Askofu mkuu Athur Roche, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa anasema kwamba, Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko iliyochapishwa tarehe 3 Septemba 2017 na inayoanza kutumika rasmi tarehe 1 Oktoba 2017 yaani “Motu Proprio: Magnum Principium” inayobadilisha Sheria za Kanisa namba 838 inakazia Kanuni za kurekebisha
maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kwa kujikita katika ukamilifu na kueleweka kwa Ibada yenyewe ili waamini waweze kushiriki kikamilifu. Haya ni mabadiliko yanayofumbatwa kwa namna ya pekee katika lugha ya Liturujia ya Kanisa na jinsi ya kufanya marekebisho haya mintarafu vitabu vya Ibada kutoka katika Madhehebu ya Kilatini. Ikumbukwe kwamba, Liturujia ni sala ya Kanisa ambayo kwa njia yake Mwenyezi Mungu hutukuzwa kikamilifu na wanadamu wanatakatifuzwa.
maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa kwa kujikita katika ukamilifu na kueleweka kwa Ibada yenyewe ili waamini waweze kushiriki kikamilifu. Haya ni mabadiliko yanayofumbatwa kwa namna ya pekee katika lugha ya Liturujia ya Kanisa na jinsi ya kufanya marekebisho haya mintarafu vitabu vya Ibada kutoka katika Madhehebu ya Kilatini. Ikumbukwe kwamba, Liturujia ni sala ya Kanisa ambayo kwa njia yake Mwenyezi Mungu hutukuzwa kikamilifu na wanadamu wanatakatifuzwa.
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikazia umuhimu wa lugha ya Liturujia, Jinsi ya kufanya Marekebisho na umuhimu wa matumizi ya lugha ya taifa katika maadhimisho ya Sakramenti na Visakramenti vya Kanisa. Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa tangu wakati huo limetoa miongozo mbali mbali na kufanya marekebisho baada ya kuchapishwa kwa Gombo la Sheria Mpya za Kanisa za Mwaka 1983 ambazo ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Lengo na maelekezo yote haya lilikuwa ni kujaribu kujibu changamoto na matatizo yaliyojitokeza mintarafu tafsiri sahihi ya Vitabu vya Liturujia ya Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko kwa kusoma alama za nyakati anaona ni vyema kuzingatia kanuni zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican mintarafu Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa sanjari na kufanya marekebisho msingi kwenye Sheria ya Kanisa namba 838 kwa kufafanua dhamana ya Vatican, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Mahalia, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Kikanda pamoja na wajibu wa Maaskofu mahalia. Wahusika wote hawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi, kila upande ukijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake kadiri ya mamlaka iliyopewa na Mama Kanisa, ili kusaidia kukamilisha tafsiri sahihi ya Vitabu vya Liturujia ya Kanisa, ambayo ni kwa ajili ya huduma ya Sala na maadhimisho ya Liturujia ya watu wa Mungu.
Askofu mkuu Athur Roche anakaza kusema, Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa limepewa dhamana kutambua “recognitio” na kudhibitisha “confirmatio” kwa kuzingatia mamlaka ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki mintarafu uwajibikaji wao katika shughuli za Kichungaji, Mafundisho Tanzu ya Kanisa na mipaka ya mamlaka na madaraka yao. Tafsiri mpya ya Sheria za Kanisa namba 838 inakazia dhamana ya Vatican katika kutambua yaani: kupitia, kutathmini na kulinda maana inayotolewa kwenye vitabu vya Ibada kwa lugha ya Kilatini, kama ilivyokaziwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wa Liturujia namba 39 – 40. Ni wajibu wa Vatican kuthibitisha Tasfiri ya vitabu vya Liturujia vya Kilatini iliyofanywa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki mahalia, ikiwa kama kazi hii imefanywa kwa uaminifu ili kweli Liturujia iweze kuadhimishwa katika ukamilifu wake.
Ni dhamana ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kuhakikisha kwamba, dhamana hii inatekelezwa kikamilifu. Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa lina dhamana ya mwisho kuthibitisha matumizi ya tafsiri ya vitabu vya Liturujia ya Kanisa kwa watu wa Mungu, ili kukuza na kudumisha umoja katika maadhimisho ya Sakramenti na Visakramenti vya Kanisa; Sala za Ekaristi Takatifu, Sala za Daraja Takatifu, Kanuni ya Misa pamoja na maadhimisho mengine ya Mafumbo ya Kanisa. Marekebisho ya tafsiri ya Sheria za Kanisa namba 838 yatasababisha marekebisho kadhaa katika Taratibu za Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni