Wito na maisha ya Upadre ni neema na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kumwilishwa katika fadhila ya huruma na mapendo kwa Mungu na jirani. Tarehe 29 Juni 1951, Miaka 65 iliyopita, Joseph Ratzinger, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, alikuwa anapewa Daraja Takatifu la Upadre kwenye Jimbo kuu la Frisinga, huku akiongozwa na maneno haya yafuatayo: “Si kwamba tunatawala imani yenu; bali tu wasaidizi wa furaha yenu; maana kwa imani yenu mnasimama”.
Alipewa Daraja Takatifu la Upadre na Kardinali Michael Von Faulhaber wa Jimbo kuu la Munich. Mfuko wa Joseph Ratzinger, hapo tarehe 28 Juni 2016 kwenye Ukumbi wa Clementina, uliopo mjini Vatican, utaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 65 tangu Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipopewa Daraja Takatifu la Upadre, tukio ambalo litapambwa kwa uwepo na ushiriki wa Papa Francisko. Hii itakuwa ni siku maalum ya kutafakari kwa kina na mapana Wito na Zawadi ya Daraja takatifu. Papa mstaafu atazawadiwa kitabu maalum kilichoandikwa kuhusu Daraja Takatifu la Upadre kama sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho haya!
Papa mstaafu Benedikto XVI anasema, wakati wa kupewa Daraja takatifu la Upadre walikuwa ni Mashemasi 40 na kila mmoja wao aliitwa kwa jina na kuitika, tayari kupiga moyo konde kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani kwa kusema, “Adsum” “Mimi hapa”. Hii ni siku ambayo kamwe haitaweza kufutika katika akili na moyo wake alipokuwa anasikiliza sauti ya ndege waliokuwa wanatumbuiza pale Kanisani na kujisemea moyoni mwake, kwa hakika hii ndiyo njia ya haki ambayo nimejichagulia mwenyewe.
Hii ni siku anasema Papa mstaafu Benedikto XVI ambayo hata kaka yake mkubwa, Monsinyo Georg alipewa Daraja Takatifu la Upadre na wote wakaadhimisha Ibada ya Misa ya Shukrani kwenye Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Oswald. Hii ni siku iliyokuwa imesheheni furaha ya maisha na utume wa Kipadre. Walikuwa wamealikwa kupita katika nyumba mbali mbali ili kutoa baraka za Kipadre zilizokuwa zinabubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Waamini na majirani zao, walikuwa wanamwona Kristo mwingine katika maisha na utume ambao walikuwa wamekabidhiwa na Kristo Yesu, ili kutakatifuza, kuongoza na kuwafundisha watu wa Mungu.
Papa mstaafu Benedikto XVI anakumbusha kwamba, Upadre ni Sakramenti ambayo Mwenyezi Mungu anamtumia mwanadamu hata katika udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu, ili kuwahudumia waja wake. Tema ya Daraja takatifu ndiyo ambayo imebeba uzito wa juu katika “Kitabu cha XII cha Kazi ya Joseph Ratzinger” maarufu kama “Volume XII dell’ Opera Omnia di Joseph Ratzinger” kinachojulikana kama “Watangazaji wa Neno la Mungu na Wahudumu wa furaha yenu”. Ni kitabu ambacho ni mkusanyiko wa machapisho 80 yanayozungumzia kwa kina na mapana Wito na Zawadi ya Daraja Takatifu la Upadre. Kitabu hiki kinachambua na kupembua taalimungu na tasaufi ya Daraja Takatifu la Upadre. Kina sheheni kwa namna ya pekee mahubiri kuhusu Uaskofu ambao ni utimilifu wa Daraja Takatifu ambalo kimsingi limegawanyika katika hatua kuu tatu: Uaskofu, Upadre na Ushemasi. Haya ni matunda ya kazi na mikono ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedito XVI katika maisha na utume wake kama: Padre, Askofu, na Kardinali, tangu mwaka 1954 hadi mwaka 2002.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni