0
Vijana wanaendelea kuchangamka ili kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, katika Sala na Ibada mbali mbali, mambo msingi yanayowawezesha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya huruma na upendo. Kuna vijana ambao wamekuwa ni washiriki wakubwa wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kuanzia kule Madrid, Rio na Cracovia. Hawa ni wale ambao wamegundua siri ya umoja, udugu na mshikamano katika Kristo Yesu.
Hawa ni vijana ambao wamejiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kwa sasa wako tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao, kwani wameonja huruma ya Mungu katika maisha na sasa wanataka kuwashirikisha wengine pia hii siri kubwa ya maisha ya kiroho hata katika mambo madogo madogo ya maisha. Huu ni ushuhuda ambayo umetolewa na mwakilishi wa vijana waliokuwa wanajitolea kwa ajili ya huduma kwa vijana huko Cracovia. Na kwa njia hii, wameonja ndani mwao, amani, furaha na uhakika wa maisha na kwamba, Mungu ana mpango na kila kijana.
Wanasema, pale vijana wanaposhiriki katika sala, tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, wanajisikia kuwa kweli ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa. Nje ya mambo haya msingi, vijana wanajisikia kuwa ni wakavu pasi na dira wala mwelekeo wa maisha. Vijana wanakumbushwa kwamba, pasi na Kanisa watanyauka katika maisha yao ya kiroho na huko watakiona cha mtema kuni! Vijana wamejifunza kuwa na imani na matumaini hata katika magumu ya maisha. Katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, wamejifunza kujenga na kudumisha: urafiki, miito na kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa.
Kijana mmoja kutoka Panama anasema, anamshukuru Mungu kwa kumkirimia nafasi ya kushiriki maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa njia hii amebahatika kupta mke na familia na sasa anajiandaa kupewa Daraja la Ushemasi wa kudumu ndani ya Kanisa. Huyu ni kijana ambaye tangu mwaka 2002 amekuwa akishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani kwa njia ya huduma inayomwilishwa katika matendo ya huruma pamoja na kupanua wigo wa mafungamano na mahusiano ya kijamii mambo yanayofumbatwa katika fadhila za Kikristo.
Kijana huyu anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kumkirimia neema ya kuendelea kuwa mwaminifu katika maisha na wito wake kama mwamini mlei anayetaka kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama mtume na mmissionari wa huruma ya Mungu. Lengo ni kumwilisha Injili ya furaha, huruma na matumaini kwa jirani, lakini zaidi kwa kupenda na kudumisha familia ambayo kimsingi ni shule ya ukarimu, upendo na uaminifu. Kijana anasema, yeye pamoja na familia yake wanataka kutumikia Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

karibu utembelee https://ludovicktmedia.blogspot.com/ kwa habar za dini

Chapisha Maoni

 
Top