Tunaadhimisha Sherehe
ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo kila mwaka siku ya Alhamisi
inayofuata baada ya kuadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Kwa kuwa Sherehe
hiyo ni Sikukuu ya amri, Kanisa imeruhusu
kuiadhimisha siku ya Dominika inayofuata ili Wakristo
wote waweze kutimiza wajibu wao wa kusali .
Kuanza na Kuenea
Kihistoria
Sherehe hiyo ilianza huko Ufaransa kutokana na maono ya mtawa Juliana aliyoanza
kuyapata mnamo mwaka
1209. Baada ya juhudi kubwa ya kumwomba Askofu wake
kuanzisha Sherehe hiyo, hatimaye ombi la sista Juliana lilipokelwa.
Mwaka 1246 iliadhimishwa kwa mara ya kwanza huko Lie’ge nchini Ufaransa.
Mwaka 1264 Papa Urban
IV (wa nne) aliitangaza Sherehe hiyo iadhimishwe popote katika Kanisa. Kumbe
kabla ya kuteuliwa kuwa Papa, Urban alikuwa shemasi na baadaye padri
wa jimbo hilo la Liege, alishaifahamu historia ya sikukuu hiyo. Papa
Urban IV alimwomba Mt.Thomaso wa Akwino(1224-1274) ambaye alikuwa mtaalamu sana
katika elimu ya Mungu kuandika sala na tenzi zote za Sherehe hiyo. Tunaona
utaalamu wake hasa katika Sekwensia ndefu ya Sherehe hiyo.
Kwa bahati mbaya Papa
Urban IV alifariki mwaka huohuo na kufanya agizo lake kutotekelezwa kwa miaka
kadhaa. Alikuwa Papa Klementi V (1264-1314, ambaye alikuwa Papa kuanzia 1305
katika Mtaguso wa Vienna(1311-1312) aliagiza kwa mkazo kwamba Sherehe hiyo
iadhimishwe potepote katika Kanisa Katoliki. Pamoja naye, baadaye Papa Yohane
XXII (ishirini na mbili) naye alisisitiza jambo hilo. Sherehe hiyo mpaka miaka
ya karibuni ilikuwa ikiitwa:Sherehe ya Mwili wa Kristo (Corpus
Christi). Ni dhahiri kuwa mwelekeo wa Sherehe ulikuwa
hasa kumwabudu Kristu katika Mwili wake kama jina la Sherehe lilivyosimama.
Basi mnamo mwaka 1849 Papa Pius wa tisa aliweka Sikukuu ya Damu
Takatifu ya Yesu ambayo iliadhimishwa Julai 1. Kwa hiyo kulikuwa
na sikukuu mbili: Sherehe ya Mwili wa Bwana na Sikukuu
ya Damu Takatifu ya Bwana.
Marekebisho
ya Mtaguso
Katika marekebisho
yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano ni pamoja na kurekebisha
Sherehe hiyo. Katika Katekisimu ndogo tunasoma:Ekaristi Takatifu ni
Sakramenti ya Mwili na Damu takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu - mtu,
katika maumbo ya mkate na divai. Mkate na divai ni alama za
Sakramenti.
Kwa vile Sikukuu hizo
mbili zilikuwa na mwelekeo wa kuzitenga alama wazi za Sakramenti hiyo moja Mwili peke
yake na Damu takatifu kuadhimishwa katika nafasi tofauti basi
marekebisho ya Mtaguso mkuu yameziunganisha kuwa Sherehe moja. Sasa Sherehe hii
inaitwa: Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu
Kristo. Ni dhahiri kuelewa kwamba mwili ulio hai ni pamoja na damu
yake hai pia. Jina hilo ndefu hufupishwa kwa kusema: Sherehe ya
Ekaristi Takatifu.
Maandamano ya
Kuabudu
Tangu Sherehe hiyo
ilipoanza imekuwa na utaratibu wa kufanya maandamano pamoja na Sakramenti ya
Ekaristi ikichukuliwa katika chombo maalum kiitwachomonstransi ili
kumwabudu Bwana wetu Yesu Kristo hadharani. Maandamano hayo yamekuwa yakipambwa
na bendera nyeupe na hata rangi nyingine zenye kuvutia pamoja na maandishi ya
kumtukuza Yesu katika Ekaristi. Bendera na vipeperushi hivyo vinapamba sehemu
mbalimbali ya maandamano hayo; yaani sehemu ya watoto, vijana, akinababa na
hata akinamama. Wasichana au pengine akinamama wachache walioandaliwa huwa
mbele ya Ekaristi na kumwaga maua kama ishara ya heshima kubwa kwa Bwana wetu
Yesu Kristo.
Kwa kawaida katika
maandamano hayo huandaliwa kituo kimoja au viwili na hata zaidi kutegemea urefu
wa njia ya maandamano. Katika vituo hivyo Ekaristi itawekwa juu ya meza
iliyopambwa vizuri na waamini husimama au hupiga magoti ili kusali kwa kitambo. Hata
iwapo maandamano siyo marefu inashauriwa sana kuwa na kituo angalau kimoja kusudi
tendo hilo la kuandamana hadharani liimarishwe na sala zinazotolewa na Wakristo
wote kama jumuiya moja inayoabudu. Katika vituo hivyo kuhani huongoza sala
kuombea parokia, Jimbo, taifa na serikali au shida za
jamii kwa jumla.
Sote Tumwabudu
Maandamano hayo na
Ekaristi yasiwe tu kama tendo la haraka kwani ni tendo la kuabudu. Tuandamane
kwa heshima mbele ya Bwana wetu Yesu Kristo. Inasisitizwa sana kuwepo na kituo
angalau kimoja ambapo waamini wote kwa pamoja watatulia wakiabudu.
Tunawapongeza sana
waamini wote wanaoshiriki maandamano hayo kwa moyo wa ibada na uchaji,
wakishiriki kuimba nyimbo za Ekaristi na nyingine zinazofaa.
Wanaonyesha mfano mzuri wa kudhihirisha imani hadharani. Iwapo kuna Misa mbili
baadhi ya Wakristo walioshiriki Misa ya kwanza huja mwishoni mwa
misa ya pili ili wapate kushiriki maandamano hayo muhimu ya kumwabudu Yesu.
Hongera sana kwa kuonyesha uhai wa imani namna hiyo.
Kwa upande mwingine
lakini tumeshuhudia baadhi ya waamini waliokuwa wakisimama pembeni mwa njia ya
maandano na kuongea bila kushiriki maandamano. Huwaangalia wenzao
wanapoandamana na wengine huendelea na biashara zao. Hilo si jambo zuri kamwe!
Ni mara moja tu kwa mwaka mzima Liturujia imeweka utaratibu wa kumwabudu Yesu
kwa namna hiyo. Wakristo wanapaswa kuvumilia adha ya kuandamana na kujitoa muda
wao kwa ajili ya Liturujia hiyo maalum ya kumwabudu Yesu na kukiri
imani hadharani.
Tendo hilo la
kuandamana ni tendo la kumwabudu Yesu Kristo na kukiri kwa dhati kwamba yeye
Mungu - mtu yumo katika Sakramenti hiyo ya Mwili na Damu yake takatifu. Pamoja
na hilo, ni tendo la kumshukuru kwa kudumu na waamini
katika Sakramenti hiyo. Anakaa katika Sakramenti hiyo usiku na
mchana pamoja nasi. Wakristo wangapi huenda pale kanisani
kumwabudu?
Kumpokea Yesu kwa
uchaji
Yesu tunayemwabudu ni
pia chakula chetu cha uzima wa milele. Kwa nafasi hii inafaa
kukumbuka utaratibu wa kupokea Komunyo kwa heshima stahiki. Wakristo wajiandae
vizuri kiroho na hata kuwa safi kimwili kwa kupokea Ekaristi takatifu. Mahali
wanapopokea Ekaristi wakiwa wamesimama mstari wakumbuke kuonyesha tendo la
heshima kama vile kuinama kabla ya kupokea Ekaristi.
Wanaopokea Ekaristi
mkononi wakumbuke kuwa mikono yote miwili iwe
tayari kwa tendo hilo kuu la kumpokea Bwana . Isiwe, kwa mfano, mkono
moja unashika leso au simu. Inawapasa kusafisha kwa ulimi kwenye kiganja pale
ilipowekwa Ekaristi takatifu kwa sababu mara nyingi hubaki
chembechembe ambazo zisiposafishwa kwa ulimi huanguka sakafuni na
kukanyagwa. Kumbe chembechembe hizo ni sehemu ya Mwili wa Bwana.
Mkristo
akishampokea Yesu katika Sakramenti haitakiwi kuinama tena bali hurejea mahali
pake kwa uchaji na kuabudu kimya kwa kitambo. Halafu aungane na wenzake katika
kuimba. Tendo hili hutendeka mara nyingi basi lifanyike kwa heshima na
uchaji.
Chanzo cha habari ni
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni