0


"ZAKA":
Zaka ni kiwango maalumu kawaida ni 10%, ambacho kila mmoja wetu, anapaswa kumtolea Mungu kutokana na mapato yake yote. Iwe ni pato la saa moja, siku moja, wiki moja, mwezi moja, au mwaka moja. Ni kiwango maalumu, 10%. Ni kama kodi.
Katika Agano la Kale, watu walikuwa hawaruhusiwi kuanza kutumia mapato yao yawe ya mashambani, ya wanyama, au fedha au dhahabu mpaka kwanza wametoa zaka.
Na katika Agano la Kale, zaka hiyo ilikuwa ni asilimia kumi. (10%). “Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wanaamri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani ndugu zao kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika viuno vya Ibrahimu.” (Ebr 7:5).
Hiyo asilimia kumi walikuwa wamepewa Walawi wale ambao baadaye walikuwa makuhani, au waliokuwa wafanyakazi katika hekalu, katika Hema ya Bwana. Zaka zilikuwa zikitolewa kwa ajili ya hawa Walawi.
Katika makabila 12 ya Waisraeli, 11 yalikuwa na urithi. Lakini hawa Walawi, urithi wao ulikuwa Bwana mwenyewe pamoja na zaka na sadaka. Kila muisraeli alilazimika kutoa asilimia 10 ya mapato yake yote na kupeleka kwa hawa Walawi.
Kwa vile zaka ni mali ya Bwana, kila mtu alilazimika kutoa zaka bila kukosa. Ikiwa mtu angeshindwa kulipa zaka kutokana na sababu yeyote ile, mtu yule alipaswa kuifidia zaka ile kwa kutoa kile kiwango cha asilimia kumi na juu yake angeongeza tena asilimia 5. (Walawi 27:31).
Zaka haikuwa kitu cha mchezo mchezo. Ilikuwa ni lazima. Mtu alikuwa na haki ya kutumia mali zake baada tu ya mtu huyo kutoa zaka, wala sio kabla ya hapo. Je, wewe unafanya hivyo? Hii inamaana hata sisi tusingeanza kutumia mishahara au mapato yetu mpaka kwanza tuwe tumetoa zaka. Hivyo ndivyo linavyoagiza Neno la Mungu.
SADAKA NI NINI?
Kuna sadaka za aina tatu;
1. Sadaka za shukrani: “Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru, mtimizie aliye juu nadhiri zako.” (Zab 50:14)
2. Sadaka za wahitaji: yaani masikini. (Mdo 3:1-3)
3. Sadaka za sifa: “Basi kwa ajili yake Yeye (Yesu) na tumpe Mungu dhabihu za sifa daima yaani tunda la midomo iiungamayo jina lake.” (Ebr 13:15)
Nini maana za sadaka ya sifa? ~Sadaka za sifa ni pale ambapo mtu unakabiliwa na mambo magumu, mambo ya kukatisha tamaa, lakini bado unaweza kumsifu Mungu.
Mfano ni ule wa yale yaliyomsibu Ayubu. Ayubu baada ya kufiwa na watoto wake wote na kupoteza mali zake zote, lakini bado alibaki akimsifu Mungu akisema; “Bwana ndiye aliyetoa, na yeye amechukuwa, jina la Bana libarikiwe.” (Ayu 1:21).
Mfano mwingine ni ule wa Paulo na Sila. Walikamatwa, walipigwa na walitiwa gerezani. Wakati wakiwa gerezani huku miili ikiwauma kutokana na mapigo, wakiwa wamekata tamaa kama vile Mungu wao hayupo, usiku walianza kumsifu Mungu. Waliimba na kumsifu Mungu huku wafungwa wengine wakiwashangaa kwani ilikuwa si kitu cha rahisi. “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wanamuomba Mungu na kumuimbia nyimbo za kumsifu na afungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.” (Mdo 16:25). Baadaye milango ya gereza ilifunguka, na aliachiwa.
Tafadhali tupe muda wako tukueleze zaidi juu yasadaka za Shukrani. Zab. 50:14.
KAZI YA ZAKA NA SADAKA NI NINI?
~Zaka na sadaka ni za muhimu sana kwani kupitia Zaka na Sadaka ndipo Habari Njema za ufalme wa Mungu zimetangazwa na kuendelezwa hapa duniani sawasawa na maagizo ya Bwana Yesu aliyotuagiza akisema, “Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Aaminiye na kubatizwa ataokoka. Asiye amini atahukumiwa.” (Mk 16:15-16).
Wengi wa waamini wanayo mawazo potofu na kusema si kazi yao ya kutoa zaka na sadaka bali ni kazi ya wazungu. Itikadi hiyo ni ya kizamani na imepitwa na wakati. Wengi wanaotoa zaka na sadaka kule ulaya ni wakulima na wafanyakazi wa kawaida kama wengi wetu tulivyo.
Lakini wamegundua kuwa mishahara yao na mali zao ni mali za Mungu. Wameamua kutoa zaka na sadaka hadi Injili ikatufikia. Mbali na kuifanya Injili ienee duniani, zaka na sadaka hutumika katika kulitegemeza kanisa kwa kuleta maendeleo ya kimwili na ya kiroho kwa watu. Kwa mantiki hiyo, ni lazima kutoa zaka na sadaka.
Kulingana na Mal. 3:8, wale wote wasiotoa zaka na sadaka ni wezi.
Wizi upo wa aina mbili. Wizi wa kwanza ni ule wa kuiba kidogokidogo, yaani kudokoadokoa. Mfano, kuna mtu kaweka gunia lake la mahindi sehemu fulani, na wewe unaenda kuiba kidogokidogo, leo debe, kesho kilo40, keshokutwa debe mbili hadi guia lote linaisha. Wizi wa aina ya pili ni ule wa kuiba jumla.
Mfano, mtu ameweka gunia lake la mahindi pale, na wewe unaenda kulibeba lote na kuondoka nalo. Hivyo basi, mtu akiwa anaiba kidogokidogo au jumla, ni mwizi tu, kwani wizi ni wizi tu.
Hata katika kumuibia Mungu tupo wezi wa aina mbili. Kuna wezi wanaomuibia Mungu kidogokidogo, yaani wanatoa zaka na sadaka kiduchu. Wenyewe wanaona inatosha bwana.
Mfano, mtu anazo shilingi elfu mbili, anachenji ili atoe shilingi mia na zilizobakiza mfukoni atazitumia kwa kunywea pombe mara atokapo kanisani. Kwa jinsi hiyo, wewe ni mwizi.
Mwingine hatoi kabisa huku akijipa moyo kwa kujidanganya kwa maneno mbalimbali pamoja na haya yafuatayo. Utasikia mtu akisema hivi; “Aah bwana wee, hata hii sadaka au zaka hii kidogo natoa kwa basi tu. Kwanza Paroko wetu ananikwaza sana. Pesa zetu tunazo mpa anasaidia ndugu zake. Kwanza ashukuru hata hiki kidogo ninachotoa.”
Ukweli ni kwamba kwa suala la kutoa sadaka na zaka si suala la paroko au padre fulani. Sio suala la hiari bali ni suala la lazima. Ni Mungu anayetaka wewe utoe zaka na sadaka. Anatutaka tutoe zaka na sadaka kwa sababu yeye ndiye aliyetupa vitu hivyo. Ni kwa sababu hiyo. Ametupa wanyama, mishahara, majumba, mali na vitu vingine vya thamani ili tumtolee zaka na sadaka. Hivyo, hatuna sababu yeyote ya msingi ya kutokutoa zaka na sadaka.
Mwingine utamsikia akisema “Aah bwana wee, mimi sitoi sadaka wala zaka. Kisa? Kwanza mshahara wangu ni mdogo. Hautoshi mimi na mke wangu wala na watoto wangu. Sasa nitatoaje zaka na sadaka?”
Ndugu,hebu tuyasikie maneno ya Mungu; “Aliye muaminifu katika lililo dogo sana, huwaminifu katika lililo kubwa pia. Na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.” (Lk 16:10). Mfano, ikiwa katika mshahara wako wa sasa wa shilingi 30,000/= unashindwa kutoa zaka ya Sh. 3,000/= kwa mwezi, Mungu gani atakayekupa wewe mshahara wa Sh. 500,000/= ili baadae umtolee zaka ya Sh. 50,000/= kwa kila mwezi, wakati wewe unashindwa kutoa Sh. 3,000/= katika mshahara wako wa Sh. 30,000/=?
Haiwezekani. Ndiyo maana Mungu amekudhibiti, huwezi kupata mshahara mkubwa. Na hupati ng’o.
Kazi ya zaka ni kufungua baraka za mbinguni. (Mal. 3:10) Milango ya mibaraka ya mbinguni inafunguliwa na zaka na sadaka tunazotoa. Kwa vile wewe hutoi zaka, huwezi kubarikiwa.
Hutapata mshahara mkubwa, hutapata pato la kutosha. Utabaki hapohapo ulipo, na kuendelea kulalamika tu kila siku. Maana wewe ni mchoyo.
Mfano, wazazi wanaweza kujua kwamba mtoto wao fulani atakapokuwa mkubwa hawezi kutunza fedha, hasa kutokana na matumizi ya fedha ndogondogo wanazompa mtoto wao. Mathalani, wamempa mtoto wao Sh. 2000/= kwa matumizi ya wiki, eti baada ya siku mbili anakuja na kulalamika kuwa ile hela imeisha.
Unampa hela nyingine na baada ya siku moja anakuja tena akilalamika tena. Hii inonyesha jinsi mtoto asivyoweza kutunza fedha, na hata akiwa mkubwa hali itakuwa ni hiyo hiyo, kwani atakuwa mbadhilifu.
Na Mungu ni hivyo hivyo. Kesha kujua wewe kutokana na mshahara wako wa Sh. 30,000/= ambao unaupata sasa hivi, na kushindwa kumtolea zaka na sadaka. Kesha kujua wewe ni mchoyo na anauhakika akikupa Sh. 1,000,000/= huwezi na hutakuwa tayari kutoa laki moja kama sehemu yako ya zaka kwa kila mwezi.
Kwa hivyo unabaki kama ulivyo. Kila siku njaa, kila siku tabu, kila siku madeni, kila siku malalamiko na kila siku kukosa amani. Sababu yenyewe mshahara mdogo. Hiyo ndiyo laana ya ufukara.
Ndugu, tusipotoa zaka na sadaka, tunapata laana, na laana yenyewe ni ufukara.
Mungu kwa kinywa cha nabii Hagai anatuambia; “Ninyi msiotoa zaka na sadaka, mtapanda mbegu nyingi, mtavuna kidogo. Mtakula lakini hamtashiba, mtakunywa lakini hamtajazwa na vinywaji. Mtajivika nguo lakini hamtapata joto, na yeye atakayepata mshahara atapata mshahara ili autie kwenye mfuko uliotobokatoboka.” (Hag 1:6)
Ndugu yangu, unalalamika mshahara hautoshi, au pato unalopata halitoshi, ndio! Unalalamika njaa, ndio! Unalalamika unapanda kwa wingi na kupata kidogo, ndio! Hiyo ni laana ya ufukara, kwa sababu hutaki kumtolea Mungu.
Tunamuibia Mungu zaka na sadaka. Neno la Mungu linasema hivyo.
Hivyo, kama bado hujafunguka kwa kumtolea Mungu zaka na sadaka kwa kujisingizia au kujibandikizia vijisababu visivyo vya msingi pamoja na kwamba pato lako ni kidogo.
Mungu hatokubariki zaidi ya hapo ulipo mpaka umeanza kuwa muaminifu. Maana kama katika Sh. 1,000/= unashindwa kumpa Sh. 100/= kwa kila mwezi, amini Mungu hatokupa 100,000/= kwa sababu anajua hutakuwa tayari kumtolea Sh. 10,000/= kwa kila mwezi. Mwenye akili timamu anajua ukweli huo.
Na wewe ndugu yangu unayesema, “mimi sitoi zaka na sadaka, ninatoa kidogo tu eti kwa sababu paroko ananikwaza, eti matumizi yake siyapendi sijui nini na nini”, hebu sikiziliza Mungu anavyokuambia sasa. “Msihukumu msije mkahukumiwa, kwakuwa hukumu ile muhukumuyo ndiyo mtakayo hukumiwa, na kipimo kile mpimiacho, ndicho, mtakacho pimiwa.” (Mt. 7:1-2).
Usiache kutoa zaka eti unakwazwa na matumizi ya paroko au padre fulani, la hasha. Neno lina sema usihukumu usije ukahukumiwa, pili, kipimo kile mpimiacho ndicho mtakachopimiwa. Ndiyo maana baraka, mapato katika nyumba yako yamepungua. Unahangaika, umekata tamaa maana kile unachopimia ndicho Mungu anachokupimia.
Yesu kama Mungu, kwa vile ilikuwa ni sehemu ya sheria, naye alitoa zaka na sadaka. Ikiwa huyu Yesu tunayemfuata, tayari ametoa zaka na sadaka, wewe ni nani ushindwe na hata ukatae kutoa zaka na sadaka? Yesu na mitume walitoa zaka na sadaka. (Mt 17:24-27).
Hivyo, narudia tena kwa kusema, tusipotoa zaka na sadaka, sisi ni wezi na tunapokea laana ya ufukara.
Ni matumaini yetu kwamba sasa umeelewa vizuri juu ya zaka na Sadaka.
Mungu awabariki.

TUMSIFU YESU KRISTO!


Chapisha Maoni

 
Top