Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni moja ya ibada zinazojulikana
sana katika Kanisa Katoliki. Ibada hii inauona Moyo wa Kibinadamu wa Yesu kama
mwakilishi wa Mapendo yake ya Kimungu kwa wanadamu, na Kanisa nayo
inaiona kama Mapendo na Huruma ya Yesu kwa wanadamu wote.
Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu imefikia hatua hii
tunayoishuhudia leo kutokana na maelekezo ya Mtakatifu Margareta Maria Alakok
aliyejifunza uendelezaji wake wakati alipokuwa anatokewa na Yesu kwa
mfululizo
kati ya mwaka 1673 na mwaka 1675.
Mtawa mwingine tena, Mwenyeheri Maria wa Moyo Mtakatifu
(1863-1899), kutoka Chama cha Kitawa cha Mchungaji Mwema huko Ujerumani,
aliisisimkia sana ibada hii baada ya kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Yesu
na akawahi hata kumwomba Papa Leo XIII, autolee ulimwengu wote kwa Moyo
Mtakatifu wa Yesu kama alivyotumwa na Yesu.
Wakati wa kipindi cha enzi ya kati, watangulizi wa ibada hii
mpya, walijitokeza kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu wa Kanisa Katoliki na
kuifanya ishike kasi na kujulikana sana katika Kanisa hilo.
Asili ya Ibada: Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni maendelezo ya Ibada ya
‘Ubinadamu Mtakatifu wa Kristo.’ Uhuishaji wa maisha ya Kitawa na ari ya
Mtakatifu Bernard wa Klervo na ya Mtakatifu Fransisko wa Asizi katika Karne ya
12 na 13, pamoja na shauku ya wapiganaji wa vita vya Msalaba waliorudi kutoka
Nchi Takatifu, walianzisha Ibada ya Mateso ya Kristo hasa ya Vidonda vyake
Vitakatifu na zaidi sana lile donda la Ubavuni mwa Yesu.
Ibada hii ya Mateso ya Kristo ilishughulikiwa zaidi na vikundi
vya Kitawa vya Wafransiskani ikishabikiwa sana na Mtakatifu Bonaventura pamoja
na Mtakatifu Jean Eudes (1602 -1680). Kwa asili, kulikuwa na
ibada mbili zilizoungana, ibada ya Moyo Safi wa Maria, na nyingine ya Moyo wa
Yesu. Lakini polepole, ibada hizi mbili zilitenganishwa na tarehe 31 Agosti,
1670 kwa mara ya kwanza kabisa kulikuwa na sherehe ya pekee ya Moyo Makatifu wa
Yesu katika shule ya Seminari ya Rennes huko Ufaransa.
Watakatifu wanaohusiana na Moyo Mtakatifu wa Yesu:
Mtakatifu Lutgarda (1246): Vyanzo vya kihistoria ya Kanisa, vinasema kuwa Yesu
alimtokea Lutgarda na akamwambia amwombe neema yoyote aitakayo. Yeye akaomba
uelewa wa lugha ya Kilatini ili asaidiwe katika kuyaelewa maandiko.Akapewa,
lakini aliona bado anakosa kitu. Akamwomba Yesu wabadilishane mioyo. Yesu
akakubali na kuanzia hapo Lutgarda alikuwa na ibada ya pekee kwa
Moto Mtakatifu wa Yesu.
Mtakatifu Mektildis Mkubwa (1298): Yesu alimtokea na akamwamuru Mektildis
ampende na aupende moyo wake katika Sakramenti ya altare; naye akafanya kama
Yesu alinyokuwa amemwamuru. Mtakatifu huyu alikuwa kati ya wale wa kwanza
kabisa kuwa na ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Mtakatifu Margareta Maria Alakok (1647-1690): Kama ilivyokwisha kudokezwa Margareta
Maria Alakok ndiye aliyekuwa mwelekezi wa ibada hii na kuifanya kama ilivyo
sasa. Maelekezo kuhusu upokeaji wa Komunyo, Ibada ya Ijumaa ya kwanza ya mwezi
, kuabudu Ekaristi Takatifu kwa saa moja kila siku ya Alhamisi, na kusherehekea
sikukuu ya Moyo Mtakatifu yalikuwa baadhi ya maelekezo ya Margarata Maria
Alakok.
Estelle Faquette: Alipewa Skapulari ya Moyo Mtakatifu wa Yesu tarehe 9/9/1876 na
Mama Bikira Maria na akaruhusiwa na Askofu wake Mkuu kutengeneza nyingi zaidi na
kuwagawia waamini wengine ilipofika tarehe 12/12/1876.
Mwenyeheri Maria wa Moyo Mtakatifu (1863-1899): Tarehe 10/6/1898 Maria alipewa ujumbe na
Yesu wa kumpelekea Papa Leo X111 kumwambia autolee ulimwengu wote kwa Moyo
Mtakatifu wa Yesu. Kwa kuwa Papa hakuutilia maanani
ujumbe ule wala hakuuamini, tarehe 6/1/1889 alipelekewa ujumbe mwingine tena wa
kumwambia kuwa Ijumaa za Kwanza za kila mwezi ziwe kwa ajili ya Ibada ya Moyo
Mtakatifu wa Yesu. Tarehe 9/6/1899 Papa Leo akatekeleza maagizo ya
kuutolea ulimwengu wote kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Kibali cha Kipapa: Baada ya kifo cha Margareta Maria Alakok, mashirika ya Kitawa tu
ndiyo yaliyoruhusiwa na Roma kuadhimisha misa maalum kwa heshima ya Moyo
Mtakatifu wa Yesu. Lakini kuanzia mwaka 1856, Papa Pius 1X aliiruhusu Kanisa
Katoliki kwa jumla kuadhimisha misa maalum kwa heshima ya Moyo Mtakatifu wa
Yesu.
Papa Pius X aliamuru ile ibada ya kuutolea ulimwengu kwa Moyo
Mtakatifu wa Yesu iliyofanywa kwanza na Papa Leo X111 irudiwe kila mwaka. Papa
Pius X1, katika Waraka wake wa Kipapa wa tarehe 8 Mei, 1928 akiri kuwa ni kweli
Yesu alikuwa amejidhihirisha mwenyewe alipomtokea Margareta Maria Alakok na
kutoa ahadi za neema kwa wale watakaouheshimu moyo wake. Waraka wa Papa ulikuwa
unarudia tena na tena yale mazungumzo kati ya Yesu na Mtakatifu Margareta
yakithibitisha umhimu wa kuuheshimu Moyo huo wa Yesu kwa fidia ya dhambi zetu.
Siku ya kumbukumbu ya miaka 100 ya kuanzishwa kwa sherehe ya
Moyo Mtakatifu wa Yesu iliyozinduliwa na Papa Pius IX, Papa Pius X11 aliwaeleza
Wakatoliki wote kwa kinaganaga sana kuhusu ibada hii katika Waraka wake wa
Kipapa wa tarehe 15 Mei, 1956.
Ukosoaji kuhusu utoaji heshima kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu: Wakristo wa madhehebu ya Kiorthodoksi ya
Mashariki wanaikosoa ibada hii wakisema kuwa imeuweka mno Moyo wa Yesu
isivyostahili katika hali ya ubinadamu. Papa Pius X11 katika moja ya Barua zake
aliujibu ukosoaji huo kwamba Moyo Mtakatifu wa Yesu unaheshimiwa kwa mujibu wa
Nafsi Takatifu ya Neno la kudumu milele na pia kama alama ya mapendo yake
inayoonekana ambayo ni ushahidi wa wokovu wetu.
Na Philip Komba
0754 054 004 kwa msaada wa mtandao.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni