Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujisadaka zaidi kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwajengea uwezo na kuwapatia matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hivi ndivyo anavyoandika kwenye ujumbe ambao amewatumia wajumbe wa Shirikisho la Vyama vya Upendo Kimataifa, “Association International des Charitès” (AIC), lililoanzishwa na Mtakatifu Vincent wa Paulo, mwaka 2017 wanapoadhimisha Jubilei ya miaka 400 tangu lilipoanzishwa.
Baba Mtakatifu anapenda kuungana na wajumbe hawa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa wanayotenda kama ushuhuda wa huruma ya Mungu miongoni mwa maskini. Maadhimisho haya iwe ni nafasi ya kushukuru, kutafakari na hatimaye, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu kujiwekea sera na mikakati endelevu ya huduma ya upendo. Shirikisho hili ni matunda ya wema na huruma unaobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa Mtakatifu Vincent wa Paulo aliyejisadaka kwa ajili ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.
Kwa njia hii, Mtakatifu Vincenti wa Paulo alitaka kuutafakari wema na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu, kwani kwake maskini walikuwa kama wawakilishi wa Yesu na sehemu ya Fumbo la mwili wake, yaani Kanisa. Alitambua kwamba, maskini ni amana na utajiri mkubwa wa Kanisa hata wao pia wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa kwa kulisaidia kumwongokea Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Vincent wa Paulo alipenda kushirikiana kwa karibu sana na waamini walei ndiyo maana Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Upendo linataka kujizatiti zaidi katika mchakato wa kuwajengea uwezo wanawake kwa kuwaondolea umaskini na mahangaiko ya: kiroho, kimwili, kimaadili na kiutu!
Mambo yote haya anasema Baba Mtakatifu Francisko ni sehemu ya utashi wa Mungu kwa mwanadamu, yaani ni upendo unaopaswa kumwilishwa katika maisha ya binadamu, ili kumletea maendeleo endelevu: kiroho na kimwili. Kipaumbele cha kwanza wawe ni wanawake pamoja na watoto wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia. Maisha yanayofumbatwa katika imani kwa Kristo na Kanisa lake, yanawasaidia waamini kutambua uhalisia wa maisha, utu na heshima ya binadamu; matatizo na changamoto anazokabiliana nazo: kijamii, kisiasa na kiuchumi na kumthamini kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Waamini wanakumbushwa kwamba, wanawajibika kuwasaidia na kuwahudumia jirani zao, changamoto inayobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho! Hapa, Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai aliyejinyenyekesha katika mambo yote na kuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi. Aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili aweze kuwainua maskini na wanyonge kutoka mavumbini, matendo makuu ya Mungu, mwaliko kwa Mama Kanisa kuyaendeleza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu. Ukombozi wa mwanadamu na maendeleo endelevu ni sehemu muhimu sana ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na kujizatiti katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, kiini cha wito na muungano wake na Mwenyezi Mungu. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa kwa Mama Kanisa kuwaendea walimwengu ili kuwapelekea wema, huruma na upole wa Mungu, changamoto kwa waamini kuendeleza mchakato huu anasema Baba Mtakatifu Francisko.
Uaminifu wa Kanisa unafumbatwa kwa namna ya pekee katika upendo wenye huruma unaowafunuliwa watu matumaini. Ni uaminifu unaofumbatwa katika ushuhuda wa mtu binafsi kwa kukutana na Kristo Yesu pamoja na kuwapatia maskini nafasi ya kumwona Kristo katika maisha yao. Kwa kukita mizizi ya maisha ya kiroho kwa Kristo Yesu, waamini wanaweza kusaidia mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa huruma unaopyaisha mioyo ya watu kutoka katika undani wao na kuwawezesha kuwa na mang’amuzi mapya!
Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake, anawataka wajumbe wa Shirikisho la Vyama vya Upendo Kimataifa, “Association International des Charitès” (AIC), kutafakari kwa kina karama ya Mtakatifu Luisa de Marilac ambaye Mtakatifu Vincent wa Paulo alimkabidhi dhamana ya kuratibu vyama vya upendo, ili kuwaonjesha huruma ya Mungu inayowainua wanyonge na kuwapatia ujasiri na matumaini thabiti. Wote hawa, Baba Mtakatifu anawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mtakatifu Vincent wa Paulo na ya Mtakatifu Luisa de Marilac.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni