0
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo, ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu anayejitoa mwenyewe ili kuwafunulia watu huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Huu ndio upendo unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Ekaristi Takatifu ni chakula cha kweli kilichoshuka kutoka mbinguni!

Ni Fumbo la imani linalopaswa kusadikiwa, kuadhimishwa na kumwilishwa katika huduma ya upendo, udugu na mshikamano; hasa na maskini
pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya maisha mapya inayowawezesha waamini kushiriki uhai wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kujenga na kudumisha Agano Jipya na la milele linalofungwa kwa njia ya Damu Azizi ya Mwanakondoo wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni kielelezo makini cha umoja wa Kanisa. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu na kwa uelewa mpana maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha yao na kamwe wasiwe ni watazamaji wa mafumbo ya Kanisa!
Familia ya Mungu nchini Ghana, hivi karibuni imehitimisha maadhimisho ya Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa, huko Jimboni Jasikan, lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu na uinjilishaji mpya”. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake kama kielelezo cha imani tendaji. Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria katika mahubiri yake aliwataka waamini kuhakikisha kwamba, wanaadhimisha vyema Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa Ibada na Uchaji mkuu!
Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu katika ngazi yoyote ile anasema Kardinali Onaiyekan ni ushuhuda amini wa uwepo wa Kristo Yesu kati pomoja na watu wake! Huyu ni Kristo ambaye anafanya hija ya maisha pamoja na waamini wake. Ni kipindi cha kukuza na kudumisha Katekesi makini kuhusu maana, umuhimu na mambo msingi ambayo waamini wanapaswa kuyazingatia wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kama mahali muafaka pa kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu katika hali ya kimya kikuu, ili kumwachia nafasi aweze kuwajaza waamini huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka!
Lengo kuu la maadhimisho ya Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Ghana, lilikuwa ni kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa kuadhimisha miaka 60 tangu Ghana ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingireza hapo tarehe 6 Machi 1957 na kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 40 tangu Serikali ya Ghana ilipoanzisha uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican. Katika tukio hili, Baba Mtakatifu Francisko alimteuwa Kardinali Giuseppe Bertello, Rais wa Serikali ya mji wa Vatican, kuwa mwakilishi wake maalum katika maadhimisho haya. Itakumbukwa kwamba, Ghana iwekwa wakfu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kumbe, maadhimisho haya yalipania kukoleza tena upendo wa familia ya Mungu nchini Ghana kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia!
Kardinali Onaiyekan anakaza kusema, ushuhuda wa upendo huu unapaswa kumwilishwa katika ushuhuda wa upendo katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji na sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya, dhamana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini wajitahidi kuzingatia: sheria, kanuni na Mapokeo ya Mama Kanisa ili kukuza moyo wa Ibada na uchaji. Mapadre waandae vyema mahubiri yao ili kuwashirikisha waamini utajiri na amana ya Neno la Mungu. Waamini wawe na ujasiri wa kutamadunisha imani yao, ili kutoa nafasi kwa Kristo Yesu na Injili yake kusafisha, kuganga na kutakasa mila na desturi zinazosigana na adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Kamwe, Fumbo la Ekaristi Takatifu lisiadhimishwe kwa mazoea, hii ni kufuru kwa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Ibada ya Misa Takatifu ni tukio muhimu sana linalowakusanya watu wa Mungu katika Liturujia ya Neno na Ekaristi Takatifu na wala si mahali pa muziki wa dansi! Baadhi ya watunzi wa nyimbo za Ibada wamesahau umuhimu wa muziki mtakatifu unaopaswa kuwasaidia waamini kukuza, kudumisha na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa uchaji na badala yake, wameligeuza Kanisa kuwa ni kuwa eti ni ukumbi wa watu kuserebuka kwa raha zao wenyewe. Utamadunisho uzingatie na kuheshimu: Sheria, Kanuni, Mapokeo na miongozo inayotolewa na viongozi wa Makanisa mahalia.
Ibada ya ufunguzi wa maadhimisho haya ilihudhuriwa pia na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu ya binadamu, aliyeongoza Ibada ya Misa takatifu kwa heshima ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho. Amewataka waamini kumwomba Bikira Maria awasaidie kukuza na kudumisha imani, matumaini na mapendo kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu, linalomwilishwa katika huduma makini ya huruma, upendo na mshikamano. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni ushindi dhidi ya dhambi na mauti, kwa kuonesha na kushuhudia uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na watu wake. Hii ni chemchemi ya maisha mapya yanayorutubishwa kwa Neno la Sakramenti za Kanisa.
Familia ya Mungu nchini Ghana ilifanya maandamano makubwa yaliyohudhuriwa na waamini 10, 000 kutoka sehemu mbali mbali za Ghana. Mapadre walipokezana kubeba Ekaristi Takatifu na waamini kumshangilia Kristo Yesu kwa nyimbo zilizosheheni amana ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, nyimbo ambazo kamwe haziwezi kupoteza utamu wake kwani zinagusa imani ya Kanisa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kumsaidia mwamini kutambua na kuonja ukuu na utakatifu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Baada ya maandamano makubwa, Askofu mkuu Justice Yaw Anokye wa Jimbo kuu la Kumasi, Ghana, aliwafafanulia waamini kuhusu uwepo na uwamo wa Kristo katika Maumbo ya Mkate na Divai. Akawataka waamini kujitaabisha kusoma Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki katika maisha yao, ili waweze kupata majiundo endelevu katika maisha na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Alikazia umuhimu wa waamini kushiriki katika Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kwani hii ni Sakramenti ya uponyaji!
Kwa hakika, wachunguzi wa mambo wanasema, maadhimisho ya Kongamano la IV la Ekaristi Takatifu Kitaifa, huko Jimboni Jasikan, lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu na uinjilishaji mpya” yametia fola kwa ushiriki wa waamini, ushuhuda wa imani na uzito wa mafundisho yaliyotolewa katika kongamano hili. Sasa ni wakati kwa familia ya Mungu kumwilisha utajiri huu kwa ajili ya kukuza na kudumisha imani, ibada na uchaji kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Ni muda muafaka wa kuendeleza majadiliano na huduma kwa maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ekaristi Takatifu isaidie kukuza na kudumisha kifungo cha upendo, huruma na mshikamano miongoni mwa wanandoa, ili kweli familia za Kikristo ziendelee kuwa ni shuhuda wa Injili ya familia, chemchemi ya furaha kwa walimwengu. Ekaristi Takatifu iendelee kulijenga na kulidumisha Kanisa, kwani Ekaristi takatifu ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa.
Kwa upande wake, Askofu mkuu Jean Marie Speich, Balozi wa Vatican nchini Ghana, amekazia umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu katika maisha yao. Wajenge utamaduni wa kukaa kimya mbele ya Kristo Yesu, ili aweze kuzungumza nao kutoka katika undani wa sakafu ya maisha na mioyo yao, tayari kuziba utupu, wasi wasi na hofu zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia! Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu imeendelea kufafanuliwa na Mababa wa Kanisa katika historia, maisha na utume wa Kanisa na kwamba, kuna uhusiano mkubwa wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu inakuza imani kuhusu uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake.
Kwa mara ya kwanza, Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Ghana liliadhimishwa kunako mwaka 1951 huko Kumasi; Mwaka 1998 likaadhimishwa Jimboni Tamale na mwaka 2005 katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji nchini Ghana, likaadhimishwa katika Jimbo kuu la Kumasi, Ghana sanjari na kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Ghana kunako mwaka 1980.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top