Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi tarehe 24 Agosti 2017 amehitimisha ziara ya kikazi nchini Russia ambako alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Kanisa la Kiorthodox kwa kukazia umuhimu wa uekumene wa sala, maisha ya kiroho, ushuhuda wa damu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Amekutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Russia . Hapa wamekazia umuhimu wa kuheshimiana; kusikilizana kwa dhati na kushirikiana ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuikabili Jumuiya ya Kimataifa.
Kardinali Pietro Parolin, kabla ya kuondoka Moscow na kurejea tena mjini Vatican, Alhamisi asubuhi, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Ubalozi wa Vatican nchini Russia. Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari vya Italia, Kardinali Parolin amefafanua kwa kina na mapana maudhui yaliyofumbatwa katika mazungumzo yake na viongozi wa Kanisa na Serikali ya Russia na kwamba, kuna mwelekeo chanya zaidi na wenye matumaini kwa siku za usoni. Imekuwa ni nafasi ya kujadiliana, kusikilizana, ili kufahamu mwelekeo wa kila upande, tayari kuwajibika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!
Kardinali Parolin amezungumzia kuhusu changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni lile wazo la kutaka nyumba za Ibada zilizotaifishwa na Serikali ya Russia kurejeshwa tena mikononi mwa Kanisa Katoliki, ili Kanisa liweze kutoa huduma za kichungaji kwa waamini wake. Hii ni tema ambayo imepewa uzito wa juu kabisa wakati wa mazungumzo yake na viongozi mbali mbali nchini Russia. Ni matumaini ya Kardinali Parolin kwamba, sasa utafutia utekelezaji wa yale mambo msingi yaliyofikiwa kwa ajili ya: maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Hii inatokana na ukweli kwamba, waamini wa Kanisa Katoliki nchini Russia hawana nyumba ya Ibada, hali inayochangia kufifisha uhuru wa kidini. Uwepo wa Makanisa kwa waamini wa Kanisa Katoliki ni jambo jema katika mchakato wa kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu!
Kardinali Parolin, akifafanua kuhusu changamoto za ukosefu wa haki, amani, ulinzi na usalama anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi badala ya “kutunishiana misuri” kwa vitisho vya mashambulizi ya silaha. Vita, ghasia, chuki na mipasuko ya kijamii imezagaa sehemu mbali mbali za dunia utadhani ni “ukungu wa asubuhi”. Kumbe, changamoto ya amani ya kudumu duniani inapaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa, kwani amani ni jina jipya la maendeleo endelevu. Vita ina madhara makubwa na yanayochukua muda mrefu kuweza kugangwa na kuponywa kabisa.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anakaza kusema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete: kulinda, kudumisha na kuendeleza mchakato wa amani na haki kwa kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu. Viongozi wa Serikali ya Russia wanafahamu fika msimamo wa Vatican kuhusu vita na machafuko ya kisiasa nchini Ukraine. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushirikiana na kushikamana katika mchakato wa kusitisha vita nchini Ukraine, ili amani na usalama viweze kutawala tena, kwa kuheshimu Mkataba wa Minski, ambao kwa kiasi kikubwa bado haujatekelezwa na wadau wanaohusika. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, shida na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Ukraine yanapewa ufumbuzi wa kudumu, mengine yatajipanga na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati wake.
Na Padre Richard. A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni