Mashemasi ni
watumishi na mitume wa Kristo wanaotumwa kumtangaza na kumshuhudia Yesu kwa
njia ya huduma ya mapendo. Yesu Kristo amejifunua kama Neno wa Baba ambaye
amekuja kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, akawa ni chemchemi ya furaha
na huduma kwa wote, yaani akawa Shemasi. Hii ndiyo
changamoto inayotolewa kwa
watangazaji na wahudumu wa Habari Njema ya Wokovu kuhakikisha kwamba, wanafuata
kikamilifu maagizo ya Kristo Yesu.
Ikumbukwe kwamba, dhamana ya
Uinjilishaji ni kwa Wakristo wote na huduma ya upendo ni njia muafaka ya
kumwilisha utume wa kumfuasa Yesu, kielelezo cha ushuhuda wa maisha
yanayojikita katika huduma. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba
Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili
ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Mashemasi wa kudumu, Jumapili
tarehe 29 Mei 2016. Ili kuwa kweli ni watumishi wema na waamifu, kuna haja ya
kujikita katika dhana ya uwepo, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili
ya zawadi ya huduma kutoka kwa Mungu inayotolewa kama sadaka safi mbele ya
Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu anawataka Mashemasi kuwa wazi na tayari daima kutoa
huduma inayobubujika kutoka katika fadhila ya unyenyekevu wa moyo, huku
wakiendelea kushangazwa na Mungu katika maisha ya kila siku. Mtumishi mwema na
mwaminifu anafahamu na kutambua dhamana, wajibu na nafasi yake, tayari
kuhudumia hata wale wanaokuja kuomba msaada nje kabisa ya muda uliokubalika,
kielelezo cha sadaka katika maisha. Kwa njia ya maisha ya kuwajibika, huduma ya
Mashemasi itaweza kuzaa matunda ya Kiinjili.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Injili ya Jumapili ya Tisa ya
Kipindi cha Mwaka wa Kanisa inakazia kwa namna ya pekee kabisa huduma ambayo
ilitolewa na Yesu kwa kuwaponya wale waliokimbilia huruma na upendo wake. Yesu
anashangazwa na maneno yaliyotolewa na Akida kwa kujiona kuwa hastahili kamwe
Yesu kuingia katika nyumba yake, lakini aseme neno tu na mtumishi wake atapona.
Unyenyekevu huu wa Akida unamgusa Yesu, kielelezo cha mfumo wa maisha ya Mungu
ambaye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mungu ni upendo
unaojidhihirisha kwa namna ya pekee katika kumhudumia mwanadamu kwa uvumilivu
na wema, daima akiwa tayari kuteseka kutokana na dhambi za binadamu. Mungu
anatafuta njia itakayomwezesha mwamini kuwa mtu mwema zaidi katika maisha,
changamoto kwa Wakristo kumuiga Mwenyezi Mungu ili kuwahudumia wengine; kwa
kuwapokea kwa ukarimu, huruma na mapendo; kwa kuendelea kujitahidi kuwafahamu
bila kuchoka; kwa kuwasikiliza kwa makini na kuwahudumia kikamilifu.
Mashemasi wakiwa na moyo wa unyenyekevu hapo wito wao kama
wahudumu wa upendo, utaweza kukua na kukomaa. Waamini wanakumbushwa kwamba,
kila mmoja wao anapendwa na amechaguliwa kwa namna ya pekee na Mwenyezi Mungu;
anaitwa na kutumwa kuhudumia, baada ya kuponywa kutoka katika undani wa maisha.
Ili kuwa wahudumu wema na waaminifu kuna haja kwanza kabisa kuwa na afya ya
kiroho; kwani moyo ulioponywa na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, hauwezi kuwa
mgumu na kujifungia katika ubinafsi wake.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Mashemasi kumwomba Kristo
Yesu, ili aweze kuwaponya, ili kufanana naye kama marafiki na wala si kama
watumwa. Mashemasi wawe ni watu wa sala inayowasilisha furaha na matumaini;
magumu na changamoto za maisha wanazokabiliana nazo kila siku. Hii iwe ni sala
ya kweli inayopeleka maisha kwa Kristo. Pale Mashemasi watakapokuwa wanahudumia
katika Ibada ya Misa Takatifu, hapo wataweza kuona uwepo wa Kristo Yesu
anayejisadaka kwa ajili yao, ili wao pia waweze kuwa ni sadaka kwa wengine.
Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri katika maadhimisho
ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Mashemasi wa kudumu kwa
kukazia utayari katika maisha; unyenyekevu wa moyo na majadiliano endelevu na
Yesu katika sala na kwa njia hii, kamwe hawatakuwa na woga wala makunyanzi ya
kuwa ni watumishi wa Kristo, tayari kukua na kutoa faraja kwa mwili wa Kristo
unaojionesha kati ya maskini wa nyakati hizi!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni