Jamani la mgambo limelia!“Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi” ndiyo maneno yanayofungua Injili ya leo. Kutoka hapo tungetegemea kusikia huko kuzaliwa kulivyokuwa kama anavyoeleza mwinjili Luka kwamba Yosefu na Maria wanaenda Betlehemu, halafu kuna kutafuta pango, kuna kuzaliwa kwa Yesu na kutembelewa na wachungaji nk. Mwinjili Mateo anachukua mwelekeo mwingine kabisa. Ili kuweza kumwelewa Mathayo hatuna budi kuelewa fukuto la kidini na kisiasa lilivyokuwa kwa wakati huo, yaani ilikuwa ni patashika nguo kuchanika! Wakati ule Wayahudi walikuwa wanasubiri ujio wa Masiha. Matumaini hayo yalipata nguvu hasa walipokuwa katika mazingira magumu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Katika kipindi hicho Wayahudi waliomba Mungu aingilie kati kufanya mabadiliko ya maisha. Kusubiri huko kulianza na nabii Natani aliyetabiri mbele ya Daudi kwamba “Ufalme wako utadumu daima na katika kiti cha enzi cha Yerusalemu, daima kutakuwa na mrithi wako.” Karne zilizofuata Manabii wengine kama Isaya, Yeremia, Ezekieli, wakaendeleza matumaini hayo kwamba, siku moja ufalme huo utatangaa ulimwengu mzima na utadumu milele. Matumaini hayo yalipata nguvu zaidi karne mbili kabla ya Kristo na kuendelea hadi karne ya kwanza baada ya Kristo mwenyewe kuzaliwa. Lakini Masiha huyo alitofautiana kutegemea na wakati na mazingira ya vikundi vilivyotapakaa huko Israeli.
Mfano, Wasadukayo walimsubiri Masiha atakayeshika utaratibu kwa sababu wao ndiyo waliokuwa wanatoa amri. Mafarisayo walimsubiri Masiha atakayefuatilia kwa ushikaji wa dhati wa Tora. Waeseni walisubiri Masiha atakayeongoza mapambano kati ya waana wa giza na waana wa mwanga. Wazeloti, walisubiri Masiha atakayewaondoa Warumi kwa kuwashikisha adabu kwa njia ya mkong’oto wa nguvu! Yaani kila kundi, lilikuwa na wazo na mbinu ya kutekeleza sera na mikakati yake.
Kumbe, mtu ambaye hakutimiza vigezo vya kimasiha kadiri ya mategemeo ya watu hawa wote ni Yesu wa Nazareti. Kwanza kwa vile alikuwa Mgalilea toka Nazareti “kitu chema kinaweza kutoka Nazareti” kwani Wagalilea walikuwa watu wa kuja, nusu wapagani na wengine ni ukoo na Wasamaria. Mbaya zaidi Yesu hakuwa na midadi ya kisiasa, kwani alishindwa kujitetea hadi akaishia pabaya, yaani atateswa, akafa na kuzikwa, lakini siku ya tatu akafufuka kutoka kwa wafu! Leo Mathayo anataka kututhibitishia kuwa: “Huyu ndiye Masiha ajaye,aliyeanzisha uliwengu mpya na msimsubiri mwingine zaidi ya huyu.” Kwa maneno mengine hapa matumaini ya watu yamegota mwamba, na Nahodha ametia nanga!
Toka hapa Mathayo anachukua mwelekeo mwingine wa masimulizi: “Mariamu mama yake, alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla ya kuanza kuishi pamoja kama mume na mke, akagundulika ana uja uzito kwa uweza wa Roho mtakatifu.” Kwa Kiebrania roho anaitwa Ruah jina hili liko katika jinsia ya kike (feminine gender). Kwa hiyo hapa uwezo wa Roho maana yake ni nguvu za mpulizio wa uumbaji wa kimungu, siyo nguvu za kiume za kibinadamu. Hebu tuone hatua za kufunga ndoa katika Uyahudi. Hatua ya kwanza ni uchumba walioita erusin na halafu ya pili ni ndoa yenyewe Nissuin. Sherehe za uchumba ziliitwa kidushimu. Sherehe za uchumba zilikuwa ni za kuwekeana mkataba Ketubah kati ya wachumba mbele ya wazazi na wasimamizi wa ndoa.
Mkataba ulifikiwa baada ya majadiliano ya takribani siku mbili tatu hivi. Baada ya makubaliano likajengwa hupa, yaani hema, alama ya nyumba ya kuishi wachumba. Halafu mkataba ulitiwa na wachumba ndani ya ile hupa. Baada ya kutiliana mkataba mwanamume alichukua tallit kitambaa walichojifunika wakati wa sala, na kufunika kichwa cha mchumba wake na kumwambia: “Tangu leo wewe ni mke wangu” na mchumba wake alijibu “wewe ni mume wangu.” Kutoka hapo walijulikana rasmi kuwa ni wanandoa, lakini walirudi kila mmoja kuishi nyumbani kwa wazazi wake kwa muda wa takriban mwaka mmoja.
Katika kipindi hicho familia zilipata fursa ya kufahamihana zaidi, aidha kilikuwa kipindi cha kusubirisha wakue kwani mara nyingi walichumbiana wakiwa wadogo msichana miaka kumi na mbili au kumi na tatu, na mvulana miaka kumi na tano au kumi na sita. Ukweli mwingine ni kwamba Yosefu na Maria walishakubaliana kufunga ndoa na kuzaa watoto kadiri ya mila na desturi za Kiyahudi. Kumbe katika kipindi hiki cha kusubiri ndipo mambo yakawa kama yalivyokuwa kwa Maria. Kama ndivyo hivyo, basi fundisho la Injili ya leo tutalipata sehemu inayofuata.
“Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.” Neno kumwacha kwa Kigiriki ni apulusai maana yake kumwacha huru. Kwa vyovyote Yusufu alishtushwa na uja uzito ule, hakujua afanye nini. Hapa tusielewe kwamba Yusufu labda alimdhania mchumba wake amekosa uaminifu na hivi akaona afadhali amwache kwa siri. La hasha, kwa sababu kila mmoja alijua Maria ni mke wa Yosefu na baada ya kujifungua siri ingekuwa njenje tu. Aidha ni dhahiri kwamba Maria mwenyewe “alishamtonya” Yusufu hali halisi ya mambo, vinginevyo wambeya wangepata agenda, kwani wengine wanadhani eti umbeya ni mtaji, kama ni kweli wengi wangekwishatajirika sana.
Lakini, kwa vile Yusufu alikuwa mtu wa haki hakutaka kuonesha kadamnasi na kujenga sintofahamu ya watu juu ya kile kilichomtokea Maria, akaamua kumwacha huru na kusubiri kitakachotokea. Kwa Waisraeli sifa hii ya haki ilimaanisha mshika sheria ya Tora kwa dhati yote. Lakini kidhati, Yusufu hakuwa na sifa ya haki, kwa sababu Tora ilimdai Bwana arusi amtangaze kadamnasi mke wake asiyekuwa mwaminifu. Hivi haki inayosemwa hapa siyo ile ya kufuata Tora neno kwa neno. Yusufu anaongozwa na haki inayofumbatwa katika upendo. Hiyo ni haki mpya inayokufanya upokee na kufuata matukio unayoletewa na Mungu hata kama ni magumu na hayaeleweki.
Kama Yesu alihubiri na kufuata haki ya Tora lakini kadiri ya mwanga wa upendo kwani binadamu ni juu zaidi ya Tora. Aidha,“Malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema Yusufu, mwana wa Daudi.” Tunakosea tunapomwita Yusufu kuwa ni baba mlishi wa Yesu kwani Yusufu alikuwa baba halisi wa Yesu. Kwani hata wanakijiji walithibitisha waliposema: “Huyu siyo yule mwana wa Yusufu?” yaani waliona jinsi Yesu alivyofanana na Yusufu. Kadiri ya Waisraeli baba siyo tu mzazi wa kimwili kwani “kuzaa mwana si kazi, kazi kulea.” Kazi ya wazazi ni kumlea na kumpa mtoto thamani za kiutu. Hatimaye mtoto anafanana na thamani za maisha ya baba, yaani upendo, kuthamini na kujali wengine. Hivi Yesu aliishi na kukua kadiri ya siha (picha) ya kibinadamu aliyojifunza kwa Yusufu. Mungu alimchagua Yusufu amlelee mwana wake aweze kuakisi uso wa kweli wa Baba wa mbinguni. Yusufu peke yake aliweza kumlea na kumwingizia Yesu thamani zile ambazo zingeweza kuonesha ni ipi sura halisi ya Baba wa mbinguni. Kwa hiyo binadamu waliochukua haki mpya ya upendo na siyo ile ya Tora ni Maria na Yusufu.
“Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto.” Mara nyingi Mungu anapoingia katika makubaliano na mkataba na binadamu hutumika lugha ya “malaika wa Bwana.” Maana yake ni ufunuo aliopata Yusufu kutoka kwa Mungu. Halafu kuhusu ndoto. Waisraeli walipotafuta kutatua matatizo yanayowasibu walienda kujiuliza kwa mganga na kazi yake mojawapo ni kutafsiri ndoto. Mfano ndoto ya Salomoni kule Gabaoni ambayo anasikia Mungu akimwuliza amwombe chochote anachotaka, naye akaomba hekima. Baadaye, Waisraeli wakaacha kufuata ndoto na kuwafuata manabii kuwa watu pekee wanaowasilisha Neno la Mungu na siyo ndoto.
Katika Agano jipya suala la ndoto linatokea mara sita tu katika Injili ya Mathayo. Hapa inaletwa kuonesha kwamba kulikuwa na ufunuo wa Mungu. Hivi Yusufu akapata ufunuo huu: “Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Maria mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.” Hofu ya Yusufu ni ile ya yule aliye mbele ya mazingira na anataka kufuata mapenzi na mwanga wa Bwana. Hofu hii katika Biblia haimaanishi woga, bali ni uchaji ya kutaka kufuata kile ambacho Bwana anakielekeza. Ni safari anayotakiwa kuifuata.
“Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” Hilo ndilo jina analolipewa Yesu kutoka mbinguni. Yusufu anakuwa wa kwanza kumwita jina anaambiwa: “utamwita jina lake Yesu” kuwa ni Mungu anayekomboa. Jina la Yesu lilikuwa la kawaida na wengi walilitumia, asili yake ni Yoshua kutoka Kiebrania Iyasha maana yake kuokoa. Yoshua ndiye aliyewaongoza watu hadi Kanaani. Lakini hawakumhusianisha na ukombozi. Kumbe, ni wakristo peke yao waliokokotoa msamiati huu wa ukombozi na kuhusianisha na Yesu. Ukombozi huo ni dhidi ya maadui hasa dhambi na mauti mambo yanayotuzuia kuishi kadiri ya utu wetu.
Katika hatima tunaambiwa: “Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa Nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jina lake Imanueli; yaani Mungu pamoja nasi.” Unabii huu umechukuliwa kutoka Isaya. Huyu alitangaza mwana atakayezaliwa kutoka kwa Bikira, akimaanisha mke wa mfalme. Kumbe, unabii huu unatimia kwa Bikira Maria, naye siyo tu bikira alipompata Yesu, bali huonesha pia upendo wake kamili kwa Mungu. Kama Yusufu atamwita jina Yesu, hapa unaona watu wengine wote wanamwita Emanueli, “nao watamwita jina lake Imanueli” yaani Mungu nasi. Amefafa nasi katika kila kitu isipokuwa dhambi.
Hapo “Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.” Kisha bila maneno anafanya kama Abrahamu baada ya kuagizwa anachotakiwa kufanya akamchukua mkewe. Yusufu ni wa kwanza kutamka jina hili Yesu kwani ndiye atakayefunua uso wa huruma na upendo wa Mungu anayeokoa kwa vile ni upendo na ni upendo tu hakuna kingine zaidi! Ninakutakia maandalizi mema ya kumpokea Yesu, yaani Mungu anayekomboa katika maisha yako!
Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni