Mwenyezi Mungu alitoa maagizo ya namna ya kufunga kupitia kwa nabii isaya akisema hivi
"Walakini wanitafuta kila siku, hupenda kujua njia zangu ; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao. Hutaka kwangu sheria za haki, humkaribia Mungu. Husema, mbona tumefunga lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu lakini huangalii? Fahamuni siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je, kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je, ni siku ya mtu kujitabisha nafsi yake? je ni kuinamisha kichwa kama unyasi na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? je utasema ni siku ya kufunga na ya kukubaliwa na BWANA? Je, saumu niliyoichagua sio ya namna hii? Kufunguo vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaachia huru walio onewa, na kwamba mvunje kila nira? Je, sio kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? umwonapo mtu aliye uchi umvike nguo, wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapo pambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia, utukufu wa BWANA (Mungu) utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita na BWANA ataitika, utalia nae atasema mimi hapa..." (Isaya 58: 2-9).
Aidha, watu walikuwa wakitumia kipindi cha kufunga kuuonesha umma jinsi walivyo wacha Mungu na hivyo kupewa heshima mtaani. Mtu asiyefunga alionekana mjinga, mtenda dhambi na asiyefaa katika jamii. Kufunga ilikuwa sehemu ya maisha na si suala la uhusiano binafsi kati ya mtu na Mungu).
Kwa vile Mwenyezi Mungu wetu ni wa upendo na huruma, alimtuma nabii isaya kuwaambia watu hao kuachana na funga hiyo isiyo na maana na badala yake kuelekeza nguvu zao katika mambo muhimu ambayo Mungu anaangalia katika kutathimini utu wa mtu. Mambo hayo ni upendo, huruma na kujitoa kama ilivyoelezwa hapo juu na kuachana uovu wa aina zote.. Kwa msingi huo, mtu mwenye upendo na anaejitoa kusaidia wengine ana thamani kubwa mbele za Mungu kuliko mtu anaeshinda njaa siku 300 za mwaka pasipo kuonesha upendo wa kweli kwa wengine.
Yesu kristo alipokuja ulimwenguni, alisisitiza maneno ya nabii Isaya kwa kutaka watu waache tabia ya funga za kujionesha kwa watu, na badala yake wajitahidi kumpendeza Mugu. Yesu alisema"Tena mfungapo msiwe kama wanafiki wenye nyuso za kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amini nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na baba yako (Mungu) aliye sirini; na baba yako aonae sirini atakujazi" (Mathayo 6:16)
Kumbe tabia ya kujionesha mbele za watu kwamba tumefunga inamuudhi Mungu na kutufanya tukose thawabu. Mtu anaejionesha au kujisifu kwamba anafunga huambulia kusifiwa na watu wa kidunia ambao wanadhani mtu huyo ni mtakatifu sana, lakini kwa mujibu wa maandiko matakatifu mtu huyo anajisumbua na kupoteza muda wake bure kwani hakuna thawabu anayo pata kwa Mwenyezi Mungu.
Tumuombe Mungu sana atuongoze na kutusaidia katika kipindi hiki cha Kwaresma na baada ya hapo.Ni wajibu wetu kujitahidi kuachana na maovu yote, kufanya toba ya kweli na kumpokea Yesu katika mioyo yetu badala ya kumuabudu kwa midomo tu. Tunapaswa kukumbuka kuwa Mungu wetu ni yule yule kabla, wakati na baada ya kipindi cha Kwaresma na hivyo kipindi hiki kiwe kipindi cha kutukumbusha na kutuandaa kwa ajili ya wakati mrefu ujao baada ya Kwaresma.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni