ili sisi wote tujazwe na
neema. Salamu Maria……
Bwana
yu pamoja nawe (Luka 1:28b)
Malaika
anamaanisha nini anapomwambia Maria “umejaa neema”? Tafsiri ya neno neema ni
“uhai wa Mungu ndani mwetu”, kwa hiyo Maria amejaa neema, kwamba amejawa na
uwepo wa Neno wa Mungu aliyefanyika Mtu. Na akiwa amejawa na Neema hiyo, ina
maana kuwa Bwana yu naye. Kwa sababu Neema haiwezi kukaa nje ya uwepo wa Mungu.
Pale uhai wa Mungu ulipo, ndipo hapo Mungu alipo. Neema ni uwepo wa Mungu.
Kwa
hiyo, kwa kuwa amejaa neema, ina maana kuwa Maria kamwe hatakuwa peke yake,
Mungu atakuwa naye daima. Na
hili sio jambo dogo. Turudi katika kitabu cha Mwanzo cha Biblia.
Kila
tunapoadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, tunasoma
kutoka kitabu cha Mwanzo cha Biblia, ambapo Mungu anawagombeza Adamu na Eva kwa
kula tunda lililokatazwa, na anapotangaza kuwa mwanadamu na nyoka daima
watakuwa maadui. Hatuwezi kuelewa vizuri Fumbo la Mungu kufanyika Mtu kama
hatajaelewa vizuri sehemu hii ya kitabu cha Mwanzo cha Biblia na matokeo yake.
[Mwanzo 3: 1-15].
Nini
kinatokea mara baada ya Mungu kumuumba Adamu? Anasema, “Sio vizuri huyu mtu
kuwa peke yake” (Mwanzo 2:18). Na hivyo anamuumba Eva kutoka kwa
Adamu. Na hilo pia ni muhimu. Siku hizi wanaharakati wa kike hawapendi
mstari huo kwenye Biblia kwa sababu wanadhani unakazia kuwa mwanamke ni mdogo
kuliko mwanaume, na kwamba pengine nia ya mwandishi wa sentensi hiyo ilikuwa
kuonyesha ubabe wa jinsia ya kiume. Hio sio sahihi. Hiyo sio maana sahihi ya
mstari huo katika Biblia.
Eva anaundwa kutokana na
Adamu ili kuonyesha kuwa hao wawili ni sehemu moja, wanategemeana (Mwa 2:23).
Wanatokana na nyama ile ile na mfupa ule ule. Kwa sababu tumeumbwa hivyo, ili
tuwe na mahusiano na kila mmoja wetu na pia tuwe na mahusiano na Mungu wetu. Ndio maana Mungu hamuumbi Adamu na Eva namna sawa na
alivyoviumba vitu vingine vyote. Mungu anaongea na vitu vingine na vinapata
kuweko. “Pawepo mwanga” na mwanga unakuwepo, nk. Adamu na Eva wao ni
tofauti. Anawagusa. Anawatengeneza kwa mikono yake, kwa sababu anapenda awe
karibu nao, awe na mahusiano nao, na anapenda wawe karibu na wawe na mahusiano
wao kwa wao.
Katika mazungumzo na
nyoka (Mwa 3:1-15) nani anajibu maswali yote? Eva. Nani yuko kimya?
Adamu. Hatimaye wanaposhawishika kufanana na miungu, nani anapokea lile tunda?
Eva. Nani anapokea tunda kama kipofu? Adamu. Anafuata mkumbo tu. Mungu
anapowahoji, anamwita nani? Adamu. Adamu anamlaumu nani? Eva na Mungu.
Lakini Mungu anapomhoji
Eva, Eva anafanya nini? Eva anasema kila kitu. Katika mazungumzo haya yote Eva
ndie jasiri. Adamu ni mfano wa mume dhaifu, na ndio maana tukio hili
limerekodiwa katika Biblia kama “dhambi ya Adamu” na sio “dhambi ya Eva”, kwa
sababu Adamu sio tu alishindwa kumtii Mungu, bali pia alishindwa katika wito
wake.
Kwanini Adamu hakuongea
na yule nyoka? Kwa nini Adamu hakumsaidia mke wake? Haikuwa vigumu sana kufanya
hivyo, angeweza kumwambia tu, “Njoo Eva, twende zetu. Sihitaji kula tunda saa hizi”.
Hii ndio sababu anguko la wazazi wetu wa kwanza lilitokea. Mungu alimwumba Eva
kutokana na nyama ile ile aliyokuwa nayo Adamu, ili wawepo kila mmoja kwa ajili
ya mwenzake. Na Adamu alishindwa kuwepo kwa ajili ya mke wake wakati Eva
alipomhitaji zaidi, wakati wa unyonge wake. Alimwacha peke yake! Ndio, Adamu
alikuwa pale, ila hakufanya uwepo wake uwe wa msaada kwa Eva. Ndio maana Bwana
Mungu alisema, “Sio vema mtu huyu akae peke yake”, kwa sababu Mungu alifahamu
kuwa vishawishi vya shetani vingeweza kumshinda mtu mmoja kama yuko peke yake.
Tunahitaji kusaidiana kama Jumuiya. Tunahitaji kuwa karibu na watu wema ili
tuweze kudumu katika njia ile nyembamba na iliyonyooka.
Na ninaposema “kuwa na
mahusiano”, simaanishi mahusiano ya wanandoa kwa maana ya tendo la ndoa nje ya
ndoa. Kuna namna nyingi za kuwa na mahusiano au ukaribu na watu bila kufanya
tendo la ndoa. Unaweza kufanya tendo la ndoa na mtu usiyemfahamu bila kuwa na
ukaribu wowote naye, akaendelea kuwa mgeni kwako. Nadhani nimeeleweka.
Kwa hiyo, dhambi ya asili
ilitokea kutokana na kukosekana kwa mahusiano. Nini kinatokea baada ya hapo?
Adamu na Eva wanajifunika na majani ya miti. Ni kama wanajificha zaidi kwa kila
mmoja wao (wanafichana sehemu zao za siri).
Kisha wanajificha kutoka
kwa Mungu. Mungu alituumba ili tuwe na ukaribu naye na pia tuwe na ukaribu sisi
kwa sisi. Kilichoharibu mpango huo wote ni matokeo ya dhambi. Hadi leo dhambi
ina matokea makuu mawili yale yale: Inaharibu uhusiano wetu na Mungu, na
inaharibu mahusiano yetu sisi kwa sisi.
Na mambo haya mawili
yanarekebishwa kupitia Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili. Kwa sababu
Maria amejaa kabisa neema ya Mungu, na Mungu yu pamoja naye, Neno wa Mungu
anamuingia kwa njia ya Roho wake Mtakatifu, na Mungu na Maria wanakuwa ni kitu
kimoja. Mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu yanarejeshwa.
Uhusiano huo na Mungu
unatufikia sisi kwa njia ya Ekaristi Takatifu. Sio uhusiano kamili, na
hautakuwa kamili, hadi tutakapofika mbinguni, lakini ule ufa kati ya Mungu na
sisi ulizibwa, kwani kwa njia ya Ekaristi tunakuwa nyama ile ile na mfupa ule
ule sisi na Mungu. Sisi kama mtu mmoja mmoja lakini zaidi sisi kama Kanisa,
tunakuwa Mwili mmoja na Mungu. Soma tena (Mwa 2:23). Mimi napenda
kufikiria kuwa ni Yesu atuambia maneno hayo hasa mara baada ya kukomunika.
Akiwa pale Msalabani,
Yesu alimwambia Maria, “Mwanamke, tazama mwanao”, kisha akamwambia Yohana, yule
mwanafunzi aliyempenda, “Mwana, tazama Mama yako” (Yn 19:26-27). Yesu
anamwita Maria “Mwanamke”, ni neno lile lile ambalo Maria anaitwa na Mungu
katika kitabu cha Mwanzo (Mwa 3:15). “Mwanamke”. Kwa hiyo, kama vile
ambavyo Eva alikuwa mama wa kimwili wa sisi wote, ndivyo hivyo hivyo Maria
anakuwa Mama yetu wa kiroho sisi wote. Na hii inawezekana kwa njia ya Kanisa.
Kwa njia ya Kanisa sisi ni wanafamilia moja tena kama ilivyokuwa hapo kwanza.
Shetani hana nguvu nasi
tena, ndugu zangu, kwa sababu, hakuna hata mmoja wetu mwenye sababu ya kuwa
peke yake tena. Kwa njia ya Ekaristi, tuna uhusiano na Mungu (uhusiano wa damu
na wa nyama), na kwa njia ya Kanisa tuna uhusiano na kila mmoja wetu. Kitu
pekee kinachoharibu uhusiano huu ni dhambi, na tunayo Sakramenti kwa ajili hiyo
pia.
Sasa kwa sababu ya Bikira
Maria kukingiwa dhambi ya asili, kupitia Ekaristi sisi nasi tunaweza kujaa
neema. Sasa, kwa sababu ya Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili, kupitia
Kanisa lake, Bwana yu pamoja nasi pia.
Mama wa Neno aliyefanyika
Mtu, Maria Imakulata, utuombee.
Umebarikiwa kuliko wanawake wote (Luka 1:28c)
Kila
wakati tunaposikia neno “umebarikiwa” likitumika katika maandiko, linamaanisha
mambo fulani. Kimsingi linamaanisha muunganiko na Mungu, au mahusiano ya
kipekee na Mungu. Maneno “umebarikiwa kuliko wanawake wote” hayasemwi na
Malaika Gabrieli wakati Neno anapofanyika Mwili, bali yanasemwa na Elizabeti,
wakati Maria anapomtembelea kumsaidia katika ujauzito wake.
Luka 1:26-44.
Sasa
tuangalie jinsi hii inavyotokea. Maria anasafiri hadi nchi ya milimani na
kumwamkia Elizabeti wakati anapoingia nyumbani kwake. Mara Elizabeti anaposikia
sauti ya Maria anapomsalimia, kitoto kichanga tumboni mwa Elizabeti, Yohana
Mbatizaji, kinaruka. Hapo ndipo Elizabeti anapojazwa na Roho Mtakatifu na
kusema kwa sauti: « Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye mzao wa tumbo lako
amebarikiwa! ».
Kwa
hiyo sehemu ya kwanza ya « Salamu Maria », ni majumuisho ya jina
ambalo Malaika Gabrieli anamwita Maria, na jina ambalo Elizabeti anamwita.
Jinsi ile ile ambavyo Malaika Gabrieli anampa jina Maria mara ya kwanza
anapokutana naye « uliyejaa neema », ni kwa jinsi hiyo hiyo naye
Elizabeti anampa Maria jina mara ya kwanza anapokutana naye
« uliyebarikiwa ».
Lakini
Elizabeti hatoi maneno haya kwa hiari. Yote ni maneno ya Roho Mtakatifu. Bila
shaka Bwana alimwambia Malaika nini cha kumwambia Maria anapofika kwake.
Elizabeti anapoongea kwa kuangaziwa na Roho Mtakatifu inahitaji maelezo zaidi
kidogo. Kwanza Elizabeti anasikia sauti ya Maria. Anasikia sauti yake yeye
aliyekingiwa dambi ya asili. Anasikia sauti ya Bikira asiye na dhambi, ambaye
sasa ana mimba ya Mungu, Neno aliyefanyika Mwili. Anasikia sauti hii na mara
moja anaitikia.
Mwitikio
huu unatoka kwake ? Hapana, mwitikio huu wa gafla hautoki kwake, unatoka
kwa mtoto wake, ambaye ndie atakayefungua njia, nabii wa Neno aliyefanyika Mtu.
Manabii walikuwa hawaongei vile wanavyojisikia wao. Walipofanya hivyo,
walijikuta kwenye shida kubwa. Ilibidi waseme tu kile ambacho Roho wa Mungu
aliwaamuru. Kwa hiyo Elizabeti anaposikia salamu ya Maria, Yohani Mbatizaji nae
anaisikia, na anaruka kwa furaha.
Tumezoea
kumsikia Yohane Mbatizaji akihubiri kwa ukali kuhusu toba, lakini kumbe mara ya
kwanza tunapokutana naye, tunamkuta katika tendo la kumsifu Mungu. Yohane
anaporuka kwa furaha, Elizabeti anajazwa na Roho Mtakatifu, na Yohane, ambaye
yumo tumboni mwake, naye anajazwa na Roho Mtakatifu. Saa ile ile, Yohane
Mbatizaji anakuwa Nabii, na kwa vile Yohane bado alikuwa hana sauti ya kutolea
unabii wake, mama yake, Elizabeti, anamsaidia. « Umebarikiwa wewe kuliko
wanawake wote ! ».
Mahali
pengi katika Maandiko Mungu anatumia mfano wa mama na mtoto, kuonyesha ukaribu
uliopo kati yake na sisi viumbe vyake.
[Kuna
watu wengine wanajiita wakristu lakini wanadhani Biblia haijakataza utoaji wa
mimba. Upofu huo!. Huko ni kutoyajali Maandiko].
Kwa
hiyo Maria amebarikiwa, lakini kwa nini amebarikiwa? Siku moja mwanamke mmoja
alimwambia Yesu, « Limebarikiwa tumbo lililokuzaa, na matiti
yaliyokunyonyesha ! » (Lk 11 :27-28). Maneno hayo ni kama
marudio ya maneno ya Elizabeti. Hata hivyo Yesu anajibu, « Wamebarikiwa
wale wote wanaolisikia neno la Mungu na kulishika ».
Je,
Yesu anabishana na maneno ya mwanamke huyu? Je, Yesu hapa anasema kuwa Maria hajabarikiwa ?
Hapana, ila wakati huohuo, hapendi watu washindwe kuona jambo hili kwa upana
wake. Sababu inayomfanya Maria awe aliyebarikiwa, ni sababu hiyo hiyo ambayo
inaweza kutufanya kila mmoja wetu abarikiwe. Maria alilisikia neno la Mungu, na daima akalishika,
Maria ndiye Mfuasi Mkamilifu. Daima anayafikiria matukio yaliyotokea katika
maisha ya Mtoto wake, Neno wa Mungu.
Bwana
Yesu anapata chakula cha jioni kwa mmojawapo wa Mafarisayo, na mmoja wa wageni
anamwambia, “amebarikiwa yeye atakayekula katika ufalme wa Mungu”. [Luka
14:15-24]. Yesu anafanya nini? Anatoa mfano wa mfalme aliyeandaa karamu kwa
ajili ya mtoto wake, na wageni walioalikwa wakakataa kuja, kwa sababu hii au
ile, hadi mfalme kwa hasira anawaamuru watumishi wake kuwatafuta na kuwaalika
watu wote mtaani, sokoni, vijijini na vichochoroni ili nyumba yake ijae. Mfalme
akaapa kuwa hakuna hata mmoja kati ya wale walioalikwa atakayeonja karamu yake.
Wale
wageni waalikwa walifanya nini kilichomwuudhi mfalme? Walitoa ahadi ambayo
hawakuitekeleza. Waliweza kupata visingizio na mambo mengine muhimu kuliko ule
mwaliko waliokuwa wamepata. Nasi kwa njia ya ubatizo, tumeitikia wito wa karamu
ya mbinguni, lakini mara nyingi tunatafuta visingizio vingi vya kutufanya
tusiitikie wito huo. Maria alifanya tofauti. Daima aliyaitikia mapenzi ya Mungu
hadi Kalvari.
Ni
wapi tunaliona neno “umebarikiwa” likitumika zaidi? Kwenye heri nane bila shaka
(Mathayo 5:3-10). Biblia nyingine neno “heri” linatumika kama mbadala. Wamebarikiwa
wale wenye umaskini wa roho, wamebarikiwa wale walio wanyenyekevu.....”.
Ukichunguza heri zote hizi, utaona kuwa Maria aliziishi zote kwa ukamilifu.
Ndio maana alibarikiwa, na ndivyo jinsi hiyo hiyo tunavyoweza nasi kubarikiwa.
Lakini, sio “umebarikiwa
kuliko watu wote, au wanadamu, au viumbe”. Ni “umebarikiwa kuliko wanawake
wote”. Kwa nini wanawake tu?
Maria amebarikiwa kuliko
wanawake wote, kwa sababu amebadilisha laana ya Eva kuwa Baraka. Na Adam,
ambaye alikuwa chini ya laana hiyo, naye amebarikiwa kwa sababu ya Maria.
Kweli Maria amebarikiwa
kuliko wanawake wote. Kupitia kwake, Baraka za Mungu Baba zimewafikia wanadamu,
na kuwaweka huru na laana iliyowafuatilia tangu dhambi ya Adamu.
Kupitia kwa Maria viumbe
vyote vimebarikiwa, kwani uzao wake unabariki ulimwengu mzima na kuukomboa
kutokana na laana. “Mwanadamu ni nani ee Bwana hata umwangalie?”(Zaburi
8:4-5).
Maria anatimiza kila wito
wa mwanamke kwa ukamilifu. Maria ni Bikira, aliyejitoa kwa Bwana, tena Maria ni
mke wa Yosef, aliyeozwa katika ndoa, Maria ni Binti wa Mungu Baba Mwenyezi,
tena Maria ni Mama wa Mungu Mwenyezi.
Maria ni ndugu kwa
watakatifu na kwa wadhambi. Ona kuwa, ni kina nani wanasimama pamoja na Maria
chini ya Msalaba pale Kalvari? Ni Maria Magdalena, na Maria wa Kleofasi.
Maria watatu wapo Kalvari. Maria wa Kleofasi ni binamu wa Maria, ndugu yake wa
damu. Maria Magdalena ni mdhambi aliyetubu, sasa ni ndugu wa Maria kwa njia ya
damu ya Mwanakondoo. Maria ni ndugu yao wote. Wanatuwakilisha na sisi kuwa tu
ndugu zake wapendwa Mama Maria katika utawala wa Mungu Mwenyezi.
Mambo haya yote
yanamfanya Maria awe Mbarikiwa, na yote yamefungamana na mzao wa tumbo lake,
Yesu.
**********************************************************
EVA WA
AGANO JIPYA
Mwanzo 3:15, na 3:20, Ufu
12:1-6.
Fananisha Eva na Maria.
Maria ni Eva Mpya. Yesu ni Adam mpya. Maria alijinyenyekesha kabisa
(alijifahamu kuwa hana chochote bila Mungu Mkombozi wake - Soma Luka
1:46-48) na hivyo Mungu alipokuta moyo /kikombe chake ki tupu kabisa,
akaweza kumjaza na neema zake hadi kikombe chake kikafurika. (Kizuizi cha neema
za Mungu ni u-mimi tunaoshindwa kuutoa kwenye nafsi zetu, tunashindwa kujimwaga
kabisa kwa Mungu kwa kuyakataa mapenzi yetu yote na kumwachia Mungu atende
anayotaka katika maisha yetu. Kwa sababu tumepungukiwa na neema. Na hili
tumeshalijadili hapo kabla).
Uzao wa Eva ulilaaniwa,
hapa tunaona kuwa uzao wa Maria umebarikiwa. “na Yesu uzao wa tumbo lako
umebarikiwa” Maria kama Mama wa kiroho wa wote walio hai, hapa tunamwona pia
kama Mama wa Adamu. Neno “Yesu” hapa lina maana pia ya Adamu wa kwanza, pia
lina maana ya mimi na wewe. Unaweza kuweka jina lako hapo na kutafakari hiyo
sentensi kwa mwanga huo kwa sababu kupitia uzao wa Maria ambao ni Yesu, sisi
nasi tumebarikiwa. Yesu ni Adam wa pili. Vitu vyote viliumbwa kwa ajili ya
Adamu, alipewa hata jukumu la kuwapa viumbe vyote majina, na jina alilowaita
Adamu likawa jina lao hata leo (Mwanzo 2:20). (maana, Adamu akikuita
ndege utaanza kuruka angani nakuishi kama ndege).
Katika Agano Jipya
tunaona kuwa Maandiko yanasema kuwa Yesu ndiye Adamu wa pili (au Adamu Mpya, au
Adamu wa mwisho – 1 Wakorintho 15:45, Warumi 5:12-19, Kumb 19:21,
Waebrania 10:12, 1 Wakorintho 15:22, nk). Vitu vyote vimeumbwa kwa ajili ya
Yesu (Wakolosai 1:16). Sisi wote na viumbe vyote tumeumbwa naye na kwa
ajili yake. Adamu huyu mpya ( naye anatuita kwa namna yoyote apendayo na jina
analotupa ndilo litakuwa jina letu milele na hakuna wa kulibadilisha.
Akikubariki hakuna wa kukulaani. Huyu ni Adam Mpya na wa milele. Adam wa kwanza
alikuwa kiashiria tu cha Adam huyu. Yesu hawezi kuwa Adamu mpya bila kuwa Mwana
wa Maria, ambaye kupitia kwake yeye Eva wa Pili, anapata Mwili wa kibinadamu
kupitia unyenyekevu wa Maria (utupu wa Maria kuweza kuruhusu kujazwa na uwepo
wa Mungu kwa asilimia 100%, “naye Neno akafanyika Mwili, akakaa kwetu”).
Nyoka amemdhibiti Eva,
ila Maria amemkanyaga nyoka, hataruhusu ushindi wake. (Haya mambo kibinadamu
yanatokea karne nyingi kati ya tukio moja na lingine, lakini katika ulimwengu wa
roho, mambo haya yanatokea wakati ule ule. Ndio maana Mungu alisema “nitaweka
uadui kati yako wewe na huyo mwanamke (angalia kuwa hasemi “huyu mwanamke”,
akiashiria kuwa alikuwa anamaanisha mwanamke tofauti na Eva), kati ya uzao wako
na uzao wake” na hapo Bwana Mungu alikuwa anazungumza na Eva na nyoka kuhusu
mwanamke ambaye uzao wake utakikanyaga kichwa cha shetani).
*********************************************
Yoh 2:4 , 19:26 Yesu
anamwita Maria “mwanamke” [kama ambavyo aliitwa katika Kitabu cha Mwanzo
3:15. Isaya 7:14,Mathayo 1:23] “Mungu pamoja nasi,
Immanueli”
Luka 1:35 Na
kile kitakachozaliwa kwako kitaitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu. - “Theotokos”
(Mama wa Mungu).
“Aliyejaa neema”
inatumika tena mahali fulani katika Biblia mara moja tu, kumhusu Yesu (Yohana
1:14)
Elizabeti anamsifia Maria
kwanza kabla ya kumsifu Yesu. Sisi nasi twaweza kupitia kwa Maria kwenda kwa
Yesu.
Mambo ya Nyakati 15: (hasa
kuanzia aya ya 14…. Pia sura ya 16) - tunaona kuwa
Wayahudi walionyesha heshima ya kipekee kwa Sanduku la Agano (la Kale) – ibada,
mavazi rasmi, nyimbo, vinubi, matarumbeta, nk. Hata sisi tunapaswa kuonyesha
ibada ya kipekee kwa Sanduku la Agano Jipya.
Luka 1:39 / 2 Samweli
6:2. Maria aliondoka na kwenda / Daudi aliondoka na kuliendea
sanduku la Agano.
Luka 1:41 / 2 Samweli
6:16 Yohana Mbatizaji / Daudi anaruka kwa furaha mbele ya
Sanduku la Agano. Nasi inatubidi turuke kwa furaha mbele ya Maria, au
tunapoisikia sauti au uwepo wa Maria turuke kwa furaha nafsini mwetu.
Luka 1:43 / 2 Samweli 6:9.
Inakuwaje Mama / Sanduku la Agano la Bwana kunijia? Ni fursa takatifu Mama yetu
anataka kuja kwetu ili kutupeleka kwa Kristu.
Luka 1:56/2 Sam 6:11 na 1
Nyakati 13:14. Mama /Sanduku la Agano lilibakia katika nyumba ile kwa muda
wa miezi mitatu.
Maria alijifungua bila
uchungu (Isaya 66:7) kwa sababu uchungu wa uzazi ni matokeo ya dhambi ya
asili ambayo hakuwa nayo. Ila, Maria anatuzaa sisi wengine wote (ndugu zake
Yesu) kwa uchungu mkubwa pale Kalvari chini ya Msalaba. Anatuzaa katika uzima
wa milele (Ufu 12:4).
Ufunuo 12:13-16 tunaona
kuwa shetani anaendelea kujaribu kumdhuru Maria hata baada ya kuzaliwa Mwokozi.
Hii ni kuthibitisha kuwa lengo la shetani sio kumwangamiza Yesu peke yake, hata
Maria ni wa hatari kwa mipango yake. Hii ni kwa sababu Mungu amempa Maria uwezo
mkubwa wa kutuombea (ni kama kusema kuwa kwa sasa Maria bado ni mjamzito, sisi
wote tuko tumboni mwake, na atatuzaa kwenye uzima wa milele kwa uchungu mkubwa,
na sisi kama Kanisa tutapelekwa sehemu ambayo Mungu alishatuandalia tangu
kuwekwa misingi ya dunia) Ufu 12.
Nafasi ya Malkia katika
ufalme: 1 Wafalme 2:12-20
Yesu ni Mfalme wa wafalme
na Maria ni Mama wa Mfalme huyu, hivyo ni Malkia. Ukisoma Biblia Agano la Kale
hasa kitabu cha Wafalme utaona kuwa kihistoria mama wa Mfalme alikuwa na Cheo
kilichotambulika kisheria katika Ufalme wa Daudi. Mfalme Sulemani ndie
aliyeanzisha cheo hiki. 1 Wafalme 2:12-20….
Baada ya Ufalme wa
Sulemani wafalme waliomfuata waliendeleza mila hii. Mama wa Mfalme ndie alikuwa
msiri wa Mfalme, mshauri mkuu na cheo chake kilikuwa muhimu sana kiasi kwamba
majina ya Malkia wote yaliorodheshwa katika kitabu cha Wafalme wa Yuda (1Wafalme
14:21, 15:13, 2 Wafalme 12:1, 14:2, 15:2, nk)
Zaburi 45:9, 1 Wafalme
2:17, 20. Mfalme hamkatalii Malkia chochote kwa mila za Wayahudi.
1 Wafalme 2:18.
Malkia anawaombea watu wake.
1 Wafalme 2:19 Mfalme
anamheshimu Malkia kwa kumketisha mkono wake wa kuume.
2 Kumb 22:10 –
Malkia anaweza kufanya mambo makubwa katika utawala wa Mwanae (hata kuangamiza
ufalme wote kama akikasirika. Andiko hili halikuwekwa kwenye Biblia kwa bahati
mbaya. Tunaye Malkia katika Agano Jipya, huyu wa Agano la Kale ni kivuli /
kiashiria tu cha mambo ya umilele.
Ndugu wa Yesu je????
Ezekiel 44:2.
Ezekiel anatabiri kuwa hakuna binadamu atakayepitia mlango atakaopitia Bwana
kuingia ulimwenguni. Huu ni utabiri kuwa Maria ni Bikira daima. Mama Maria hana
watoto wengine kimwili ila ni Yesu tu. Mt. Yosef kama Myahudi mcha Mungu (Roho
Mtakatifu anamwita “mtu wa haki” – Mathayo 1:19) alifahamu andiko
hili vizuri sana, na alipofahamu kuwa mimba aliyo nayo Maria ni kwa uwezo wa
Roho Mtakatifu, alijua kuwa asingeweza au kuthubutu kumkaribia Maria kimwili
kamwe maisha yao yote.
Yohana 7: 3-4, Marko 3:21. Wadogo
zake Yesu wasingeweza kumgombeza kaka yao mkubwa kama kweli ni ndugu wa tumbo
moja kwa sababu kufanya hivyo kwa mila za Wayahudi ni ukosefu mkubwa wa
nidhamu.
Yohana 19:26-27. Maria
angekuwa na watoto wengine Yesu asingeweza kumrithisha Mama yao kwa rafiki yake
Yohana ilhali watoto wengine wapo, hiyo ni kukiuka mila za Wayahudi na
kuwadharau ndugu zake. (Tunajua kuwa Yosef alishafariki dunia Yesu akiwa na
miaka 29, kabla hajaanza kazi yake rasmi, hivyo Maria alikuwa mjane wakati huu
(alikuwa na umri wa miaka kama 50 hivi), na alihitaji mwangalizi. Japo pia hapa
Yesu alikuwa na maana pana zaidi ya kiroho kwa kumpa Mama yake kwa ‘yule
mwanafunzi aliyempenda).
Yohana 19:25, Maria
mke wa Kleofasi ni dada wa Bikira Maria. Mathayo 27:61, 28:1 –
Maria mke wa Kleofasi ndie Yule “Maria mwingine:.
Mathayo 27:56; Marko
15:47. Maria mke wa Kleofasi ni mama wa Yakobo na Yosef. Hivyo hawa
ni binamu zake Yesu na sio wadogo zake kwa mama mmoja.
Mahali pengine neno
“ndugu” linatumika bila kumaanisha ndugu wa damu mfano,
Luka 1:36,
Luka 22:32,
Matendo
1:12-15, 23, 32, 28:17, 21.
Warumi
7:26, 11:1, 13:15, 38, 15:3, 23, 32, 28:17, 21.
Warumi
9:3, Mwanzo 11:26-28, 13:8,
14:14, 16, 29:15.
2
Samweli 1:26,
1
Wafalme 9:13, 20, 32. Tobiti
5:11,
Amosi
1:9.
CHANZO CHA HABARI NI http://mkatolikileotafakari.blogspot.com/
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni