0

Yamekuwa ni mapokeo kwa Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kutoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi wa Jimbo lake wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari! Huyu ndiye Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, Mfalme na Masiha anayewafunulia watu wa Mataifa uso wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.
Kardinali Pengo katika Ibada ya kutoa Daraja ya Ushemasi, amewataka Mashemasi wapya kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu katika maisha na utume wao, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu, vinginevyo wataishia pabaya kama ilivyokuwa kwa Mfalme Herode ambaye hofu na wasi wasi wake wa kudhani kwamba angeporwa Ufalme huo, aliishia katika mauaji ya watoto wasiokuwa na hatia! Kristo Yesu, alizaliwa kwenye Pango la kulishia wanyama kule mjini Bethlehemu. Mamajusi katika mawazo yao ya kibinadamu, wakaenda
kumtafuta Mfalme wa Wayahudi kwenye Jumba la Kifalme mjini Yerusalemu! Hapa walighafilika kama binadamu, lakini walipoiangalia nyota, ikawaelekeza hadi pale alipokuwepo Mtoto, wakafurahi sana na kumpatia Mtoto hazina zao yaani: dhahabu, uvumba na manemane. Kardinali Pengo anawaalika waamini lakini zaidi Mashemasi wapya kuongozwa na nyota ili hatimaye, waweze kukutana na Mtoto Yesu, Ufunuo wa upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu.
Kardinali Pengo, ametumia maadhimisho haya kutangaza Parokia Mpya ya Mtakatifu Benedikto, ambayo kwa sasa inakuwa ni Parokia ya 109 zinazounda Jimbo kuu la Dar es Salaam, hadi kufikia Januari 2018. Amewapangia Majandokasisi 5 vituo vya mwaka wa kichungaji pamoja na kuwabadilishia Mapadre vituo vya kazi na utume. Katika mabadiliko haya, Kardinali Pengo amemteua Padre Frank Mtabangu kuwa Katibu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Padre Aidan Mubezi aliyekuwa anashikilia nafasi hii amepangiwa kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mapadre Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S kwa ushirikiano na Padre Joseph Peter Mosha kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Chapisha Maoni

 
Top