0
Taarifa ya 13 juu ya uhuru wa kuabudu duniani imetolewa Jumatano tarehe 16 Novemba 2016, ikiwa na lengo la kutetea jumuiya za kikristu zinazoteseka sababu ya imani. Alessandro Monteduro, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya makanisa hitaji, akitoa utangulizi wa taarifa hiyo amesema, Korea ya Kaskazini ni mahali ambapo kuna hali mbaya zaidi kuhusiana na uhuru wa kuabudu, sababu hakuna kikundi chochote cha kidini kinachoruhusiwa kuishi na kuishuhudia imani yake.
Kati ya mataifa 192 yaliyofanyiwa uchunguzi na taarifa hiyo, 38 ni yale yaliyo katika hali ngumu zaidi, na kati ya hayo, kwenye mataifa 23 kuna mateso makali, 12 mateso kutoka katika serikali zao, na 11 kutoka kwa makundi ya kijeshi ya waasi, na 15 yapo katika hali ya manyanyaso na unyanyapaaji. Mataifa saba ni yale ambayo yapo katika hatari ya kunyimwa uhuru wa kuabudu, nayo ni Saudi Arabia, Iraq, Siria, Afghanistan, Somalia, Nigeria ya kaskazini na Korea ya kaskazini. Taarifa inalenga kurudisha matumaini kwa wanaoteswa, kupitia miradi ya Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya makanisa hitaji.
Kardinali Mauro Piacenza, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji amesema: uhuru wa kuabudu unapaswa kulindwa na kila utawala wa sheria, kwa namna ya pekee, mataifa ya kidemokrasia, na uhuru huo uonekane wazi hadharani.
Askofu Jacques Behnan Hindo, wa Madhehebu ya kikatoliki-siria, katika Hassake-nisibi, katoa ushuhuda kwamba, Sharia ya kiislamu inanyima uhuru wa dhamiri, na hivyo Siria hakuna uhuru wa kuabudu kwa wakristu, na hiyo ni kwa sababu, nchi ya Siria ni nchi iliyovamiwa, na uislam nchini humo ni siasa. Wadaeshi hawapingi wakristu peke yao, wanapinga yeyote asiye mdaeshi.
Katika taarifa hiyo, wamekumbukwa wanawake wawili ishara ya matumaini ya uhuru wa kuabudu: Asia Bibi, mpakistani aliyechini ya ulinzi mpaka sasa, na Ishrat Akhond, mbangladeshi aliyeuwawa katika shambulio la Dacca hivi karibuni.
Na Padre Celestine Nyanda

Chapisha Maoni

 
Top