Tangu zamani za kale Waisraeli walitolea
sadaka za wanyama na mazao kama alama ya
shukrani. Hata wakati waisraeli
walipotoka utumwani Misri ibada ya pasaka na sikukuu ya mkate isiyochachwa
ikaunganishwa na kuadhimishwa sasa kama sadaka moja ya ibada ya wokovu,
ikifanyika sasa kukumbuka walipotoka utumwani Misri. Tangu zama hizo hata leo
bado wanadhimisha ibada hii. Wakati wa Kristo, mwanakondoo
wa Mungu amejidhabihu msalabani akajitoa kama chakula katika karamu ya mwisho
katika juma la pasaka ya waisaraeli. Tunaadhimisha ibada hiyo kila mwaka katika
juma kuu. Kristo ameiletea dunia yote wokovu kwa karamu yake na msalaba wake.
Kadiri ya imani yetu, tendo lile lile la karamu na msalaba linaendelezwa na
Kristo katika misa takatifu iliyo karamu na sadaka ile ile ya Kristo.
Karamu (chakula cha) ya bwana maana yake ni
Ekaristi Takatifu. Karamu hii ni ukumbusho wa karamu ya mwisho ya Bawana pamoja
na mitumume waleke alipoweka Ekaristi Takatifu. Mapokeo fulani ya Kiyahudi
yalieleza neno pasaka kwa maana ya kuvuka, yaani kuvuka bahari ya Shamu - kut.
14. Kristo na sisi pamoja naye tutauvuka ulimwengu huu wa dhambi na kwenda kwa
Baba katika nchi ya ahadi – Kut. 21. Kristo ameshatuvusha, hivyo ni juhudi na
bidii yetu kubaki pamoja naye ili tufike tuendako. Ili tufike kwa Baba
yahitajika juhudi binafsi, juhudi ya jamii inayoamini - walipo wawili au watatu
kwa jina langu nami nipo kati yao. Lakini zaidi sana yahitajika neema ya Mungu
ili tuweze kufika kwake.
JUU YA KARAMU YA PASAKA.
Kadiri ya wainjili Matayo, Marko, na Luka,
Yesu alifanya karamu ya pasaka siku ya alhamisi jioni – Mt. 26:17, Mk.
14:12, Lk.22:7. Yesu alipokula karamu ya Pasaka jioni ile aliweka ibada mpa ya
karamu. Katika kuweka karamu mpya katikati ya karamu ya Pasaka, Yesu alidokeza
kwamba ibada yake mpya ni utimilizo wa pasaka ya kale - karamu ya Bwana
au chakula cha bwana maana yake ni ekaristi takatifu -1Kor.11:20. Karamu hii ni ukumbusho wa karamu ya mwisho ya Bwana pamoja na mitume
wake alipoweka ekaristi takatifu. Nayo inakumbusha kifo cha Yesu, tena ni amana
ya karamu ya kimasiya - siku za mwisho - Mt. 26:29, Md. 2:42 - wakawa
wakidumu katika fundisho la mitume na katika ushirika na katika kuumega mkate
na katika kusali. Katika tendo hili kuu na takatifu, Yesu aliweka sakramenti ya
daraja, sakramenti ya ekaristi na pia amri ya Bwana ya kupendana.
SAKRAMENTI YA DARAJA
Katika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki
tunasoma hivi;
Na. 1539 - taifa teule liliwekwa na Mungu kama
ufalme wa makuhani na taifa takatifu lakini ndani ya taifa la Israeli Mungu
alichagua moja ya makabila kumi na mawili, lile la Walawi akalitenga kwa ajili
ya huduma ya liturujia. Mungu mwenyewe ni fungu la urithi wake. Ibada ya pekee
ilitakasa mianzo ya huduma ya liturjia. Mungu mwenyewe ni fungu la urithi wake.
Ibada ya pekee ilitakasa mianzo ya ukuhani wa agano la kale. Ndani yake
makuhani waliwekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu ili kutoa
matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi – Ebr. 5:1, Kut. 29:1-30, Law. 8.
Na. 1540 - ukuhani huu uliwekwa kwa ajili ya
kutangaza neno la Mungu - Mal. 2:27-29 na kwa ajili ya kurudisha uhusiano
pamoja na Mungu kwa sadaka na sala. Hata hivyo unabaki hauna nguvu ya kuleta
wokovu ukiwa na lazima ya kurudia sadaka zake bila kukoma na kutoweza kutoa
utakaso halisi ambao ungetimizwa tu na sadaka ya Kristo – Ebr. 5:3,
7:27,10:1-4.
Kwa kifupi sakramenti ya
daraja ni sakramenti ya upendo. Ili sakramenti ya ekaristi iliendelee
kuadhimishwa ni lazima wawepo mapadre ambao kwa dhamana waliyopewa wanaweza
kugeuza mkate na divai kuwa mwili na damu ya Bwana wetu Yesu Kristo.
SAKRAMENTI YA EKARISTI
Na. 1322 - Ekaristi Takatifu hukamilisha
kuingizwa katika ukristo wale walioinuliwa katika heshima ya ukuhani wa kifalme
kwa ubatizo na kufananishwa kwa ndani zaidi na Kristo na kwa kipaimara
hushiriki pamoja na jumuiya yote katika sadaka moja ya Bwana.
Na. 1323 - mwokozi wetu katika karamu ya
mwisho usiku alipotolewa aliweka sadaka ya ekaristi ya mwili na damu yake. Alifanya
hivyo ili kuendeleza sadaka ya msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi
amwachie bibi arusi mpendwa yaani kanisa ukumbusho wa kifo chake na ufufuko
wake sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya pasaka ambamo
Kristo huliwa na roho hujazwa neema na ambamo tunapewa amana ya uzima wa
milele.
Na. 1324 - Ekaristi ni chemichemi na kilele
cha maisha yote ya kikristo. Sakramenti nyingine kama zilizo pia huduma zote za
kanisa na kazi za utume zaungana na ekaristi na zaelekezwa kwake. Kwani katika
ekaristi takatifu mna kila hazina ya kiroho ya kanisa yaani kristo mwenyewe
pasaka wetu.
Na. 1325 - Ekaristi ndio ishara thabiti na
sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja ule
wa taifa la Mungu ambao unalifanya kanisa liwepo ekaristi ni kilele cha tendo
la Mungu la kuutakatifuza ulimwengu katika kristo na kilele cha tendo la
kumwabudu Mungu wampalo watu kristo na kwa njia yake wampalo baba katika
mtakatifu.
Na. - 1326 - mwishowe kwa njia ya adhmisho la
ekaristi tunaungana tayari sisi wenyewe na liturjia ya mbinguni na tunaanza
kutangualia kushiriki uzima wa milele Mungu atakapokuwa yote katika wote - 1
Kor. 15:28 - basi vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake ndipo mwana mwenyewe
naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiisha vitu vyote ili kwamba Mungu awe
yote katika wote.
Na. - 1327 - kwa ufupi ekaristi ndiyo juma na
muhtasari wa imani yetu, namna yetu ya kufikiri hulingana na ekaristi na
ekaristi kwa zamu yake huimarisha namna yetu ya kufikiri.
MAHUBIRI YANAJIKITA KATIKA VIFUNGU VIFUATAVYO:
I.
KUT. 12:1-8,11-14
II.
1 KOR. 11: 23-26
III.
YOH. 11:13,1-5
Mazingira ya nchi ya Israeli na makazi -
umbali na ugumu wa njia – msafiri alipofika au bado akiwa safarini alihitaji
kupumzika na katika kupumzika huko alihitaji kuoshwa miguu na kupewa chakula.
Hiyo ndiyo ilikuwa desturi ya wenyeji. Mapumziko haya yalihitajika ili kupata
nguvu ya kuendelea na safari baadaye au kesho yake baada ya mapumziko hayo.
Ekaristi Takatifu yachukua nafasi hiyo sasa.
Maisha ya mkristo hapa duniani ni sawa na safari ndefu na ngumu. Safari ya
kwenda mbinguni kwenye makao ya milele. Njiani tunachoka na kunyauka hata
kupata kishawishi cha kutaka kukata tamaa. Leo hii bado kishawishi hiki kipo.
Lakini twaona kuwa Yesu katufutilia mbali ugumu huo na leo hii anatupatia
ekaristi, pumziko letu - ndani yake tunapata muda wa kunawa miguu na
kupata chakula cha mwili na roho tayari kuendelea na safari yetu iliyo mbele
yetu tena ngumu, ya kwenda juu kwa baba. Ekaristi daima ni viaticum au nguvu ya
safari kwani tunapata nguvu ya kuendelea na safari yetu kwenda juu.Mambo yanayofanyika ni kukaa pamoja mezani, kula na kunywa pamoja
na kuagana na kwa mifano hai n.k. Tendo la kuosha miguu - Mtume Petro anasita
na angependa yeye afanye jambo hilo kwa Yesu. Jibu la Yesu - mimi nitakuosha
miguu wewe - Yoh .13:8.
Kwanza Yesu anatuosha sisi na uchafu wetu ili
tuwe watu wake,
·
Halafu tunapata kibali
cha kuosha miguu ya dada na kaka zetu katika kristo,
·
Mtume Petro alipoelewa
hilo alisema basi Bwana siyo miguu tu hata pia mikono na kichwa – Yon. 13:9,
·
Ili hilo liwezekane,
Bwana atuita leo tujaribu kulielewa fumbo hilo na kuwa karibu naye. Ili
iwezekane kuoshwa hatuna budi kuwa karibu na Bwana - yule aliye na sinia ya
maji, sabuni na taulo. Leo hii alhamisi kuu Bwana anatuosha miguu ili tena tuwe
wasafi tuweze kushiriki karamu yake na tuwe na nguvu ya kuendelea na safari
yetu ya kwenda mbunguni,
·
Upande mwingine wa
shilingi baada ya Bwana kuosha mitume miguu anawaagiza nao waende wakafanye
hivyo hivyo. Baada ya ibada yetu ya leo tunaagizwa na Bwana nendeni nanyi
mkafanye hivyo hivyo – Yoh. 13:12-15,
·
Kwa tendo hili Yesu
anatuachia ukumbusho wa ajabu tena ukumbusho mtakatifu ambao unaambatana na
wajibu mkubwa mbele yetu,
·
Ametuosha miguu na
anatuagiza tuwaoshe wenzetu miguu- ekaristi ni utumishi,
·
Kama ekaristi ni mahali
ambapo Bwana anatuosha miguu basi maisha yetu ya kila siku yatuwajibisha
kufanya hivyo hivyo. Haiwezekani kupokea/kushiriki ekaristi ambalo ni tendo
takafitu na kuacha kuendeleza tendo la kuoshana miguu,
·
Ekaristi ni maisha na
anayefanya kinyume chake yaani anayeshiriki ekaristi takatifu na hapo hapo
akaendeleza tena kwa makusudi mazima alama yoyote inayopingana na hilo basi
anakufuru,
·
Yesu alivunja/alimega
mkate wa ekaristi na kuosha miguu ya mitume,
·
Ni lazima tufuate
mfano wake katika altare ya ekaristi na katika altare ya maisha,
·
Kinachoonekana hapa ni
kwamba katika tendo lolote la wokovu ambalo Mungu amefanya kwetu ni yeye kwanza
anayeanzisha hilo halafu anatualika sisi tuende. Biblia takatifu inatuonesha hilo
na Mungu anachukua jukumu kwanza halafu anatualika sisi tuende tukafanye hivyo
hivyo.
CHANGAMOTO
Ekaristi ni maisha, ni uhai, ni upendo - kujigawa vipande,
kuwaosha wengine, kubariki kazi zao nzuri, kuanza upya, kuvuka vizingiti ya
makwazo, ni wajibu na zaidi sana ni fumbo. Tusipoteze muda wetu kutaka
kulielewa fumbo hili kwa akili ya kibinadamu. Yesu ameshatuachia mfano hai
nanyi fanyeni hivyo hivyo. Tutumie muda wetu kuweka katika matendo yale
aliyotuachia Bwana - nanyi fanyeni hivyo hivyo. Tuinuke, twende tukawaoshe
wenzetu miguu, mikono na hata miili yao.
Bwana Yesu katika upendo wake alituona tumechoka, tu wachovu,
tulihitaji kuoshwa, kulishwa na kupumzika. Nawe ndugu yangu chukua dakika
chache uone leo, dunia yetu inahitaji nini zaidi ya hicho ufanyacho. Jirani
yako anahitaji nini zaidi, mwenzako wa ndoa, watoto wako, mtaa wako, jumuiya
yako n.k unaahidi nini kwao katika pasaka hii unayoadhimisha mwaka huu? Yesu
aliona mahitaji yetu akatupatia maji tunywe na mkate tule ili tubaki wazima
daima. Yesu ametupatia ekaristi, daraja la upadre na zaidi sana jukumu la
upendo ili tuweze kufika kwake. Na siyo kufika tu bali tufike tukiwa wazima na
si wafu. Tunalo jukumu la kutakatifuza hali zetu, maisha yetu na sadaka
zetu zaidi ili tufike mbinguni.Hilo ndilo lengo na mapenzi yake baba.
UFAFANUZI WA KINA
Katika injili, Mtume Petro anasita kuoshwa miguu na Yesu. Baada ya
mvutano anakubali. Kuosha na kuoshwa miguu ni sehemu ya maisha ya kikristo. La
muhimu zaidi ni kumwacha Yesu atuoshe sisi. Nisipokuosha mimi basi huna shirika
nami - Yoh 13:8. Kwanza Yesu hutuosha miguu sisi ili tuwe safi. Halafu
tukishakuwa safi tunapata nguvu na uwezo wa kuosha wengine. Mtume Petro
alipoelewa hilo alishinda mashaka yake na akalia Bwana si miguu tu bali hata
mikono na miguuu – Yoh. 13:9. Kutoka kwetu Yesu anahitaji uwepo wetu na kumpa
Yesu nafasi ya kutuosha miguu. Matokeo yake ni sisi kufanya kama alivyofanya
Bwana yaani kuosha miguu ya wenzetu. Baada ya Bwana kuwaosha miguu
aliwaambia mmeelewa nilichofanya? Mwaniita mwalimu na Bwana na ni sawa. Kama
mimi nimefanya hivyo basi nanyi fanyeni hivyo kati yenu – Yoh. 13:13-15.
Alikwisha kusema kuwa ni lazima kula mwili wake na kunywa damu
yake ili kuupata uzima wa milele. Hivyo ekaristi kuu ya Yesu inaanza kwa kuosha
miguu na kumalizika na ushuhuda katika utukufu wa msalaba. Hapa Yesu anaonesha
wazi utukufu wa Mungu katika umbo la mwili. Anachukua hali ya mtumwa ili tuweze
kumfikia. Yesu anajifunua ili tuweze kuuona utukufu wa Mungu.
Yesu anakula pamoja na mitume kama walivyofanya wengine lakini
katika mlo huu anaongeza maneno - toeni mle na toeni mnywe - huu ni mwili wangu
na kunywa damu yangu. Marafiki wa kweli hukaa pamoja, huufurahia uwepo wao kati
yao na si tu kumbukumbu na matukio. Leo hii na wakati huu kwa imani tunashiriki
mapenzi haya ya Mungu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Hapa Bwana Yesu anatengeneza mwanzo mpya wa maisha na namna mpya
ya kuishi. Kama ekaristi ni mahali ambapo bwana huosha miguu yetu basi maisha
ni mahali ambapo sote hatuna budi kuoshana miguu. Ekaristi ni maisha na maisha
ni Ekaristi.
Zawadi na mfano tuupatao katika kuosha miguu ni kielelezo
tosha cha ukristo wetu. Tusiufananishe ukristo na mtindo fulani wa
kimaadili/kimaisha tu. Kwanza ya yote ni zawadi – Mungu anajitoa mwenyewe
zawadi kwa ajili yetu. Hatoi kitu bali yeye anajitoa mwenyewe – anakuwa uzima
yaani katika Fumbo la Ekaristi. Tunahitaji kuosha miguu - alama ya
unyenyekevu kabisa na Yesu alifanya hivyo akijua aina ya kifo kinachomsubiri -
kama mwizi -akafanya hivyo akionesha mfano - kuosha dhambi zetu kila siku.
Tutafakari juu ya sakramenti ya kitubio. Katika sakramenti hii daima Yesu
anaosha dhambi zetu ili tuweze kukaa meza moja naye. Yesu aliosha miguu wakati
wa karamu ya mwisho. Wakristo wa kwanza walielewa ni mlo wa aina gani.
Walisherehekea hilo siku za Dominika ikawa mazoea yao.
Mazingira ya nchi ya Palestina - milima na mawe. Na safari
nyingi wakati ule zilifanywa kwa miguu na msafiri alipofika au kwa mwenyeji au
mahali pa kulala alipewa maji ya uvuguvugu ili kukanda na kuosha miguu
iliyokuwa imechoka na kudhoofu. Baada ya hapo alipewa chakula na mwenyeji
wake. Ikieleweka katika mtazamo huo, Ekaristi ni mahali pa kuponea kwa
ajili ya wasafiri. Maisha ya mkristo ulimwenguni ni safari ya hija, safari
ndefu. Njiani tunakumbana na mengi, vishawishi na kukata tama. Yesu katupatia Ekaristi
mahali pa kuweza kupata nafuu na afadhali ya maisha. Tunapotoa komunyo pamba
kwa mgonjwa twaita viaticum - msaada wa safari, hutupatia nguvu katika safari
na katika mahangaiko ya maisha.
KKK 1409 – EKARISTI NI KUMBUKUMBU YA PASAKA YA KRISTO, yaani ya
kazi ya wokovu iliyotekelezwa kwa maisha, kifo na ufufuko wa kristo, kazi
inayofanywa iwepo kwa tendo la kiliturjia.
Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.
Chanzo cha habari ni
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni