0
Waandaaji wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Cracovia, Poland kuanzia tarehe 26- 31 Julai 2016 wameweka pia masalia ya Mtakatifu Maria Magdalena, mtume wa mitume na shuhuda wa huruma ya Mungu, kama mfano bora wa kuigwa kwa vijana kama sehemu ya mchakato wa majiundo ya kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Kwa mra ya kwanza, Kanisa hapo tarehe 22 Julai 2016 limeadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Maria Magdalena mtume wa mitume.


Masalia haya yaliyotolewa kwenye Jimbo Katoliki la Frèyus Toulon, Kusini mwa Ufaransa yatahifadhiwa kwenye Kanisa la Mtakatifu Kasmiri linalohudumiwa na Wafranciskani, huko Cracovia. Lengo ni kuwasaidia vijana kutafakari maisha ya Mtakatifu Maria Magdalena, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuabudu, kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa njia ya maisha yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, tema inayoongoza maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani.
Taarifa inaonesha kwamba, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kutakuwepo pia masalia ya Watakatifu Faustina Kowalska, Yohane Paulo II, Mtakatifu Marximilliano Maria Kolbe, shuhuda wa mateso ya Auschwitz, ambaye kwa mwaka 2016, Kanisa linakumbuka miaka 75 tangu alipoyamimina maisha yake kwa ajili ya ushuhuda wa Injili ya upendo. Kuna masalia pia ya Mtakatifu Piergiorgio Frassati, kijana alionesha na kushuhudia moyo wa huruma kwa maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii: kiroho na kimwili.
Huyu ni kijana ambaye hakuwa na utajiri wa mali, lakini aliweza kusadaka muda, maneno na uwezo wake wa kusikiliza shida za watu kwa umakini mkubwa, kiasi hata cha kuacha chapa ya kudumu kwa wasikilizaji wake. Leo hii kuna watu wanaoelemewa na upweke hasi, kiasi cha kuwatumbukiza katika utamaduni wa kifo! Ni kijana aliyewahudumia maskini kwa moyo wa huruma na upendo, bila kujitafutia “ujiko” bali akatekeleza yote kwa sifa na utukufu wa Mungu. Kama shuhuda wa Injili ya upendo, akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 24 tu!
Huyu ni mfano wa kuigwa na vijana wote wa kizazi kipya; wale waliobahatika kwenda Poland, wale wanaofuatilia maadhimisho haya kwa njia ya mitandao ya kijamii hata na wale ambao pengine hata hawajui kile kinachoendelea kwa sasa huko Jimbo kuu la Cracovia, nchini Poland.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

    Chapisha Maoni

     
    Top