Kardinali Gerhard Ludwig Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa anasema, Waraka mpya wa “Iuvenescit Ecclesia” “Upyaisho wa Kanisa” uliochapishwa na Baraza lake na kuzinduliwa rasmi Jumanne, tarehe 14 Juni 2016 unawahamasisha Maaskofu mahalia kuangalia uhusiano uliopo kati ya viongozi wa Kanisa na vyama pamoja na mashirika ya kitume yaliyoidhinishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko.Maaskofu wanayo dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, vyama na mashirika haya mapya ya kitume yanasaidia mchakato wa kulipyaisha Kanisa katika maisha na utume wake. Mashirika na vyama hivi vya kitume ni zawadi inayoweza kusaidia kuchachua imani ya familia ya Mungu kwenye Makanisa mahalia. Hii inaonesha jinsi ambavyo Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anavyothamini mchango wa vyama na mashirika ya kitume, zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa la Kristo kwa ajili ya roho za waamini wanaomtumainia Mungu katika maisha yao na kwamba, huu ni msaada mkubwa kwa familia ya Mungu ambayo kimsingi ndiyo mlengwa mkuu wa vyama na mashirika haya ya kitume.
Kardinali Muller anasema, historia ya Kanisa inaonesha kwamba, vyama na mashirika haya ya kitume yanapaswa kusimamiwa kikamilifu na viongozi wa Kanisa na wakati mwingine yanahitaji kusafishwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ya Kanisa, ili viweze kutekeleza vyema wajibu na dhamana yake katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu mahalia wanapaswa kuonesha upendo wa dhati na kuvisaidia vyama na mashirika haya kuwa ni chachu ya utakatifu na upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa.
Vyama hivi visaidiwe kuingia kikamilifu katika sera na mipango ya Kanisa mahalia mintarafu shughuli za kichungaji, ili wanachama hawa waweze kuchangia kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Yote haya yanawezekana ikiwa kama viongozi wa Kanisa watakuwa karibu zaidi na wanachama wa Mashirika haya, ili kuwaongoza, kuwasaidia pale wanapoonekana kwenda kinyume cha: Sheria, Kanuni na Mapokeo ya Kanisa. Kumbe, utamaduni wa majadiliano ni muhimu sana, ili zawadi hii ya Roho Mtakatifu kwa Makanisa mahalia iweze kusaidia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu na kuendelea kulipyaisha Kanisa.
Kardinali Muller anakaza kusema, vyama na mashirika haya lazima yawe na utambulisho wake na karama zake, ili ziweze kuleta mafao kwa Kanisa zima. Viongozi wa Kanisa wawe na ujasiri wa kutoka katika ubinafsi, tayari kujenga madaraja ya majadiliano na vyama na mashirika haya, ili yaweze kuendeleza karama ya Unabii hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kanisa linafahamu, utajiri, changamoto na magumu yanayowakabili wanachama wa vyama na mashirika haya ya kitume, kumbe, wote hawa wanapaswa kusaidiwa ili waweze kutembea katika njia ya haki, umoja na mshikamano, kwa ajili ya ujenzi na upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa la Kristo!
Huu ndio utii unaofumbatwa katika majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wakati mwingine vyama na mashirika haya ya kitume ni changamoto na mwiba, ambao unasumbua, lakini ukweli wake wa kinabii unaweza kueleweka kadiri ya muda, historia na mazingira ya watu. Hapa viongozi wa Kanisa wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kutoka ili kujenga madaraja ya majadiliano.
Baba Mtakatifu Francisko anatoa vipaumbele na mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa, anapenda kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kulipyaisha Kanisa la Kristo kwa kukumbatia karama na zawadi mbali mbali zinazoendelea kuibuliwa ndani ya Kanisa. Hapa, viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa makini zaidi. Watakatifu katika historia ya maisha, waliweza kuunganisha kati ya mambo ya kale na mang’amuzi mapya ndaani ya Kanisa; wakawa waaminifu kwa utashi na maongozi ya Mungu katika maisha yao; wakajisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa Kristo na Kanisa lake.
Kardinali Muller anakaza kusema, wanachama wa vyama na mashirika ya kitume wanapaswa kupendwa na kusindikizwa katika maisha na utume wao, ili waendelee kujisadaka na kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani zao na utakatifu wa walimwengu. Watambue pale wanapoteleza na kuanguka, wawe tayari kurekebishwa na kufundwa katika wema na ukweli; kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa linaloitwa na kutumwa kuhudumia kwa njia ya viongozi wa Kanisa na kati ya waamini wa kawaida, bila mtu kutengwa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni