0

Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu ni Sakramenti pacha zinazotegemeana na kukamilishana, kama sehemu ya mchakato wa ukumbusho endelevu wa uwepo wa Kristo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Katika huduma hii takatifu kwa familia ya Mungu, Mapadre hawana budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo endelevu wa Kristo katika maisha yao. Mapadre wanatakiwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, katika hali ya unyenyekevu na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa utii. Mapadre watambue daima kwamba, huduma yao ya Kiekaristi inasimikwa katika unyenyekevu unaotolewa na Kristo kwa Kanisa lake. Ukuhani ni madaraka ya mchungaji mwema anayeyatoa maisha yake kwaq ajili ya Kondoo wake.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume kuhusu Ekaristi Takatifu Sakramenti ya Upendo, “Sacramentum caritatis” anabainisha kwamba, Ekaristi Takatifu ni Fumbo linalopaswa kuadhimishwa kwa moyo wa ibada na uchaji; ni Fumbo linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Kikristo kwa kuwa ni Ekaristi kwa jirani na kuwatangazia wengine kwa njia ya ushuhuda wenye mguso na mashiko; Ekaristi ni
Fumbo linalopaswa kutolewa kwa ajili ya ulimwengu, ili kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji na utamadunisho.
Askofu mteule Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Tanzania anawataka Wakleri, Watawa na Waamini wajenge na kuimarisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, licha ya kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu. Hii ni changamoto kubwa iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake, ni kiongozi aliyekuwa na Ibada ya pekee ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Mapadre kwa namna ya pekee, watenge muda wa kukaa, kuzungumza na kumwabudu Yesu katika Sakramenti kuu ya Ekaristi Takatifu.
Naye Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anawataka Wakleri kuendelea kupyaisha maisha yao kwa kujitoa bila ya kujibakiza kama ilivyokuwa kwa Kristo, Bwana na Mwalimu. Kristo alikuwa ni kiongozi mahiri, mwaminifu na mtii kwa Baba yake wa mbinguni, changamoto kwa Wakleri kujivika karama hizi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu.
Kristo alikuwa na upendo mkuu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, Wakleri waoneshe upendo, unyofu, unyenyekevu na huruma kwa Familia ya Mungu wanayoihudumia, ili kwa njia ya maisha na utume wao, watu waweze kumkimbilia Mungu. Wakleri watambue kwamba, Yesu Kristo ni Bwana, Mlezi na Mwalimu wa wakleri katika maisha na utume wao.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.


Chapisha Maoni

 
Top