0
Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linaitaka Serikali ya Nigeria kuhakikisha usalama wa raia mali zao dhidi ya mashambulizi na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa nchini humo! Tamko la viongozi wa Kanisa nchini Nigeria linafuatia mashambulizi ya risasi yaliyofanywa dhidi ya Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja alipokuwa barabarani kati ya
Bebin na Ekpoma, Jimbo la Edo.
Kardinali Onaiyekan, Ijumaa, tarehe 22 Aprili 2016 wakati akirejea kutoka katika Ibada ya kumbu kumbu ya miaka 10 tangu Askofu mkuu Augustine Obiora Akubeze alipowekwa wakfu na kusimikwa rasmi kama Askofu mahalia! Dereva wa Kardinali Onaiyekan anasema, wakati akipunguza mwendo wa gari kutokana na shimo, ghafla bin vu, watu wawili waliokuwa na silaha waliaanza kufyatua risasi kuwaelekea wao na wengine waliokuwa wanafyatua risasi kutoka nyuma!
Dereva ilimbidi kugeuza gari na kurudi nyuma na baadaye wale watu waliokuwa na silaha walikimbia tena mstuni. Shambulizi hili limepasua kioo cha gari na kuharibu baadhi ya sehemu za gari. Dreva na Kardinali Onayeikan wanamshukuru Mungu kwa kuwasalimisha salama salimini!
Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Kardinali Onaiyekan anasema hakuwa mlengwa mkuu wa shambulizi hili kwani hii ni barabara kuu na ilikuwa na magari mengine. Kwa bahati mbaya walishambuliwa kwa vile tu walijikuta wakati mahali pabaya kwa wakati mbaya. Kardinali aliweza kuendelea na safari yake kwa ulinzi wa Askari Polisi.
Anasema, kumekuwepo na mashambulizi ya mara kwa mara kwa raia na mali zao, changamoto kwa vikosi vya ulinzi na usalama kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika jamii. Serikali inapaswa kuhakikisha usalama wa raia na mali za ona kwamba, ulinzi na usalama wa nchi ni dhamana ya wananchi wote wa Nigeria.  Askari Polisi wapewe vifaa na rasilimali ya kutosha, lakini pia raia wema wasaidie mchakato wa ulinzi na usalama.
Mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu, bado: ulinzi, usalama umoja na mshikamano wa kitaifa haujapewa kipaumbele cha kutosha. Kuna haja kwa Serikali na wadau mbali mbali nchini Nigeria kusima kidete kupambana kufa na kupona na umaskini wa hali na kipato kwa kutumia vyema rasilimali ya nchi. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana ni changamoto kubwa inayopaswa kuvaliwa njuga kwani ni kutokana na umaskini, vijana hawa wanatumiwa na wanasiasa ucharwa kufanya vitendo vya kigaidi na kihalifu kama kinavyofanya Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, huko Kaskazini mwa Nigeria.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.


Chapisha Maoni

 
Top