Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Kardinali Santos Abril y Castellò, mhudumu mkuu na msimamizi wa kitume wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu lililoko mjini Roma. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Kardinali Stanislaw Rylko, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Walei kuwa mhudumu mkuu na msimamizi wa
kitume wa Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu.
Itakumbukwa kwamba Kardinali Rylko alizaliwa tarehe 4 Julai 1945 huko BielskoZywiec, Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja ya Upadre tarehe 30 Machi 1969. Baadaye alijiendeleza katika masomo ya juu Jimbo kuu la Cracovia kati ya mwaka 1971- 1972 na baadaye kutumwa kusoma katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kati ya Mwaka 1972- 1978 na hapo akajipatia shahada ya uzamivu katika masuala ya Sayansi Jamii.
Kati ya Mwaka 1978 - 1987 aliteuliwa kuwa Gombera msaidizi sanjari na kuwa ni Jaalimu wa Sayansi Jamii kwenye Seminari kuu ya Jimbo kuu la Cracovia. Mwaka 1979 akateuliwa kuwa Katibu wa Tume ya Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Poland. Kunako mwaka 1987, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kiongozi mkuu Idara ya Vijana, Baraza la Kipapa la Walei na kupewa dhamana ya kuandaa maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani.
Tarehe 20 Desemba 1995, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Walei na kumpandisha hadhi ya kuwa ni Askofu na hatimaye, kuwekwa wakfu hapo tarehe 6 Januari 1996. Tarehe 4 Oktoba 2003 akateuliwa kuwa Askofu mkuu na Rais wa Baraza la Kipapa la Walei. Tarehe 24 Novemba 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Kardinali. Kwa miaka yote hii, ameendelea kuwa ni Rais wa Baraza la Kipapa la Walei, hadi pale Baba Mtakatifu Francisko alipoamua kufanya mageuzi makubwa katika muundo wa Baraza hili kwa kulivunja na hatimaye, kuunda Baraza la Kipapa la walei, Familia na Maisha.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni