0
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 tangu yalipofanyika mageuzi makubwa ndani ya Kanisa yatafanyika tarehe 31 Oktoba 2016 huko Lund, Uswiss katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni Liturujia itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Lund, Uswiss na baadaye kutakuwa na tukio la hadhara litakaloadhimishwa kwenye Uwanja wa michezo wa Malmo; tukio ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa na umati mkubwa zaidi.

Haya yamo kwenye tamko la pamoja kati ya Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 tangu yalipofanyika mageuzi makubwa ndani ya Kanisa. Maadhimisho haya ni mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene kati ya Waluteri na Wakatoliki, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Maadhimisho ya pamoja ya Miaka 500 kati ya Makanisa haya mawili ni wakati muafaka wa shukrani mwa Mwenyezi Mungu; ni kipindi cha toba na changamoto ya kujikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Lengo kuu ni kumshukuru Mungu kwa zawadi ya mageuzi makubwa ndani ya Kanisa na kuomba msamaha kutokana na utengano ulioneshwa na Wakristo wa Makanisa haya mawili. Kanisa kuu la Lund ni mahali ambapo maadhimisho ya Liturujia ya pamoja yatafanyika kwa kuzingatia Mwongozo wa Liturujia uliotolea na Makanisa haya mawili hivi karibuni unaojulikana kama “Sala ya Pamoja” inayobubujika kutoka katika Hati ya pamoja kati ya Wakatoliki na Waluteri ijulikanayo kama “Kutoka kwenye kinzani, kuelekea kwenye Umoja”.
Uwanja wa michezo wa Malmo ni mahali ambapo wawakilishi wa Makanisa haya mawili watatoa ushuhuda wa huduma inayotolewa kwa ushirikiano kati ya Kanisa la Kiinjili la Kiluteri na Kanisa Katoliki, hasa kwa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Makanisa yamekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; haki na amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Tamko hili linaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Askofu Dr. Munib A. Younan, Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani na Mheshimiwa Martin Junge, Katibu mkuu wa Shirikisho hili wataongoza “Sala ya Pamoja kwa kushirikiana pia na viongozi wa Makanisa ya Kiluteri pamoja na Jimbo Katoliki la Stockholm.
Viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri wanasema pale ambapo waamini wanajikita katika njia ya majadiliano, kinzani na mipasuko inafukuziwa mbali na hapo wanapata nguvu mpya. Waamini wa Makanisa haya wanahamasishwa kutoa huduma kwa walimwengu. Kumbe, maadhimisho haya ya pamoja ni kielelezo cha ushuhuda wa upendo na matumaini mintarafu neema ya Mungu. Kwa upande wake Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema kwa kujikita katika ufahamu wa Mungu wenye mwelekeo unaojikita kwa Kristo, waamini wa Makanisa haya wanaweza kuadhimisha Jubilei ya mageuzi makubwa ndani ya Kanisa huku wakiwa na mwelekeo wa kiekumene kwa kuzama katika imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.
Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani linasema kwamba, hili ni tukio kubwa la kihistoria linalotarajiwa kuwashirikisha zaidi ya watu elfu kumi. Maadhimisho haya kwenye Uwanja wa Michezo wa Malmo ni kielelezo cha mchakato wa kuwaondoa wakristo kutoka katika mawazo ya kinzani na migogoro na kuanza kutembea tena katika mwanga wa umoja na matumaini kwa ajili ya siku za usoni sanjari na huduma ya pamoja kwa walimwengu anasema Askofu mkuu Antje Jackelen wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Uswiss.
Kwa upande wake, Askofu Anders Arborelius wa Jimbo Katoliki la Stockholm nchini Uswiss anasema Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wakuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani watakapotembelea mjini wa Lund na Malmo watasaidia kuwatia moyo Wakristo wote kufuata njia inayouendea umoja wa Wakristo.
 Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Chapisha Maoni

 
Top