0
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano, tarehe 29 Juni 2016 amesema, Mama Kanisa anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa mahubiri na ushuhuda wa Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, msingi wa imani ya Kikristo na mwanga angavu kwa Kanisa zima. Yesu aliwatuma mitume wake wawili wawili ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama ilivyo kwa watakatifu Petro na Paulo, wanaotofautiana kwa mambo mengi.



Mtakatifu Petro alikuwa ni mvuvi wa kawaida kabisa; Paulo Mtume alikuwa ni mwalimu na msomi; mashuhuda na vyombo vya imani, waliojitosa kimasomaso kumtangaza na kumshuhudia Kristo hadi miisho ya dunia. Leo hii kama imani kwa Kristo Yesu inafahamika mjini Roma na kuwa ni sehemu ya msingi wa amana ya maisha ya kiroho na utamaduni wa watu ni matunda ya ujasiri wa mitume hawa waliotoka huko Mashariki.
Hawa ni watu ambao waliacha yote na kuambata upendo wa Kristo, licha ya matatizo na changamoto zote walizokabiliana nazo njiani, kiasi hata cha kutua nanga ya matumaini mjini Roma. Hawakujibakiza hata kidogo, wakajimwaga kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kati ya watu wa mataifa, na hatimaye wakayamimina maisha yao kama mhuri wa kufunga utume wao wa imani na upendo. Watakatifu hawa leo bado wanaendelea kuwatembelea waamini na watu wote wenye mapenzi mema wa mji wa Roma, wanabisha hodi katika milango, lakini zaidi katika malango ya nyoyo za watu, ili kuwaonesha uwepo wa Kristo Yesu katika maisha yao!
Watakatifu hawa wanataka kuwaonjesha na kuwashirikisha upendo wake wenye huruma; faraja na amani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kupokea ujumbe wao na kuambata amana na utajiri unaofumbatwa kutokana na ushuhuda wa maisha yao. Mtakatifu Petro anaonesha imani thabiti na Paulo, mtume ni shuhuda wa moyo mkuu; mambo yanayowasaidia Wakristto kuwa ni watu wenye furaha, waaminifu kwa Injili ya Kristo na wazi katika mchakato wa utamaduni wa kukutana na watu!
Baba Mtakatifu anasema wakati wa Ibada ya Misa Takatifu amebariki Pallio takatifu 25 kwa Maaskofu wakuu wapya walioteuliwa katika kipindi cha mwaka 2015- 2016 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anawatakia kheri na baraka ndugu, jamaa na wale wote waliosindikizana na Maaskofu hawa wakuu katika Ibada ya Misa Takatifu. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime, ari na moyo mkuu ili waendelee kutekeleza dhamana na wajibu wao wa huduma kwa Injili, huku wakifumbata umoja wa Kanisa zima, lakini zaidi na Khalifa wa Mtakatifu Petro kama ushuhuda wa Pallio Takatifu.
Baba Mtakatifu anatambua uwepo wa Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kielelezo cha udugu kati ya Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki, mwaliko ni kuendelea kusali ili kuweza kuimarisha vifungo vya umoja na ushuhuda wa pamoja. Baba Mtakatifu anawaweka waamini wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria afya ya Warumi, ili waweze daima kutafuta na kuambata tunu msingi za maisha ya kiroho na kimaadili, nguzo madhubuti kwa maisha ya kijamii na utume wake nchini Italia, Ulaya na Ulimwenguni kote!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

Chapisha Maoni

 
Top