Wapendwa taifa la Mungu, wito na ujumbe tuupatao leo katika Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu ni kutafakari juu ya Fumbo na maana ya wito wa Mungu na hivyo kusali kwa ajili ya ongezeko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa, yaani: wito wa ndoa takatifu kiini cha miito yote; wito wa upadre na maisha ya kitawa!. Tunafurahi na kumshukuru Mungu kwamba anamwita na kumtuma mwanadamu kuutangaza ufalme wake. Tukisoma injili ya Yoh. 10:27 – Yesu anatamka wazi – mimi ni mchungaji mwema. Hakika kwa Waisraeli tamko kama hili liliwashtua sana kwani kadiri ya mafundisho na imani yao mchungaji wao ni mmoja tu naye ni Bwana Mungu na tunaona katika – Zab. 23,1 – Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Zaidi sana katika Yoh. 10:30 – anasema - Mimi na Baba tu umoja. Pia tamko kama hilo halikuwa la kawaida kwa watu wale na lilihitaji mtazamo mpya. Ni kama vile mtu afike hapa leo na aseme – tangu leo mahali hapa ni pangu – hali tukijua wazi kuwa ni mali ya parokia au nyumba ya malezi au ardhi ya fulani au chuo chetu n.k.
Ndugu zangu, katika KKK 01 – tunasoma kuwa ‘Mungu ametuumba ili tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake mbinguni’. Katika mpango wa ukombozi wa mwanadamu, Mungu alimpeleka Mwanae, tena kwa mamlaka, naye mwana anawapeleka wale aliowachagua, tena anawapeleka kwa mamlaka – Yoh. 20:21-23 – Basi Yesu akawaambia tena amani iwe kwenu, kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi, naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, pokeeni Roho Makatifu, wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa, na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.
Hii ni aina mpya kabisa ya maisha ya kiroho. Maisha mapya katika Kristo huanza na ubatizo. Mt. Thomas wa Aquino anasema – ubatizo unafuta doa au kosa la zamani na kufanywa wapya. Mfalme Mt. Lui IX, alibatizwa katika kanisa la Poisi huko Ufaransa. Alipopewa ufalme aliupokea katika kathedrali ya Rheims nchini Ufaransa. Mhuri wake wenye saini na aliotumia kuweka saini kwenye barua rasmi uliandikwa Louis wa Poisi. Alipoulizwa kwa nini anafanya hivyo alisema anafanya hivyo kwa sababu Poisi ndipo alipobatizwa na akaendelea kusema nikifa ufalme wangu unaishia hapa duniani lakini ubatizo wangu utanifikisha mbinguni.
Ndugu wapendwa, mwenyezi Mungu anampatia mwanadamu msamaha wa dhambi. Katika hali hii mtazamo wa kawaida wa kibinadamu juu ya mapenzi ya Mungu kwetu hautoshi. Ni kama vile wawili wanaogombana na ghafla mmoja anasema haya basi nakusamehe. Pengine mmoja anasema hivyo ili yaishe tu kwa nje ila moyoni bado uchungu unabaki. Katika mtazamo huu mpya tunaona kuwa Mungu anatuma na anatoa zana za kazi. Kwanza tunaona kuwa Yesu anachukua hatua za kuita wale aliowachagua – Yoh. 15,16 – si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi, nami nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kukaa, ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awaapeni – na zaidi sana akaweza kusema awapokeaye ninyi, anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma - Mt. 10:40. Na katika Mt. 28,18 – tunasoma kuwa, Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.... na katika Yoh. 10:11 tunaambiwa kuwa mchungaji mwema ni yule atoaye uhai wake kwa ajili ya kundi. Hili ndilo fumbo la wito wa Mungu.
Ndiyo maana tunaposali leo kwa ajili ya miito tunasali pia ili tuweze kuelewa vizuri maana ya wito wa Mungu ili tuweze kutofautisha wito wa Mungu na wito toka kwa mwanadamu. Neema ya Mungu husikilika na kupokeleka tukitoa nafasi na muda kutafakari juu ya mapenzi yake kwetu. Katika Rum. 10:17 twaambiwa kuwa imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo. Huu ufahamu ndio uliomsukuma Paulo na wengine kwenda kwa mataifa, Yohani kushuhudia na sisi tulioko hapa leo kuendelea kuamini na kusadiki juu ya upendo huo wa Mungu.
Dr. David livingstone alikuwa mmisionari, tabibu na mvumbuzi hodari. Stanley alimpata baada ya kumtafuta kwa muda mrefu. Akampata Ujiji Kigoma. Baada ya kukaa naye kwa muda wa kutosha Stanley aliomba abatizwe na kuwa mkristo. Stanley anashuhudia kuwa namna Livingstone alivyohudumia wale watu aliokaa pamoja nao na kuwatibu magonjwa yao ilitosha kugusa maisha yake. Yote aliyoyaona na kushiriki ilikuwa ni katekisimu iliyokamilika. Hapa tunaona jinsi mwanadamu anavyoweza kuishi na kushuhudia hili fumbo la wito.
Somo la kwanza linatusaidia pia kutafakari sana wito wa leo. Kanisa la kwanza linaishi huo ushuhuda – wanatangaza na kuteseka. Mtume Petro na wale kumi na mmoja wanamshuhudia Kristo mfufuka. Wametambua upendo wa Mungu na wanautangaza. Ili kuitangaza Pasaka hatuna budi kuutangaza na kuishi ushindi wa Kristo Mfufuka. Kuishi maisha ya furaha na utukufu. Katika somo la pili, Mtume Petro anasema wazi, tutende mema na kuvumilia mateso tukiiga mfano wake. Wafuasi wanaalikwa kuishi hilo pendo la Mungu. Watashinda wakiishi maisha kama ya Kristo Mfufuka. Katika waraka wa 1Kor. 9:22, mtume Paulo anasema kwa wanyonge nilikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Huu ndio wito anaotuita Mungu ili tumfuate. Huu ndio ushuhuda wa hilo fumbo la wito.
Ndugu zangu, wito wa Mungu si kitu ambacho kinaenda kwa mpangilio maalumu kadiri ya uelewa wa kibinadamu. Tutafakarishwe na wito wa Elisha. Nabii Eliya anapita na anamtupia Elisha vazi lake la kinabii ikimaanisha wito wake kumtumikia Mungu. Elisha alikuwa katika shughuli zake. Hakutegemea kuitwa namna hiyo katika maisha yake. Kwa kupakwa mafuta, anakuwa mfuasi wa Eliya na mrithi wake. Na tangu siku hiyo maisha yake yanachukua mtindo mwingine kabisa. Mipango na harakati zake zote zinachukua mkondo mpya. Anaingia rasmi katika mpango wa wito wa Mungu. Anamtumikia Mungu.
Mwinjili Luka kuanzia sura ya 9 na kuendelea anaoonesha mwenendo mzima wa maisha ya wito wa Yesu – kwamba ni maisha endelevu kwenda Yerusalemu, ambapo atapata mateso, kifo lakini pia ufufuko. Akiwa safarini anawafundisha wafuasi wake. Kwa ustadi mkubwa anawaita wafuasi wake na anawataka kuwa makini na wavumilivu. Pia anawakumbusha juu ya nguvu ya maamuzi – au kumfuata yeye au kumkataa. Anawaalika kuwa waangalifu na nguvu au vifungo binafsi, familia na hali yo yote ile inayoweza kuzuia kumfuata. Anaonesha wazi kuwa ufalme wa Mungu una thamani kubwa zaidi kuliko hali zetu, chaguzi zetu na yote tuliyonayo au tutamaniyo kufanya.
Swali la kawaida kabisa la kibinadamu linalofuata ni hili – je yawezekana kumfuata Bwana? Mtume Paulo katika Gal. 5:1,13-18 anasema ni roho ya Kristo inayotuita tuwe huru na inayotuwezesha kutoa jibu katika huo ufuasi. Wito wa ufuasi hautegemei kusikia sauti ya roho zetu bali twaitwa kusikiliza sauti ya roho yake Kristo. Wakati mwingine ili kuwapata kondoo hatuna budi kuvaa ngozi ya kondoo. Mungu si mwanadamu, lakini alijifanya mtu ili apate kutukomboa. Kila aisikiaye sauti ya Mungu na kumwamini na kumsadiki anaalikwa kulichunga neno hilo la Mungu. Sote tunaalikwa kusali ili wapatikane wengi wanaojitoa kueneza ufalme wa Mungu na kuwaombea na kuwatunza wale wote waliojitoa kueneza habari njema kwa sala, maneno na matendo.
Tumsifu Yesu Kristo.
Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni