0

SOMO 
1 Zek. 12 :10-11

Bwana asema: Nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Werusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza. Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIK ATI 
Zab. 63:1-5,7-8 (K) 1

(K) Ee Mungu. Mungu. wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu.

Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, 
Nafsi yangu inakuonea kiu,
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji. (K)

Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai;
Midomo yangu itakusifu. (K)

Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai;
Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono; 
Kinvwa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha. (K)

Maana Wewe umekuwa msaada wangu,
Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
Nafsi yangu inakuandama sana;
Mkono wako wa kuume unanitegemeza. (K)


SOMO 2 
Gal. 3 :26-29

Ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa vala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


SHANG1LIO 
Yn. 6:63,68

Aleluya, aleluya, 
Bwana, maneno yako ni roho tena ni uzima; Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. 
Aleluya. 

INJILI 
Lk. 9 : 18-24

Yesu alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? Wakamjibu wakisema, Yohane Mbatizaji; lakini wengine, Eliya; na wengine kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu. Akawaonya, aka- wakataza wasimwambie mtu neno hilo.
Akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.
Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.

Jumapili, Juni, 19, 2016. 
Dominika ya 12 ya Mwaka C wa Kanisa.


Zek 12: 10-11, 13:1; 
Zab 63: 2-6, 8-9; 
Gal 3: 26-29; 
Lk 9: 18-24.


KUCHUKUWA MISALABA YETU!

Leo somo la kwanza linalotoka katika kitabu cha Nabii Zakaria, linaongelea kuhusu kosa ambalo kila mmoja wa Yerusalemu alikuwa anahusika. Zakaria anatabiri anasema kwa kifo cha huyo mtu asiye na hatia, kijito cha maji kitatiririka kwa manufaa ya watu wote, na wote wakaojiosha katika maji hayo watasafishwa na uovu wao au dhambi yao. Yohane katika Injili yake, anaonesha unabii huu wa Zakaria ukitimia mara baada ya askari mmoja kumchoma Yesu ubavuni kwa mkuki (Yn 19: 37). Leo Kanisa limeamua kuchukua ujumbe huu wa Zakaria kama utambulisho unao tangulia ujumbe wa Yesu katika Injili ambapo Yesu hatangazi tuu mateso na kifo chake bali pia kushiriki kwetu ndani yake.

Somo la pili linalotoka katika barua ya mtume Paulo kwa Wagalatia, Paulo anasisitiza kwamba kinacho okoa ni Imani juu ya Yesu mfufuka na upendo kwa jirani. Hakuna kingine kinachohitajika na hamna kingine kinacho weza kuokoa. Anatuambia kwamba kwa ubatizo Kristo ametufanya wana wa Mungu kwakuvunja vikwazo vya zamani ambavyo mwanadamu alikuwa amejiwekea zamani nakujikweza navyo kila wakati. Katika Ekaristi takatifu Jumapili ya leo ni muda muafaka wakuvunja vikwazo tulivyojiwekea wenyewe ndani yetu au katika jumuiya zetu kwa wiki hii iliopita.

Somo ambalo Injili ya leo inatoa nikwamba: mfuasi wa kweli wa Yesu, kama anajali Ufalme wa milele ni lazima awe tayari kubeba msalaba wake, na hata ikimlazimu awe tayari kupigiliwa misumari juu yake, kama Yesu mwenyewe. Sisi ni Wakristo kwasababu kwa uaminifu tunataka kuurithi ufalme wa milele ambao Yesu alikuja duniani kuutangaza. Alipita katika njia ya mateso na kifo msalabani, kifo cha aibu na mateso makubwa kabisa. Alifanya hivyo ili sisi tuurithi ufalme wa Mbinguni. Yeye ni mwana wa Mungu. Hakuwa na dhambi au hatia yeyote iliyompasa afe kwaajili hiyo. Mateso yake yote ilikuwa ni kwaajili yetu. 

Inatuwia vigumu, kwamba, tunapaswa kumuiga yeye kwaajili ya faida yetu na kwa jinsi Mungu anavyotaka kutoka kwetu, kwa kubeba misalaba yetu. Kwa kipindi cha karne ya 19 hivi, katika Historia ya Kanisa, tunaona kulikuwa na wanaume na wanawake walikufa mashahidi kwa kuteswa na kuuwawa kuliko kulikana jina la Yesu na kupoteza ufalme wao wa milele. Tunawapongeza kabisa na kuwaheshimu. Kati yetu tunajisikia kabisa ingekuwa mimi pengine ingekuwa vigumu sana kukabiliana na jaribu hili kubwa la Imani yetu. Lakini Mungu huwa anaona, wakati anatuma msalaba mkubwa, pia anayapa pia mabega yako nguvu uweze kuubeba. 
Tunacho itiwa wengi wetu leo na kinachotarajiwa kutoka kwetu, ni kuchukuliana misalaba yetu kwa furaha na upendo. Tukichukuliana na kuvumiliana katika hali zetu za maisha, kuchukuliana katika ndoa, kumvumilia mume/mke unayeona pengine anakutesa, wakati mwingine kukaa kimya pale unapoona nikiongea nitaharibu Amani, hii ndio maana halisi ya kuwa shahidi polepole kwa nyakati zetu. Kuwasamehe waliotukosea nakutokutaka kurudisha kisasi ni msalaba mkubwa. Wengi wetu tunataka wale wote waliotukosea wapate matatizo, wakisitawi tunachanganyikiwa na tunatamani turudishe kisasi! Kusamehe nakuachilia yote ni msalaba pia, beba, ndio kufa shahidi, usitafute jinsi ya kumdhuru. Kumuachia Mungu na kusamehe badala ya kubaki kulalamika na kunungunika kila mara ni aina nyingine ya kufa shahidi ndani ya Kristo. 

Katika maisha ya wakfu (utawa au Upadre) tofauti na ndoa, maisha yenyewe ni aina ya kukataa na kuachilia yale yote ambayo pengine ulimwengu unaona ni ya thamani sana na kwamba wanadhani mwanadamu aliyekamilika hawezi kuishi bila kuwa nayo. Pengine kwa kuchagua maisha hayo, ulipata upinzani kutoka kwa ndugu au jamaa au marafiki pengine na wengine wengi hawakukuelewa na hawaelewi kwanini wewe na uzuri au afya njema umechagua maisha hayo. Ni msukumo wa Yesu unaosukuma roho zetu na muitikio wake wakuitika ujumbe wake wa Injili wa kutaka kumfuata bila kujibakiza. Katika kumfuata yeye kunahitaji majitoleo ya kweli ikiwemo ni pamoja nakubeba msalaba wetu. Watu na ulimwengu wanaweza wasikuelewe lakini yule anayeita (Kristo) atatupatia furaha na tumaini linalopatikana katika kuhubiri neno lake na kuishi maisha ya wakfu.

 “Wakati tunasafiri bila msalaba, wakati tunajenga bila msalaba, wakati tunamuungama Kristo bila msalaba, sisi sio wafuasi wa Kristo ni wafuasi wa ulimwengu” Baba Mtakatifu Fransisko. 

Sala: Aasante Mungu, kwa zawadi ya Imani. Asante Yesu kwakufanya ufalme wa milele uwepo kwaajili yangu, na kunionesha jinsi ya kuupata. Nakuomba unipe neema na nguvu kwakuonesha kwamba nastahili wito wako wa mbinguni kwa kubeba misalaba yangu kila siku ninayokutana nayo. Amina.

Chapisha Maoni

 
Top