Askofu Eusebius Nzigilwa; Padri Marandu hakujali maslahi yake binafsi
Akitoa homilia kwenye Misa hiyo Takatifu, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa amesema kuwa, Padri Gallus alikuwa ni mtumishi aliyejituma kwa kuhudumia watu pasipo kujali faida yake mwenyewe .
“Mimi binafsi niliridhishwa na utendaji wake wa kazi na maaskofu walizitambua kazi na jitihada zake. Ukiona mtu anafanya kazi mahali kwa muda mrefu pasipo kuhamishwa, ujue huyo ni mtaalamu na kazi zake zinafahamika sana. Hilo ni fundisho tosha kwa kila mwanajamii na waamini, kuiga na kulienzi katika maisha yao ya kila siku, kwani wengi wanafanya kazi kwa kutanguliza faida binafsi na si ya Mungu,” amesema Askofu Nzigilwa.
Amesema kuwa, Baraza la Maaskofu, linazitambua kazi za Marehemu Padri Marandu, na kwa kawaida kuna kikomo cha kufanya kazi hizo, hasa kwa watendaji wengi waonaohudumu kwa kipindi cha miaka 6 na kuhamishiwa mahali pengine, lakini Padri Marandu alidumu kwa miaka 15, hivyo ni wazi kuwa kazi zake zilithaminika na utendaji wake ni mzuri, ndio maana Maaskofu hawakuona kama kuna haja ya kumhamisha.
Ametoa mwaliko wa kuwajibika na kutenda kazi pasipo kuwa na vigugumizi, kwani wengi wanashindwa kutenda kazi vizuri kutokana na vigugumizi vyao, ambapo vinawakwamisha katika kazi nyingi za uinjilishaji, kwa kutojikabidhi kwa Kristo na kuwaasa waamini waishi kwa uzima katika kumtegemea Kristo na si nguvu zao wenyewe,” amesema Asofu Nzigilwa.
Askofu Nzigilwa, amewataka waamini na jamii kuendeleza yale yote ambayo Padri Marandu aliyafanya, hasa kuwaweka kuwa wamoja kwa kupitia dini zao japokuwa jambo hilo si la mchezo, wameona matunda yake.
Sote hapa tu mashuhuda katika hilo, kuwa marehemu alipambana katika kuleta ustawi kwa kutuunganisha na watu wa Dini nyingine, lakini kubwa tutambue alikuwa akituunganisha kwa kutuletea maendeleo ya roho na mwili na daima maendeleo popote hayana dini wala kabila,” amesisitiza Askofu Nzigilwa.
Adhimisho hilo lilihudhuriwa pia na viongozi wa Dini mbalimbali, Askofu Titus Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara na Mhashamu Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa, ambaye ndiye aliyekuwa mhubiri katika Misa hiyo Takatifu pia alikuwepo Naibu Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro.
Historia ya Utume wake
Mwaka 1994 mpaka 1998 alikuwa ni mmojawapo wa Walezi katika Novisieti ya Shirika iliyopo Magamba Lushoto. Wakati huohuo alikuwa Msarifu wa Novisieti.
Mwaka 1998 mpaka 2002 alifanya shughuli za Uchungaji katika kisiwa cha Pemba Jimbo Katoliki Zanzibar. Wakati huohuo tarehe 11/2/2001 aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mahusiano baina ya Dini Mbalimbali. Kati ya mwaka 2002 na 2005 alihamishiwa Bagamoyo katika Jimbo Katoliki Morogoro ambapo alikuwa Wakili Paroko na Mkurugenzi wa Hija na Makumbusho ya kikatoliki ya Bagamoyo.
Tarehe 8 Septemba mwaka 2005 aliongezewa majukumu ya kuwa Katibu wa Tume ya Wahamiaji na Wasafiri na kushughulikia mambo yanayotokana na shughuli za Tume ya Kipapa ya masuala ya Kiutamaduni na Urithi wa Kiutamaduni wa Kanisa.
Mwaka 2006 alihamishia makao yake kwenye Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mahusiano ya Dini Mbalimbali pia akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Utamaduni na Tume ya Wasafiri na Wahamiaji.
Mwaka 2013 mpaka 2016 alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Katibu Mtendaji wa Idara ya Uchungaji pamoja na kusimamia Tume ambazo alikuwa amekabidhiwa kabla.
Kati ya Aprili 2014 na Novemba 2014 alikaimu Ukatibu Mtendaji wa Idara ya CARITAS.
Kifo chake
Marehemu alipata tatizo la kuumwa takribani majuma mawili yaliyopita akiwa mjini Addis Ababa Ethiopia alipokwenda kuhudhuria semina ya uchungaji iliyoandaliwa na Umoja Wa Wanachama Mabaraza ya Maaskofu ya Afrika Mashariki na Kati AMECEA. Ingawa alipata matibabu akiwa huko, tatizo halikutatuliwa kikamilifu. Kwa hiyo aliporejea nchini aliendelea na vipimo mbalimbali na matibabu. Baada ya kutopata nafuu akapangiwa kulazwa Jumatatu ya tarehe 27 Machi asubuhi ili aweze kufanyiwa upasuaji.
Hata hivyo siku ya Jumapili tarehe 26 Machi 2017 mnamo saa 6 mchana hali ya marehemu ilibadilika ghafla. Ilibidi baadhi ya watumishi wa TEC kumkimbiza hospitali ya Temeke. Hata hivyo jitihada hizo hazikufanikiwa kwani marehemu alifariki dunia saa 6.30 mchana akiwa njiani kupelekwa hospitali. Baada ya kufikishwa hospitali madaktari walibaini kuwa Padri Gallus alikwishafariki mnamo saa 6 mchana akiwa njiani.
Marehemu anazikwa huko Usa River Seminari Jimbo Kuu Katoliki Arusha.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni