0

1. Katika kila kusanyiko la Dominika, ni Yesu mwenyewe anaongea na Waumini.
Vitabu mbalimbali vinavyounda Biblia ni matokeo ya kazi ya Karne kadhaa. Ilichukua miaka mingi, chini ya uongozi wa Mungu, masimulizi yaliyo katika Biblia kuandikwa na kuwa na vitabu vya Biblia kama tulivyonavyo leo hii. Kwa vizazi vingi, Biblia ilinakiliwa kwa mikono. Mungu aliwaongoza wale walionakili wafanye hivyo kwa umakini ili wasikosee au kupotosha maudhui yake.
Mambo yalikuwa rahisi kutokana na uvumbuzi wa Teknolojia ya Uchapishaji. Kwa wakati huu, Biblia imekwisha tafsiriwa kwa lugha nyingi, kadiri ya maongozi ya Mungu ili watu wengi zaidi waweze kuupata ujumbe unaokomboa wa Mungu.
Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa teknolojia hii ya kisasa hususani viwanda vya uchapishaji, Radio, Television, Tovuti na hata simu za mkononi ambavyo vimewezesha Neno la Mungu liwafikie mamilioni ya watu duniani kote.
Ikumbukwe kwamba vitabu mbalimbali vya Biblia, mara nyingi havikukusanywa pamoja katika kitabu kimoja kama ilivyo sasa. Ni Kanisa, likiongozwa na Roho Mtakatifu lilivileta pamoja vitabu mbalimbali ambavyo Mungu alivuvia viandikwe na kuviacha vingine ambavyo ingawa ni vizuri kwa vyenyewe, vilikuwa
kazi ya mikono ya wanadamu.
Kimsingi kuna tofauti baina ya Biblia na vitabu au maandishi mengine. Ukiangalia Biblia kama kitabu, hakuna tofauti na kitabu kingine pengine cha Uchumi au Jiografia. Lakini kila Neno la Mungu lisomwapo, msomaji huitimisha kusema: “Hilo ndilo Neno la Mungu” au “Hii ndiyo Injili ya Bwana,” nasi twaitikia “Tumshukuru Mungu” au “Sifa kwako Ee Kristo.”
Kiitikizano chetu ni uthibitisho kwamba kile kilichosomwa, nasi tukakisikia, siyo Neno la kawaida bali ni Neno la Mungu ambalo Mungu ameongea nasi kwa njia ya Nabii au Mtume au Mwinjili. Ni kuthibitisha kwamba ni ileile Injili iliyohubiriwa na Kristo miaka 2000 iliyopita huko Palestina.
Ni jambo la kushukuru kwamba Mungu anatujulisha leo ujumbe uleule uliowakomboa wengi hapo zamani, ni ujumbe huo huo unaotuongoza hata sisi leo katika njia ya Uzima. Kuna cha ziada hapa. Inagawa tumesikia Neno la Mungu likitangazwa kwa kinywa na sauti ya mwanadamu, katika uhalisia wake ni Yesu aliyetangaza mwenyewe kama alivyohubiri katika mji na vijiji vya Palestina wakati wa maisha yake hapa duniani.
Mmesikia Neno la Mungu katika sauti yangu, lakini amini usiamini mimi sikuwa zaidi ya KIPAZA SAUTI. Asiyeonekana kwangu na kwenu ndiye Kristo aliyeongea nanyi. Nisingethubutu kusema haya kwa niaba yangu. Mababa wa Kanisa katika Mtaguso Mkuu wa Vaticano II wanatuambia kwamba: Kristo yupo daima katika Kanisa lake kwa jinsi ya pekee katika maadhimisho ya kiliturujia
· Kristo yuko katika Neno lake, kwani ni yeye anaongea wakati Maandiko Matakatifu yanaposomwa Kanisani. 
Yupo kwenye sadaka ya Misa katika Nafsi ya Kasisi au Padre mwadhimishi. Padre ni Kristo mwingine.
· Yupo hasa chini ya maumbo ya Ekaristi. 
Yupo kwa nguvu yake katika Sakramenti ilikwamba mtu anapobatiza, ni Kristo mwenyewe anayebatiza
· Yupo tena Kanisa linaposali na kuimba zaburi kwa vile aliahidi “Walipo wawili au watatu kwa jina langu nami nipo pamoja katikati yao [Mt 18:20]
2. Neno la Mungu ni hai tena lina nguvu ya kutenda sawasawa na lilipozungumzwa kwa mara ya kwanza.
Wafu hawaongei, ninapoongea hapa, maneno yangu kwa namna fulani, yanabeba sehemu ya maisha yangu, yaani pumzi yangu. Hata hivyo neno langu halina nguvu fulani juu yangu. Mtumishi anaweza kutii amri yangu, lakini vitu vilivyoumbwa kama upepo, maji na kadhalika, haviiti sauti yangu.
Tofauti kabisa ni kwamba kama tulivyosikia katika somo la pili, waraka kwa Waebrania, Neno la Mungu lina nguvu, tena ni hai. Maana yake ni kwamba, Neno hilo linasababisha vitu kuwepo: LINAUMBA. Ndiyo kusema kile kinachotamkwa kinatokea. Tuangalie baadhi ya mifano katika Biblia:
· Siku moja Mungu alisema, Nchi na itoe majani, iwe nuru, ikawa nuru, na liwe anga katikati ya maji, likatenge maji na maji, nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, ndege na wanyama, navyo vikatokea, akaona yote ni mema, ikawa asubuhi, ikawa jioni …[simulizi la uhulushi (Mwa 1:1ff)
· Katika nafasi fulani Yesu alimwambia Mkoma TAKASIKA [Mk 1:41], na alipokuwa akiongea alama za ukoma zilifutika mwilini mwa mkoma.
· Katika nafasi nyingine Yesu aliongea na Msichana aliyekufa “Msichana nakuambia inuka” na mara msichana akawa hai tena, akainuka akaenda zake [Mk 5:41-42]
· Katika Karamu ya mwisho, Bwana Yesu alichukua Mkate na Divai akisema “Huu ndio MWILI wangu” na “Hii ndiyo DAMU yangu” akawapa Mitume wake, wale na wanywe. Walichokula Mitume siyo mkate na kunywa divai, bali ni MWILI na DAMU ya Kristo. Tena akawaamuru wafanye hivyo daima kwa kumkumbuka yeye [Mk 14: 22, 24].
Nguvu hii ya Neno la Mungu siyo jambo la zamani, pasipo kuonekana machoni petu Neno la Mungu linaendelea kutenda miujiza katika siku hizi zetu.
· Mtu anapobatizwa kwa Jina la Baba na la Mwana na Roho Mtakatifu, anapokea kweli maisha ya uzima wa kiroho na anafanyika kwa ndani kabisa kuwa Mwana wa Mungu na mrithi wa Uzima wa Milele pamoja na Kristo.
· Katika sakramenti ya Upatanisho Padre anapotamka “Nami nakuondolea dhambi zako, kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, dhambi za mhusika zinaondolewa, msamaha unapatikana na maisha ya utakaso yanaanza mara.
· Tunapoadhimisha Ekaristi Takatifu, Padre anarudia maneno yaleyale ya Yesu “Huu ndio Mwili wangu na Hii ndiyo Damu yangu.” Kwa maneno haya Mkate na Divai hugeuka kuwa Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Padre anahuisha ile sadaka ya Msalaba. Mikono ya Padre ni kama tumbo la Bikira Maria kwani anamzaa Kristo altareni na kumkabidhi kwa waumini.
· Sakramenti nyinginezo kadhalika zinafanyika na kuhuishwa kwa Njia ya Neno la Mungu.
Leo hii, Neno la Mungu ni Hai, tena lina Nguvu. Ni Mungu peke yake anayefahamu ni mamilioni mangapi ya watu wanaomwongokea kwa sababu ya kusikia sauti yake katika dhamiri zao. Ndugu zangu wapendwa, katika Maandiko mtajazwa na Roho ya Bwana ambaye ni roho ya Hekima na Ufahamu, roho ya Shauri na Uweza, roho ya Maarifa na kumcha Bwana. Na furaha yako itakuwa ni katika kumcha Bwana (Isa 11:1-3)
3. TUNAPOSIKILIZA NENO LA MUNGU, LINA MAMBO MATATU MUHIMU SANA MAISHANI MWETU.
1. Neno la Mungu ni kama MBEGU: Yesu mwenyewe alisema hivyo katika Injili. Neno la Mungu linapooteshwa moyoni mwa mtu lina nguvu ya ajabu: “Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, [kwa ajili ya watu wote wenye mapenzi mema na dhamiri safi bila kujali dini au dhehebu lake], na yanafaa katika
· Kufundisha ukweli, Kuonya, Kusahihishana makosa, Kuwaongoza watu waishi maisha ya adili, ili mtu anayemtumikia Mungu awe mkamilifu na tayari kabisa kufanya kila tendo jema” [2Tim 3:16-17].
Inafaa kama tukirudia somo la pili kutoka waraka kwa Waebrania, tukilisoma katika hali ya kutafakari:
Neno la Mungu lina ukali kuliko upanga uwao wote, ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho na viungo na mafuta…ndiyo kusema Neno la Mungu linabeba nguvu ya Mungu ndani yake.
Neno la Mungu sharti lizae matunda ndani yetu. Kwa bahati mbaya mtu binafsi anaweza kuzuia Neno la Mungu lisizae matunda tarajiwa. Mahali pengine hata jumuiya imeshiriki kulifanya Neno la Mungu lisizae matunda. Tuwajibike kupalilia roho zetu, tukizinyeshea kwa Neema zitokanazo na Sakramenti ili Neno hilo lizae nyingine 100, nyingine 60 na nyingine 30.
2. NENO LA MUNGU NI KAMA HAKIMU: Hakimu ni mtu anayechunguza na kutathimini kwa makini kile alichosema au kutenda mtu ili kubaini kama mhusika ni mkosaji au mtu huru na safi. Mara kadhaa, tusikiapo Neno la Mungu kama dhamiri zetu ni hai, Neno hilo hutusuta. Katika mwanga wa Neno la Mungu tunatambua kuwa mara kadhaa tumeenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Katika hilo tunajisikia kuwa mbele ya mahakama naye hakimu akitusomea hukumu yetu. Neno la Mungu linahukumu siyo tu maneno na matendo yetu bali pia mawazo na makusudi ya mioyo yetu.
Katika Barua yake, Yakobo anatuambia kwamba Neno la Mungu ni kama kioo: “Kwa sababu mtu akiwa ni msikilizaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama anayejiangalia uso wake kwenye kioo [Yak 1:23].
Tunapokuwa mbele ya kioo, tunajiona vile tulivyo. Kioo kinatusaidia kuona kama uso na nguo zetu ni safi na nadhifu au la. Vivyo hivyo tunaposikia Neno la Mungu, Roho wa Mungu ndani yetu, anatualika kuchunguza kwa kina kama maisha yetu yanalandana na kile kinachoagizwa na Neno la Mungu, ili tubaki waaminifu kwa Bwana wetu Yesu Kristo
Kwa bahati mbaya, kama asemavyo Yakobo, tunaziweka kando dhamiri zetu na kujidai kusahau kile ambacho kinatusuta katika KIOO cha Neno la Mungu na kwenda mbali na kioo hicho. Yakobo anasema, mtu asiye na hekima: “Hujiangalia, kisha huenda zake mara akasahau jinsi alivyo.”[Yak 1:24]. Huenda siku moja tukajutia kutokujali kwetu Neno la Mungu.
3. TUNAPOSIKILIZA NENO LA MUNGU, KRISTO ANAKUWA HAKIMU WETU NA KIOO CHETU.
Tumesema hapo juu kuwa Kristo yupo wakati Neno la Mungu linasomwa na kuhubiriwa, ndiyo kusema, ni yeye anaongea nasi kwa Neno lake. Barua kwa Waebrani inatueleza kwamba “Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote ni utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.” [Ebr 4:13].
Mtu kipofu, akisikia mtu anaongea pembeni yake, ingawa hamwoni mtu huyo akiongea, kipofu huyu anatambua kuwa yule anayeongea anamwangalia. Wakati huu Yesu ameyaelekeza macho yake kwetu na anaona mpaka moyoni mwetu. Hatuwezi kujificha wala kuficha kitu kwake kwani anatuona vyema kabisa.
Tumebakiwa na njia mbili mbadala:
· Au kupiga magoti miguuni pake, chini ya mbawa zake, tukiomba mwanga na nguvu tuliyopungukiwa ya kuishi kadiri ya Neno lake.
· Au kumkimbia yeye na kubaki katika hali yetu ya giza na dhambi!
Tuwe na hekima na busara katika kufuata ushauri wa Kristo kadiri ya Neno lake kwani Yeye ni Njia Ukweli na Uzima.
UTAJIRI NI KIKWAZO KWA NENO LA MUNGU KUZAA MATUNDA NDANI YETU
Mt. Paulo alimwandikia Timotheo na kusema: “Kweli, [utauwa] Dini humfanya mtu awe tajiri sana, ikiwa anatosheka na vitu alivyo navyo, maana hakuleta kitu chochote hapa duniani wala hatachukua kitu chochote. Kwa hiyo basi kama tunacho chakula na mavazi inafaa kuridhika. Lakini wale wanaotaka kutajitrika huanguka katika majaribu, na kunaswa katika mtego wa tamaa nyingi mbaya za kipumbavu, ambazo huwavuta mpaka kwenye uharibifu na maangamizi.” [1 Tim 6:6-9]. “Kupenda mno na kujihusisha kupita kiasi na mali za dunia ni kipingamizi cha kufikia utawala wa Mbinguni”
Injili inatupa mfano wazi jinsi utajiri unavyoweza kuwa kikwazo kwa wokovu wa wengi. Tunakutana na kijana wa umri kati ya miaka 17-18 hivi aliyejisikia kuvutwa na Yesu. Kwa heshima kubwa anamwendea Yesu akampigia magoti na kumwuliza: “Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?” [Mk 10:17].
Kijana huyu anasema nifanye nini nipate “Kuurithi” uzima wa milele. Hasemi nifanye nini ili nipate kuutawala, kustahili au kupata uzima wa milele. Anatambua kuwa si matunda ya jitihada zetu. Urithi ni zawadi, ni tunda la majitoleo ya wengine. Kwa hiyo uzima wa milele siyo mastahili ila ni zawadi kutoka kwa Baba kwa wanawe.
Swali lake lilikuwa la mtu aliyeguswa na wema wa Bwana Yesu, akivutwa kufuata njia yake. Jibu la Yesu ni la pekee. Yesu anamtajia vigezo. Cha kushangaza ni kwamba anamwambia azisheke Amri. Amri anazoambiwa azisheke ni kuanzia Amri ya 4-10. kwa nini Yesu hataji juu ya Amri ya 1-3 ambazo zinamhusu Mungu? Yesu anamwambia inatosha kudhihirisha upendo wako kwa Mungu kadiri unavyohusiana na jirani yako! Alipoambiwa anapaswa kuzishika Amri, kijana huyu alimjibu Yesu kuwa “Haya yote nimejitahidi kuyashika tangu utoto wangu.
Kijana huyu hakuwa anajisifia bali alikuwa akieleza kile alichokifanya kwa moyo radhi. Je, maelezo yake yanapingana na kile anachosema Yohani kuwa: “Tukisema kuwa hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo ndani yetu!” 1Yn 1:8.
Ukweli ni kwamba kijana huyu ana mtazamo chanya juu yake. Si mtu wa kujilaani na kujihukumu. Huenda ana makosa lakini ile shauku ya kumfuasa Kristo na kuwa mkamilifu inamsukuma atafute msaada zaidi, ndiyo maana Yesu alimkazia macho, akampenda. Yesu aliona ishara na kiu ya Utakatifu ndani ya kijana huyu, ndiyo maana anampa miongozo zaidi ya kufikia ukamilifu. [Mk 10:21].
Yesu anampa kijana huyu siyo amri bali ushauri wa kwenda kutoa sadaka: Nenda kauze ulivyo navyo vyote kisha uwape maskini, kisha njoo unifuate. Yesu alikuwa anataka kumwambia huyu ndugu kuwa licha ya jitihada zako katika kuzishika Amri za Mungu, mali yako imekuwa kikwazo kufikia ukamilifu. Ni kama Kristo anamshauri kwamba tumia utajiri wako kuwakwamua ndugu zako masikini, wanaokufa njaa na wasio na mahitaji ya msingi. Kristo anamhakikishia kijana huyu kuwa ukiyazingatia hayo utakuwa na utajiri utoshao yaani, hazina ya thamani kubwa - Uzima wa mbinguni kitu ambacho yeye alikitamani.
Lakini kijana katika hali ya huzuni alikunja uso. Hakuwa tayari kubandukana na utajiri wake. Hakuwa tayari kupokea mwaliko wa Yesu: “Akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.”
Isingewezekana vinginevyo, kijana yule alipoondoka kwa huzuni, kwa hakika alikuwa akiachana na chanzo halisi cha furaha ya kweli. Injili haiendelei kuongea juu yake. Lakini tunaweza kuona kwamba maisha yake yalisheheni huzuni nyingi.
Ni kwa kiasi gani alipaswa kufikiri nafsini mwake “Ingekuwaje kama ningetekeleza kile Yesu alichoniagiza na kuona tofauti katika maisha? Hakuna mwenye furaha ya kweli kama yuko mbali na Yesu. Yesu mwenyewe alisikitika kwamba yule kijana ameondoka na uso wa huzuni. Maneno ya Yesu kwa wanafunzi wake yanatuhusu hata sisi “Jinsi itakavyokuwa mbinguni kwa wenye mali kuingia katika Ufalme wa Mungu [Mk 10:23]
Tukiwa matajiri au Maskini, lazima tuwe na mtazamo chanya kwa yale tunayomiliki.
· milikaji siyo mbaya kwa wenyewe. Chochote tulicho nacho kiwe ni kidogo au kikubwa ni zawadi kutoka kwa Mungu. Na Mungu hatupi mambo mabaya kama zawadi
· Siyo utajiri ulio mbaya, uchoyo na tamaa inayoletwa na utajiri ndio unaofanya utajiri kuwa hatari.
TUMSIFU YESU KRISTO Wapendwa



Chapisha Maoni

 
Top