0
MASOMO YA MISA, JUNI 5, 2016
SOMO 1
1 Fal. 17:17-24
Mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, aliugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena. Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu je! Umenijulia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu. Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake. Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka. Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka orofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai. Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu; nay a kuwa neno la Bwana kinywani mwako ni kweli.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 30:1, 3-5, 10-12 (K)


(K) Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua.
Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
Umeniinua nafsi yangu,
Ee Bwana, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa
Miongoni mwao washukao shimoni. (K)
Mwimbieni Bwana zaburi,
Enyi watauwa wake.
Na kufanya shukrani.
Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
Katika radhi yake mna uhai.
Huenda kilio huja kukaa usiku, 
Lakini asubuhi huwa furaha. (K)
Ee Bwana, usikie, unirehemu,
Bwana, uwe msaidizi wangu.
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
Ee Bwana, Mungu wangu,
Nitakushukuru milele. (K)
SOMO 2
Gal. 1: 11-19
Ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo. Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Name naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kasha nikarudi tena Dameski. Kasha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO
1 Sam. 3:9; Yn. 6:68
Aleluya, aleluya!
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia; Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.

INJILI
Lk. 7:11-17
Yesu alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipokaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
[6/4, 15:08] +255 755 444 471: “MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, Juni, 5, 2016. 
Jumapili ya 10 ya mwaka C wa Kanisa.
1 Fal 17: 17-24; 
Zab 29: 2, 4-6, 11-13; 
Gal 1: 11-19; 
Lk 7: 11-17
NIMEKUJA ILI WAWE NA UZIMA!
Liturujia ya leo inasisitiza kuhusu Mungu na mwanae Yesu, kama chanzo cha uzima na maisha yote. Katika somo la kwanza tunaona Eliya kwa njia ya sala huko Serapta, alirudisha tena uhai wa mtoto wa mama mjane. Katika Injili pia tunamuona Yesu anamrudishia uhai mtoto wa mjane wa Naimu.
Ndani ya ujumbe inaonesha huzuni, hasa kwa mwanamke ambaye tayari ameshampoteza mumewe (Mjane). Kumpoteza tena mtoto ni kitu ambacho kitamfanya ajione kama mtu asiye na thamani ndani ya jamii. Yesu kwa tukio hili anamuonea huruma kwa yaliompata. Yesu (Luka anamuonesha Yesu kama “Bwana”, kwa mara ya kwanza kichwa cha habari kinakuwa kwaajili ya Mungu pekee) akisogelea mwili wa aliyekufa, anawaambia waliombeba wasimame na mara anaamuru yule kijana anyanyuke. Neno “kunyanyuka” neno linalo onesha ufufuko, “nimekuja ili wawe na uzima”.
Muonekano wawatu ulionekana walipatwa na mshangao mkubwa na heshima kuu. “ Nabii mkuu ametokea kwetu na Mungu amekuja kati ya watu wake”. Hawakuwa na wasiwasi ya juu asili ya kile walichoona kikitendeka pale; ilikuwa ni kazi ya Mungu. Haikuwa hadithi yakushangaza waliosikia bali ilikuwa ukweli walioona kwa macho yao wenyewe. Habari hii ilienea kama moto unaochoma msitu, kwanzia Yudea na mipaka yake. Kwa kumuita Yesu Nabii, pengine watu walikuwa wakimfikiria nabii mwingine mkubwa, Eliya, ambaye pia alimfufua kijana wa mjane alikuwa na huzuni nyingi.
Lakini Eliya ni tofauti na Yesu. Eliya anasali kwa Mungu kwakupitia mila na sala za Wayahudi ilikurudisha tena uhai wa kijana yule. Yesu yeye hajasali kwa yeyote, yeye aliamuru kwani ni Mwana wa Mungu mwenye mamlaka. Yesu anaongea maneno ya faraja kwa yule mawanamke na kisha anatoa amri yule kijana anyanyuke. Eliya ni Nabii wa Bwana; Yesu ni Bwana, yeye ni ufufuo na uzima.
Wengi wetu tumekufa. Kama lile kundi walivyokuwa wakibeba ile maiti wakizungunga mijini, sisi nasi tunatembea huku tukiukimbia ufalme wa Mungu. Lakini Yesu kwakutupenda, analeta ufalme wa Mungu kati yetu. Anatembea akitufuata sisi, akitugusa nakutuleta tena kwenye uzima wa milele. Mt. Ireneous mara nyingi hukotiwa; “Utukufu wa Mungu ni mtu anayeishi kikamilifu”. Pengine tujitafakari leo kidogo ni kwa jinsi ghani mimi naishi kikamilifu katika maisha yangu? Yesu ametuahidia kutupa Uzima, tena uzima tele. Upo tele, kazi yetu ni kushirikiana na neema ya Mungu ili tuweze kuupata uzima huu. Mwaka huu wa huruma ya Mungu ni nafasi kwetu kujikabidhi kwenye huruma ya Mungu na kukumbatia huruma yake.
Katika somo la pili tunamuona, Mt. Paulo akikiri pia uwezo wa nguvu ya Yesu, kwamba uwezo na nguvu ya Injili anayoihubiri haitokani na nguvu za kibinadamu. Paulo anakiri nguvu ya Yesu yenye uwezo wote wakuweza kubadili hata kile ambacho kwa akili ya kibinadamu, tunadhani kwamba hakiwezekani. Nguvu ya Yesu imeshinda mauti, kifo hakina uwezo tena katika miili yetu, kifo sasa kwetu ni njia yakupitia kuelekea ushindi aliyotutayarishia Kristo mwenyewe. Nguvu ya Yesu inauwezo wakufufua miili yetu iliyokufa kwasababu ya dhambi zetu, kufufua tena ile neema tuliopokea wakati wa ubatizo. Mt. Paulo anakiri nguvu hii ya Yesu kwa ujasiri kabisa kwasababu anatambua Yesu mwenyewe alimfufua kutoka katika hali yake ya uasi, na utesaji wa watu wa kanisa lake na kumfanya kiumbe kipya, chombo cha Injili yake. Je, wewe una dhambi ambayo unadhani huwezi kusamehewa na Mungu? Pengine ujiulize dhambi yako ni kubwa kuliko aliotenda Paulo kabla ya wongofu wake? Ni dhambi ghani ambayo unadhani Mungu hatakusamehe? Tulegeze mioyo yetu, kwa unyenyekevu, tumjongee Yesu katika sakramenti ya kitubio atufufue tena atupe neema tuweze kumsifu tena na kukiri nguvu ya neno lake katika maisha yetu.
Sala: Bwana, naomba nifufuke katika hali zangu zote za giza za maisha yangu ili niweze kupata neema na furaha za uzima wa milele. Amina

From Maurice Nyambane


Pakua nyimbo hapa

http://www.swahilimusicnotes.com/nyimbozajumapilinasikukuu/ratiba/jumapili-ya-10-mwaka-c/27

Chapisha Maoni

 
Top