Katika Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, tarehe 29 Juni 2016, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kubariki Pallio takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 25 na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi zao kwa wakati muafaka. Kutoka Kanisa Barani Afrika, ni Askofu mkuu mteule Roger Houngbedgi wa Jimbo kuu la Cotonou nchini Benin.
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amejikita zaidi katika alama ya ufunguo ambao Kristo Yesu alimkabidhi Mtakatifu Petro ili aweze kuwafungulia watu mlango wa Ufalme wa mbinguni na wala si kuufunga mbele ya watu wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kama walivyokuwa wanafanya Waandishi na Mafarisayo, ambao walikemewa na Yesu mwenyewe.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika Liturujia ya Neno la Mungu mambo makuu matatu yanatiliwa mkazo wa pekee: kufungua: Petro anafunguliwa kutoka gerezani; inaonesha jinsi Jumuiya ya Kikristo ilivyokuwa ikisali na mwishowe jinsi ambavyo Mtakatifu Petro alivyobisha hodi na kufunguliwa mlango kwenye nyumba ya Mama yake Yohane aliyejulikana kama Marko, baada kufunguliwa kutoka gerezani.
Baba Mtakatifu anasema, sala ni njia kuu inayopaswa kutumiwa na Jumuiya ya waamini badala ya kujifungia ndani mwake kwa kuogopa dhuluma, nyanyaso na wasi wasi wa maisha; hii ni njia iliyokuwa wazi kwa Mtakatifu Petro ambaye mara tu baada kukabidhiwa utume wake anajikuta akitupwa gerezani na Mfalme Herode na kwamba, hapa adhabu ya kifo ilikuwa mbele ya macho yake. Lakini wakati wote alipokuwa gerezani, Jumuiya ya waamini ilisali kwa nguvu na Mwenyezi Mungu akasikiliza sala yao na kumtuma Malaika wake ili kumwokoa Mtakatifu Petro kutoka katika mkono wa Herode. Sala ni hali ya kujiaminisha mbele ya Mungu na njia ya kujiondoa katika hali na tabia ya jumuiya na waamini binafsi kujifungia katika undani mwao!
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hata Mtakatifu Paulo anapomwandikia Mtume Timoteo juu ya uzoefu na mang’amuzi yake ya kuachiliwa huru baada ya kuwa amekuhukumiwa adhabu ya kifo, kwani Kristo Yesu alikuwa karibu yake kiasi cha kumwezesha kutekeleza dhamana ya Uinjilishaji kati ya watu wa mataifa. Lakini hapa Mtakatifu Paulo anajikita zaidi katika kufunguliwa ili kuelekea katika maisha ya uzima wa milele baada ya kumaliza mashindano ya hapa duniani na kwamba, anamshukuru Mungu kwa kuweza kutangaza na kushuhudia Injili yake kwa watu wa mataifa sasa anataka kujiachilia mikononi mwa Kristo Yesu, ili aweze kufurahia maisha ya uzima wa milele huko mbinguni.
Baba Mtakatifu akirejea tena kwa Mtakatifu Petro anasema, imani yake kwa Kristo Yesu ni chanzo cha dhamana na utume ambao alikabidhiwa. Maisha ya Petro mtume, kama yalivyo maisha kwa kila mtu yanapata mwelekeo mpya pale yanapokea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya imani. Hapa Mtakatifu Petro anajikuta akiwa njiani katika mchakato wa kutoka katika undani mwake, ili kuachia usalama wa kibinadamu, lakini zaidi kung’oa kiburi kilichochanganyika na ushupavu na ukarimu kwa jirani. Hapa sala kutoka kwa Yesu ndiyo iliyokuwa kinga yake kuu, ili asitindikiwe imani na kwa imani hii aweze kuwaimarisha ndugu zake.
Yesu alimwangalia Petro kwa jicho la upendo na huruma, baada ya kuwa amemkana mara tatu, anapogundua hili, machozi ya toba yanabubujika. Hapa Simoni Petro anafunguliwa kutoka katika kifungo chake cha kiburi na woga na kuvuka kishawishi cha kujifungia katika ubinafsi wake, tayari kubeba Msalaba na kuanza kumfuasa Yesu katika Njia ya Msalaba.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Petro alipofunguliwa kutoka gerezani alikwenda moja kwa moja kwenye nyumba ya Mama yake Yohane, aliyejulikana kama Marko, ambako bado walikuwa na wasi wasi kuhusu madhulumu waliyokuwa wanafanyiwa Wakristo wakati ule, kiasi hata cha kujifungia ndani. Hiki ni kishawishi cha Kanisa kutaka kujifungia ndani mwake pale linapokabiliana na hatari, lakini sala ni njia pekee inayoweza kulikwamua Kanisa katika hali kama hii anasema Baba Mtakatifu Francisko.
Hapa kuna haja kwa Kanisa kushikamana katika umoja badala ya kuendekeza utengano na migawanyiko ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa ujumbe wa kiekumene kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza unaoshiriki katika maadhimisho haya alama ya umoja wa Kanisa zima kama inavyooneshwa pia na Maaskofu wakuu wapya kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambao wamekabidhiwa Pallio Takatifu, kielelezo cha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Pallio hizi anasema Baba Mtakatifu watavishwa na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi husika kwa wakati muafaka! Mwishoni, anawaomba watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani waendelee kuliombea Kanisa ili liweze kutembea katika njia hii ya furaha na kupokea baraka za Mungu ili kuweza kumshuhudia kwa wote!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni