Maadhimisho haya kwa mwaka huu yatafanyika Jimbo kuu la Genova, ambako waamini wataweza kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye kushuhudia imani yao kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu wakati wa maandamano kuzunguka viunga na mitaa ya mji wa Genova. Kardinali
Waamini wanahamasishwa kujiandaa kikamilifu
ili hatimaye, kuweza kuadhimisha Fumbo hili la imani linalopaswa kumwilishwa
katika familia na Jumuiya za Kikristo kwa kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na
ushiriki mkamilifu katika Ibada ya Misa takatifu na tafakari ya Neno la Mungu
linalomwilishwa katika ushuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili.
Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni fursa ya kukutana na Kristo katika
Neno la Meza ya huruma, upendo na huduma.
Waamini wanaposhiriki katika maadhimisho ya
Fumbo la Ekaristi Takatifu wamwachie nafasi Kristo ili aweze kuwamegea huruma
na upendo wake kwa njia ya Neno na hatimaye, wokovu unaobubujika kutoka katika
Fumbo la Msalaba. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa
Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu anayetembea na waja wake hadi utimilifu wa
dahali. Uwepo wake unafichika katika maumbo ya Mkate na Divai; Sakramenti ya
Upendo na chakula safi cha wasafiri kuelekea mbinguni kwa Baba.
Ekaristi Takatifu ni chachu ya huruma na
upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Uwepo wa Yesu katika Tabernakulo ni kielelezo
cha mwanga angavu na uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Kardinali Bagnasco
anakumbusha kwamba, Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo linaloendelea kuboreshwa
kwa njia ya: unyenyekevu wa moyo, sala na upendo uliopyaishwa na kufumbatwa
kwenye Jumuiya za Kikristo zilizotakaswa kwa Damu Azizi ya Kristo.
Maadhimisho ya Kongamano la XXVI la Ekaristi
Takatifu Kitaifa nchini Italia yanaongozwa na kauli mbiu “Ekaristi ni chemchemi
ya utume”. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa linalojikita katika Ekaristi,
hili ni Kanisa la kimissionari linalotumwa kutangaza na kushuhudia huruma na
upendo wa Mungu katika maisha ya watu! Waamini wanahamasishwa kuwa kweli ni
mashuhuda na vyombo vya upendo unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya
Ekaristi Takatifu kwa kushuhudia kile walichoona na kusikia, kwa kuwatangazia
wengine, ili wao pia waweze kushiriki na hatimaye, kufumbatwa katika Fumbo la
Utatu Mtakatifu. Kardinali Angelo Bagnasco anahitimisha barua ya mwaliko
kwa familia ya Mungu nchini Italia kujiandaa vyema kwa ajili ya maadhimisho ya
Kongamano la Ekaristi Takatifu kitaifa, ili hatimaye, kuvuna matunda
yanayokusudiwa yaani: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni