ASKOFU wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evarist Chengula amewapongeza wajubilanti 6 kwa kutimiza miaka 25 ya nadhiri ya utawa huku akibainisha kwamba hiyo siyo kazi rahisi kwa mapenzi yao bali wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuendelea kumuomba awasaidie ili wazidi kusonga mbele kwa kushirikiana katika mashirika yao
.
.
Askofu Chengula ameyasema hayo wakati wa Homilia ya adhimisho la misa takatifu ya miaka 25 ya utawa na kuweka nadhiri za daima kwa masista sita wa Shirika la Bikira Maria Malkia wa Mitume wa Mbeya iliyofanyika katika Kanisa Kuu la kiaskofu la Mtakatifu Anthony wa Padua Parokia ya Mbeya Mjini.
Wajubilanti hao walioadhimisha miaka 25 ya utawa na kula kiapo cha nadhiri za daima ni Sr.Astrida Katimbuka, Sr.Asteria Nyamwela, Sr.Victoria Aswile, Sr.Yosepha Ayobangila, Sr.Adelphina Kipangula na Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Jimbo Katoliki Mbeya, Sr,Joyce Nchalla wote wa Shirika la Bikira Maria Malkia wa Mitume wa Mbeya
.
Amesema kutimiza miaka 25 ya utawa kwa kuachana na kila kitu katika ulimwengu na kuamua kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuwaletea watu neema ya kiroho na kimwili si kazi ndogo, hivyo amewapongeza na kuwaalika kuendelea kumtegemea na kumuomba Mama Maria kama alivyofanya kwa Elizabeth awaongoze katika kuendelea kuwatendea mema wengine.
Amesema nguvu zao hazingetosha kufikia miaka 25 hiyo bali ni kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, lakini kadri miaka inavyozidi kusonga mbele kuna hatari ya baadhi ya watawa kuwa na roho ya mgando ya uvuguvugu, hivyo amewakumbusha kuwa duniani ni mahali pa kutafuta ukamilifu.
“Mmetembea na kufanya kazi hiyo kwa miaka 25 kwa kutembea na Mwenyezi Mungu, hivyo muamshe nguvu hiyo ndani ya mioyo yenu, ninyi mnayaona kama mambo ya kawaida lakini muelewe hayo mambo hayazoeleki wala si ya kawaida kwani sisi tulio nje tunayaona siyo ya kawaida, kumbuka wazazi wenu, ndugu, jamaa na marafiki wameacha kazi zao wamekuja kuwashuhudia kuwasikia na mnavyojivunia kwamba mtaendelea tena kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu katika maisha hayo,”
“Nawatakia ujumbe mwema wa Mama Maria daima kuona mnawajibika kuwaletea watu neema na popote mtakapokuwa lazima iwe sababu ya majirani kupata neema, neema ya kutambua uwezo wake Mwenyezi Mungu kama Mama Maria alivyofanya kwa Elizabeth.”
Askofu Chengula amewaasa watawa kuwa sehemu ya faraja kwa maisha ya wenzao watakao kumbana na magumu akibainisha kuwa ikitokea basi wasimuache mwenzao anahangaika ili asijisikie mpweke akakata tamaa lakini kama watamfuata Mama Maria itakuwa ni rahisi kwao kwenda kuzungumza na mwenzao aliyepo kwenye matatizo na siyo ya kimali au kimwili bali ni katika mambo ya kiroho.
“Sote tunajuwa kuwa watawa wameingia utawani kwa ajili ya kuwa wakamilifu kama Mungu Baba na tukiona ndugu yetu hafuati mfumo huo, huo ni umaskini lazima kwenda kumsaidia na kumsalimia siyo lazima kumpigia kelele, ila Roho wa Bwana anayekuwa ndani yetu ndiye atakayemsukuma, atakayemfanya atambue kwamba yeye ameingia katika Shirika kwa ajili ya kujikamilisha, wengine wanasema kujitakatifuza, kukamilisha utakatifu,”amesisitiza.
Amewaalika kuwa kielelezo cha upendo katika utume huo kwa kutembeleana na kuwasihi endapo itatokea mwenzao katika hali ya kibinadamu hataki kukutana na Roho Mtakatifu, kwa kuwakwepa wajue kuwa anakumbana na nguvu ya kiza, wasimtenge bali wawe naye kwa njia ya kumuombea na kuzungumza naye daima.
Aidha Askofu Chengula amesema watawa wanaoadhimisha nadhiri ya miaka 25 waepuke kufanya utume kwa mapenzi yao na kupitia siku hiyo inawakumbusha wengine kuacha mapenzi yao na kutakiwa kufuata mapenzi ya Shirika ambalo linaongozwa na Kanisa.
“Chagueni viongozi kwa manufaa ya shirika na mjue kuwa mbele yenu pamoja na Mama Maria ni kazi moja kuwachagua watu watakaowasimamia muwe wakamilifu siyo kufanya katika mapenzi yetu, na siyo kuchagua watu wa mkoa gani, au vijana, hapana tufurahi, tuwe watu wa kushukiwa na roho,”Amefafanua.
Amebainisha kuwa viongozi watakaokuwa wanawachagua wajue kuwa wameshukiwa na Roho Mtakatifu ili awasaidie, huku akiendelea kuwasisitiza kuzingatia na kuziishi kanuni za Kanisa na Shirika lao katika muongozo wa pamoja hasa katika kukazia juu ya kusali.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni